

Hali ya hewa kuwa hivi hadi mwishoni mwa Oktoba hii
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza uwepo wa vipindi vya mvua baadhi ya maeneo nchini hadi Oktoba 31, 2026, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA ya kipindi cha Oktoba 21 hadi 31, mvua zinatarajiwa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, magharibi mwa nchi, nyanda za juu kaskazini-mashariki na maeneo ya pwani, ingawa kiwango na usambazaji wake vitatofautiana kulingana na kanda.
TMA imesema Kanda ya Ziwa Victoria, inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara, inatarajiwa kupata vipindi vya mvua vinavyoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo.
Katika nyanda za juu kaskazini-mashariki, zinazojumuisha Arusha, Manyara na Kilimanjaro, vipindi vya mvua vinatarajiwa katika maeneo machache, hasa katika siku tano za mwisho za mwezi Oktoba.
Hali kama hiyo inatarajiwa katika ukanda wa pwani ya kaskazini, unaojumuisha Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, ambako mvua zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo, hasa katika siku tano za mwisho za kipindi hicho.
Kwa upande wa magharibi mwa nchi, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora inatarajiwa kupata vipindi vya mvua vinavyoambatana na ngurumo za radi katika maeneo machache.
Hata hivyo, TMA imeeleza uwepo wa hali ya ukavu katika Kanda ya Kati, inayojumuisha Dodoma na Singida, pamoja na Kanda ya Kusini, inayojumuisha Mkoa wa Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro.
Katika nyanda za juu kusini-magharibi, zinazojumuisha Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa, mvua nyepesi zinatarajiwa katika maeneo machache.
Aidha, mikoa ya Lindi na Mtwara inatarajiwa kupata vipindi vya mvua katika maeneo machache, hususan katika siku tano za mwisho za Oktoba.
TMA imeeleza mwenendo huo wa mvua unahusishwa na mabadiliko ya mifumo ya migandamizo ya hewa katika ncha za kaskazini na kusini mwa dunia, pamoja na hali ya joto la uso wa bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, migandamizo mikubwa ya hewa ya Azore na Siberia iliyopo kaskazini mwa dunia inatarajiwa kuendelea kuimarika, huku ile ya St. Helena na Mascarene iliyopo kusini mwa dunia ikitarajiwa kudhoofika.
Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuifanya sehemu ya ukanda wa mvua unaojulikana kama ITCZ kuendelea kubaki kusini, huku ukiwa katika maeneo ya Ziwa Victoria na magharibi mwa nchi.
Vilevile, joto la bahari katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi, karibu na pwani ya Afrika Mashariki, linatarajiwa kuwa juu ya wastani ikilinganishwa na eneo la mashariki mwa bahari hiyo, karibu na pwani ya Indonesia.
TMA imesema hali hiyo inatarajiwa kuimarisha upepo wenye unyevunyevu kutoka baharini kuelekea ukanda wa pwani na nyanda za juu kaskazini-mashariki, hivyo kuimarisha mifumo inayosababisha mvua katika maeneo hayo.
You may also like


Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade


Leave a Reply