

Chadema yashinda mahakamani, yaendelea kudai Sh500 milioni za ruzuku
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata ushindi Mahakama Kuu baada ya kutupwa kwa shauri dogo la maombi ya zuio lililolenga kukizuia kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama hadi kesi ya msingi kuhusu mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali ndani itakapoamuliwa.
Wakati kikipata ushindi huo, Chadema inaendelea kufuatilia malimbikizo ya ruzuku ya Sh500 milioni ya Juni hadi Oktoba 2025, huku Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikikitaka kuwa na subira wakati suala hilo likishughulikiwa.
Fedha hizo zinahusishwa na uwakilishi wa Chadema bungeni.
Chadema yashinda shauri la zuio
Ushindi wa Chadema umetokana na uamuzi uliotolewa leo, Alhamisi, Oktoba 22, 2026, na Jaji Awamu Mbagwa wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Katika uamuzi huo, Mahakama ilitupa shauri dogo la maombi ya zuio baada ya kubaini kuwa waombaji wameshindwa kuthibitisha vigezo vyote vinavyohitajika ili Mahakama itoe amri hiyo.
Shauri hilo lilitokana na kesi ya madai namba 13832 ya mwaka 2026 inayohusu mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali ndani ya Chadema kati ya upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na Ahmed Rashid Khamis, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutoka Zanzibar.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kupitia shauri dogo hilo, waombaji walikuwa wameiomba Mahakama itoe amri ya muda ya kuwazuia walalamikiwa kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Vigezo vya zuio havikuthibitishwa
Katika uamuzi wake, Jaji Mbagwa amesema ili Mahakama iweze kutoa amri ya zuio, mwombaji anapaswa kuthibitisha vigezo vitatu.
Kigezo cha kwanza ni kuwepo kwa hoja inayobishaniwa au mgogoro unaohitaji kuamuliwa na mahakama. Kigezo cha pili ni kuwepo kwa madhara ambayo mwombaji anaweza kuyapata iwapo amri hiyo haitatolewa, huku kigezo cha tatu kikiwa ni kwamba madhara hayo hayawezi kufidiwa.
Jaji Mbagwa amesema waombaji walifanikiwa kuthibitisha kigezo cha kwanza, yaani kuwepo kwa mgogoro, lakini walishindwa kuthibitisha vigezo vingine viwili.
Kutokana na kushindwa huko, Mahakama iliona kuwa hakuna msingi wa kutoa amri ya zuio waliyoomba na hivyo kulitupilia mbali shauri hilo dogo.
“Sioni kigezo cha kuifanya Mahakama ilazimike kutoa amri ya zuio katika hatua hii. Hivyo waombaji wameshindwa kukidhi vigezo vya kuifanya Mahakama itoe amri ya zuio. Kwa maombi haya, hayana mashiko na mahakama hii inayatupilia mbali,” amesema Jaji Mbagwa.
Katika kesi ya msingi walalamikaji wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Madai mengine ni ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Awali kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo na Mohamed, Khamis na Maulida Anna Komu (marehemu kwa sasa), ambaye pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Chadema kutoka Zanzibar.
Pia, walifungua shauri la maombi madogo ya zuio la muda dhidi ya walalamikiwa wakiomba mahakama iwazuie kufanya shughuli za siasa na kutumia mali za chama kusubiri kuamuliwa kwa kesi hiyo.
Juni 10, 2025, Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Hamidu Mwanga aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo alikubaliana na maombi hayo baada ya kuyasikiliza upande mmoja kutokana na wakili wa wajibu maombi hao (walalamikiwa) kujiondoa siku hiyo kwenye kesi hiyo.
Hivyo, alitoa amri ya zuio dhidi ya chama hicho kupitia kwa walalamikiwa hao, kutokujihusisha na shughuli za kisiasa wala kutumia mali za chama kusubiri uamuzi wa kesi hiyo.
Hata hivyo, amri hiyo ilibatilishwa na Mahakama ya Rufani Aprili 15, 2026 baada ya kutumia mamlaka yake kufanya mapitio ya kesi hiyo pamoja na mashauri madogo yaliyotokana na kesi hiyo, kufuatia barua iliyoandikwa na Chadema wakilalamikia mwenendo wa kesi na mashauri hayo.
Katika uamuzi huo, Mahakama ya Rufani ilisema baada ya wakili wa wajibu maombi kujiondoa Mahakama kuwa haikuwa sahihi kuendelea na usikilizwaji wa maombi hayo upande mmoja na kwamba wajibu maombi kutokana na kutokuwa na wakili wa kuwawakilishwa walinyimwa haki ya kusikilizwa.
Hivyo, ilibatilisha mwenendo wa shauri hilo kuanzia pale wakili wa wajibu maombi alipojitoa mpaka uamuzi wa zuio hilo.
Pia, Mahakama ya Rufani iliamuru kesi isikilizwe na jaji mwingine na ikaelekeza jaji huyo aanze kusikiliza na kuamua kwanza pingamizi la walalamikiwa.
Katika pingamizi hilo walalamikiwa walikuwa wakidai kuwa kesi hiyo haipaswi kusikilizwa, wakidai kuwa imefunguliwa nje ya muda kinyume na Sheria ya Ukomo wa Muda, kutokana na hati ya madai kutokubainisha muda ambao mambo waliyokuwa wakiyalalamikia yalitokea.
Pingamizi hilo lilisikilizwa na Jaji David Ngunyale Mei 20 na Mei 28, 2026, katika uamuzi wake alikubaliana na hoja ya Chadema kuwa hati ya madai haibainishi kuwa mambo wanayolalamikia yalianza lini jambo ambalo alisema linaifanya mahakama ishindwe kuona kama ina mamlaka ya kuisikiliza au la.
Hivyo, kutokana na kasoro hiyo, jaji Ngunyale aliitupa kesi kabla ya kuisikiliza madai ya msingi.
Hata hivyo, siku chache tu baada ya kesi hiyo kufutwa wadai hawa wawili walirudi mahakamani hapo, walifungua upya kesi hiyo baada ya kurekebisha kasoro za kisheria zilizobainishwa na mahakama, na wakafungua tena maombi hayo ya zuio.
Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 22, 2026, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesisitiza kuwa bado suala la ruzuku ya Chadema linafanyiwa kazi, akieleza kuwa, mwaka wa fedha ukiisha fedha zinarudi Hazina, hivyo lazima ziombwe upya.
“Bado tunalifanyia kazi, siwezi kusema tumefikia wapi, lakini waliomba (Chadema) suala lao bado linafanyiwa kazi,” ameeleza Nayahoza.
Mara ya mwisho Juni 18, 2026 Nyahoza, alisema Chadema iliwasilisha barua ya kudai fedha hizo na kuwaeleza kuwa suala lao linashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
“Fedha za ruzuku hazikai tu katika Ofisi ya Msajili; hutolewa na Hazina na kupelekwa kwa chama husika. Hivyo, si sahihi kusema fedha hizo zipo ofisini tu, kwa kuwa ni lazima kwanza tuziombe kutoka Hazina,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Bara, Amani Golugwa amesema hadi sasa bado hawajapata mwelekeo kuhusu fedha zao za ruzuku.
“Kwa nyakati tofauti tumeandika barua tatu za kukumbushia, kati ya hizo moja ndio iliyojibiwa, lakini hatujapata mrejesho unaoeleza fedha zitawekwa lini kwenye akaunti ya chama,” amesema Golugwa.
Nyongeza na Bakari Kiango
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply