

Dodoma yakabiliwa na upungufu wa maji lita milioni 68 kwa siku
Dodoma. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa) imeeleza kuwa jiji hilo linakabiliwa na upungufu wa lita milioni 68 za maji kwa siku, hali inayosababisha baadhi ya wakazi kuendelea kupata huduma hiyo kwa mgao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Oktoba 26, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Aaron Joseph, amesema kuwa mahitaji ya maji yamefikia lita milioni 159.9 kwa siku, lakini mamlaka hiyo inazalisha lita milioni 91 pekee, sawa na takribani asilimia 57 ya mahitaji yote.
Amesema ongezeko la watu upanuzi wa makazi na shughuli za kiuchumi, pamoja na Serikali kuhamia Dodoma, vimeongeza mahitaji ya maji kwa kasi kuliko uwezo wa uzalishaji.
“Kwa sasa tunazalisha takribani lita milioni 91 kwa siku, wakati mahitaji ni lita milioni 159.9. Hii ina maana tuna upungufu wa lita milioni 67 hadi 68 kwa siku, ndiyo sababu tunaendelea kutoa huduma kwa utaratibu wa mgao,” amesema Joseph.
Amesema kabla ya Serikali kuhamia Dodoma, uzalishaji ulikuwa lita milioni 61.5 kwa siku, huku mahitaji yakiwa lita milioni 48, lakini hali imebadilika kutokana na kukua kwa jiji.
Kwa mujibu wa Joseph, ifikapo mwaka 2030 mahitaji yanatarajiwa kufikia lita milioni 180 kwa siku, jambo linalohitaji uwekezaji mkubwa katika vyanzo vipya na miundombinu ya usambazaji maji.
Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, Duwasa imeandaa miradi yenye thamani ya takribani Sh51 bilioni inayolenga kuongeza uzalishaji kutoka lita milioni 91 hadi angalau milioni 121 kwa siku.
Miongoni mwa miradi hiyo ni wa Mji wa Serikali wenye thamani ya Sh35 bilioni unaohusisha uchimbaji wa visima, ujenzi wa matanki na uwekaji wa mabomba yenye urefu wa zaidi ya kilomita 60.
Amesema mradi huo umefikia asilimia 40 ya utekelezaji na unatarajiwa kuongeza uzalishaji kwa zaidi ya lita milioni 10 kwa siku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Aaron Joseph, akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 26, 2026 Jijini Dodoma
Pia, mradi wa Nzuguni awamu ya pili wenye thamani ya Sh4.7 bilioni unalenga kuboresha huduma katika maeneo ya Nzuguni, Ilazo, Ipagala, Daraja Dogo, Swaswa, Mnarani na sehemu za Mpamaa na Kisasa.
Joseph amesema mradi huo umefikia takribani asilimia 40 na unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji ndani ya miezi sita hadi saba ijayo.
Miradi mingine ni Zuzu-Miganga, unaotarajiwa kuongeza uzalishaji kwa lita milioni 12 hadi 15 kwa siku, pamoja na miradi ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Nala.
Amesema kwa muda wa kati, Serikali inaendelea na hatua za utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Farkwa, unaotarajiwa kuipatia Dodoma angalau lita milioni 128 za maji kwa siku baada ya kukamilika kwa miundombinu inayohitajika.
Aidha, mkakati wa muda mrefu unahusisha kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Singida hadi Dodoma.
Pamoja na mikakati hiyo, Joseph amewataka wananchi kulinda miundombinu ya maji, akisema mita 103 zimeibwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, hali inayosababisha usumbufu na gharama za ziada.
Amesema Duwasa itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine kuboresha huduma, huku akisisitiza kuwa ongezeko la uzalishaji ni muhimu ili kupunguza mgao na kukidhi mahitaji ya jiji yanayoongezeka.
Naye mkurugenzi wa usambazaji maji wa Duwasa, Bernard Rugayi amesema Mamlaka hiyo inawekeza kwenye visima vipya vya maji ambayo ni hatua ya muda mfupi ya kukabiliana na uhaba wa maji, huku wakisubiri mradi wa muda mrefu wa kutoa maji ziwa Victoria ambalo litamaliza mgao wa maji Jijini Dodoma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa Duwasa, Lenna Mwakisale amesema kwa kipindi cha Julai hadi June mwaka 2025 wamepokea jumla ya malalamiko 12,336 ambapo mengi yalifanyiwabkazi isipokuwa malalamiko 177 ambayo yalikuwa ya malalamiko ya wananchi kukosa maji hasa maeneo ambayo yna uhaba mkubwa wa maji
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply