

Dalili za kumtambua mwenza laghai
Katika baadhi ya uhusiano, mtu anaweza kuanza kupoteza kujiamini bila kuelewa chanzo cha mabadiliko hayo.
Anaomba msamaha mara kwa mara, anaogopa kueleza hisia zake na hujikuta akibadilisha tabia ili kumfurahisha mwenza wake, hata pale ambapo hajaelewa kosa alilofanya.
Hali hiyo inaweza kumfanya ajiulize, “Je, tatizo ni mimi?” Kadiri siku zinavyopita, anaweza kuanza kuamini kwamba kila mgogoro unatokana na makosa yake, huku mahitaji na hisia za mwenza wake zikipewa kipaumbele.
Mabadiliko hayo yanaweza kuwa miongoni mwa ishara za ulaghai wa kihisia, unaojulikana kwa Kiingereza kama emotional manipulation. Hii ni hali ambayo mtu hutumia lawama, hofu, hisia au mbinu nyingine kushawishi mwenza wake afanye mambo kwa namna anayoitaka.
Hata hivyo, si kila kutoelewana, ugomvi au kutofautiana kwa maoni katika uhusiano ni ulaghai. Watu wanaweza kukosea, kujitetea au kushindwa kueleza hisia zao vizuri. Kinachopaswa kuangaliwa ni tabia inayojirudia na kuanza kumdhibiti mwenza au kumfanya ajione hana thamani.Zifuatazo ni dalili nne zinazoweza kusaidia kutambua hali hiyo.
Mojawapo ya ishara za ulaghai wa kihisia ni mtu kushindwa kuwajibika kwa makosa yake na badala yake kumfanya mwenza aonekane ndiye chanzo cha tatizo.
Kwa mfano, mtu anapofanya jambo linalomuumiza mwenza wake, anapoulizwa kuhusu kitendo hicho anaweza kujibu: “Kama usingenikasirisha, nisingefanya hivyo,” au “Wewe ndiye uliyenifanya nifanye hivyo.”
Badala ya kukubali kosa na kutafuta namna ya kurekebisha hali, anahamisha mjadala kutoka kwenye kitendo chake na kuuelekeza kwenye tabia ya mwenzake.
Katika uhusiano yenye afya, kila mtu anapaswa kuwajibika kwa matendo yake. Kuomba msamaha kunapoambatana na kukubali kosa na kufanya juhudi za kubadilika, kunaweza kusaidia kurejesha uaminifu.
Hisia zake ni muhimu kuliko zako
Uhusiano unahitaji kusikilizana, kusaidiana na kutambua mahitaji ya kila mmoja. Hata hivyo, wakati mwingine uhusiano unaweza kugeuka kuwa wa upande mmoja, ambapo hisia za mtu mmoja hupewa nafasi huku za mwingine zikipuuzwa.
Mwenza wako anapokuwa na changamoto, unamsikiliza na kumpa faraja. Lakini unapohitaji msaada, anaweza kubadilisha mazungumzo na kuanza kueleza matatizo yake. Unaposema umechoka au una jambo linalokusumbua, anakujibu kwamba unalikuza tatizo au kwamba halina umuhimu.
Wakati huohuo, changamoto zake zinapotokea, anatarajia usimame na kumpa muda na uangalizi anaohitaji.
Tofauti hiyo ikijirudia inaweza kuashiria kwamba mahitaji ya mmoja yanatawala uhusiano. Mwenza anayejali si lazima awe na majibu ya kila tatizo, lakini anapaswa kuwa tayari kusikiliza, kutambua hisia za mwenzake na kuonyesha kujali.
Anakufanya utilie shaka uwezo wako
Dalili nyingine ni mwenza kutumia maneno yanayodhoofisha kujiamini kwa mwenzake, hasa pale anapotoa maoni, kueleza maumivu au kuweka mipaka.
Kwa mfano, unaposema jambo limekuumiza, anaweza kukuambia, “Unafikiria sana.” Ukipinga uamuzi fulani, anasema, “Wewe ni mtu wa matatizo.” Unapojaribu kuweka mipaka, anadai umebadilika au humjali tena.
Maneno kama hayo yakijirudia yanaweza kumfanya mtu aanze kuogopa kuzungumza, kutoa maoni au kufanya maamuzi. Anaweza kuhisi kwamba kila anachosema kitatafsiriwa kuwa kosa.
Hali hii inahitaji umakini kwa sababu uhusiano mzuri unapaswa kuruhusu watu kutofautiana bila kudhalilishana. Kutokubaliana hakumpi mtu ruhusa ya kumshambulia mwenzake au kumfanya ajione hana uwezo wa kufikiri.
Anataka uangalizi lakini hataki kutoa
Kila mtu anahitaji upendo, muda na uangalizi katika uhusiano. Hata hivyo, changamoto hutokea pale mtu anapotaka mahitaji yake yatimizwe kila wakati huku akipuuza mahitaji ya mwenza wake.
Fikiria mwenza anayotarajia uache shughuli zako anapougua au anapokuwa na tatizo. Anataka umsikilize, umsaidie na uwe karibu naye. Lakini unapopitia kipindi kigumu na kuomba msaada, anatoa jibu fupi kisha anaendelea na shughuli zake bila kuonyesha kujali.
Hali hiyo ikijirudia inaweza kuonyesha kutokuwapo kwa usawa katika uhusiano. Mtu mmoja anakuwa na matarajio makubwa kwa mwenzake, lakini hataki kuwajibika kwa namna hiyo hiyo.
Tafakari kabla ya kufanya uamuzi
Kumtambua mwenza anayetumia hisia kumdhibiti mwingine kunahitaji kuangalia mwenendo wa muda, si tukio moja pekee. Ni muhimu kujiuliza kama mara nyingi kila tatizo huishia kuwa kosa lako, kama unaogopa kueleza hisia zako, kama unaomba msamaha bila kuelewa kosa au kama mahitaji yako hayapewi nafasi.
Majibu ya maswali hayo yanaweza kusaidia kutathmini hali ya uhusiano. Ikiwa tabia hizo zinajirudia na kuathiri ustawi wako, zungumza na mtu unayemwamini au mshauri wa uhusiano. Pale ambapo kuna vitisho, udhibiti mkali au hofu ya usalama, kutafuta msaada unaofaa ni muhimu.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply