

Epuka mambo yanayomfanya mtoto ajione hana thamani
Dar es Salaam. Katika maisha ya mtoto, familia ndiyo sehemu ya kwanza anayojifunza kutambua thamani yake, kujenga kujiamini na kuelewa namna anavyopaswa kuhusiana na watu wengine.
Hata hivyo, baadhi ya wazazi, bila kutambua athari zake, wamekuwa wakitumia mbinu za malezi zinazoweza kuwafanya watoto wajione hawafai au hawana uwezo kama wenzao.
Kwa mfano, mzazi anaweza kushindwa kushiriki katika mahafali ya mtoto, kupuuza mafanikio yake ya masomo, kumlinganisha na watoto wengine anapokosea au kumkosoa mara kwa mara bila kutambua juhudi anazofanya.
Ingawa wakati mwingine tabia hizo hutokana na shughuli nyingi, matarajio makubwa au nia ya kumrekebisha mtoto, zinapojirudia zinaweza kumfanya ajihisi kuwa hapewi kipaumbele katika familia yake.
Hat hivyo, swali la msingi kwa wazazi la kujiuliza ni hili; Je, namna wanavyowalea watoto wao inawasaidia kutambua uwezo wao au inawajengea hisia za kutokuwa na thamani?
Katika hatua za ukuaji, watoto hutegemea kwa kiasi kikubwa namna wanavyotendewa na watu wanaowalea ili kuelewa kama wanapendwa, wanakubalika.
Mzazi anapomtambua mtoto kwa juhudi zake, kumsikiliza na kumtia moyo anapokumbana na changamoto, humsaidia kujenga kujiamini. Kinyume chake, mtoto anapokosolewa kila mara, kudharauliwa au kuonyeshwa kuwa wenzake wanathaminiwa na wazazi wao, yeye anaweza kuanza kuamini kuwa hapendwi n anatengwa.
Kwa mfano, mtoto anapopata matokeo mazuri shuleni lakini mzazi akashindwa hata kumpongeza au kufika kwenye matukio yay eye kusherehekea na wenzake sambamba na wazazi wao, atanyongea na kumfanya aone kuwa hawezi kumridhisha mzazi wake hata anapofanya mazuri.
Baadhi ya watoto wanaweza kuanza kuogopa kujaribu mambo mapya kwa kuhofia upweke.
Hali hii mara nyingi pia huwa inashuhudiwa katika mahafali na matukio mengine muhimu.
Ni miongoni mwa nyakati ambazo watoto hutamani kushiriki furaha yao na watu wanaowapenda.
Mzazi anaposhindwa kuhudhuria matukio hayo bila kumweleza mtoto sababu au kutafuta namna nyingine ya kuonyesha kujali, mtoto anaweza kuhisi kuwa mafanikio yake hayana umuhimu kwa familia.
Hata hivyo, kutohudhuria tukio moja hakumaanishi moja kwa moja kuwa mzazi hampendi mtoto. Changamoto hujitokeza pale ambapo kutokuwepo, kutotambua mafanikio na kutompa mtoto nafasi ya kueleza hisia zake vinapokuwa mwenendo wa kawaida.
Ni muhimu wazazi kuelewa kuwa watoto hawahitaji zawadi za gharama kubwa ili wajione wanathaminiwa. Wakati mwingine, uwepo wa mzazi, pongezi za dhati na muda wa kuzungumza nao vinaweza kuwa na maana kubwa.
Baadhi ya wazazi huamini kuwa kumlinganisha mtoto na wenzake kutamhamasisha kufanya vizuri zaidi. Hata hivyo, mbinu hiyo inaweza kuleta matokeo tofauti, hasa inapofanywa kwa maneno ya kumdhalilisha.
Kauli kama, “Angalia mwenzako anavyofaulu, wewe kila siku unashindwa,” humwelekeza mtoto kujiona kwa kuzingatia mafanikio ya wengine badala ya kutambua uwezo wake na maeneo anayopaswa kuboresha.
Ni bora mzazi azungumze na mtoto kuhusu changamoto alizonazo, amsaidie kuweka malengo yanayowezekana na kumpongeza anapoonyesha maendeleo. Kila mtoto ana vipaji, uwezo na kasi yake ya kujifunza.
Kwa sababu kwanza, mzazi anapaswa kujifunza kumsikiliza mtoto bila kupuuza hisia zake. Mtoto anaposema ameumia kwa jambo fulani, mzazi anaweza kumruhusu kueleza kilichotokea kabla ya kutoa ushauri au kumrekebisha.
Pili, anatakiwa kutambua juhudi na mafanikio ya mtoto, hata kama ni madogo. Pongezi za kweli humsaidia kuelewa kuwa jitihada zake zinaonekana na kuthaminiwa.
Tatu, mzazi anapaswa kurekebisha makosa bila kumshambulia mtoto kama mtu. Badala ya kumwita mvivu au asiye na akili, anaweza kueleza kosa lililofanyika na namna ya kulirekebisha.
Hivyo ni muhimu kuonyesha upendo usiotegemea matokeo. Mtoto anapaswa kuelewa kuwa bado anapendwa hata anapofeli mtihani, anapokosea au anaposhindwa kufikia matarajio fulani.
Kwa kuwa malezi ni zaidi ya kumpatia mtoto mahitaji, kumlea hakumaanishi kumpatia chakula, mavazi, ada na makazi pekee.
Pia kunahusisha kumsaidia kujenga mtazamo chanya kuhusu nafsi yake ikiwamo kumpa furaha ya kweli.
Mtoto anayekua katika mazingira ya upendo, heshima na kutiwa moyo hupewa nafasi ya kujenga kujiamini na kujitambua.
Huo ndio msingi wa malezi yanayomsaidia kukua akiwa mtu anayethamini nafsi yake na kuheshimu thamani ya wengine.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply