

Japan yakabidhi magari 16 ya doria kwa nchi za EAC
Arusha. Serikali ya Japan imekabidhi magari 16 ya doria kwa nchi nane wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa lengo la kuimarisha usalama mipakani, kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka na kurahisisha biashara halali.
Magari hayo aina ya Pickup, mawili kwa kila nchi, yametolewa kupitia ufadhili wa Japan na kutekelezwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS), chini ya mradi unaolenga kuimarisha usalama wa mipaka na kuboresha mazingira ya biashara na forodha katika ukanda huo.
Nchi zilizonufaika ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika jijini Arusha, leo Ijumaa Oktoba 23, 2026, yamefuatia tathmini ya kitaalamu iliyofanyika katika vituo 16 vya mipakani na kubaini ukosefu wa vyombo vya usafiri kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri operesheni za usalama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa EAC, Stephen Mbundi, amesema magari hayo yataongeza uwezo wa vyombo vya usalama kukabiliana na magendo, usafirishaji haramu wa binadamu na aina nyingine za uhalifu wa kuvuka mipaka.
Amesema pia magari hayo yatasaidia kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo ya mipakani.
Mbundi amezitaka nchi zilizopokea magari hayo kuhakikisha yanatunzwa vizuri na kutumika kwa shughuli za ulinzi na usalama mipakani pekee.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Stephen Mbundi, akizungumza wakati wa makabidhiano ya magari 16 ya doria yaliyotolewa na Japan kwa ajili ya kuimarisha usalama mipakani na kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka, jijini Arusha.
“Usalama na urahisishaji wa biashara havipaswi kuonekana kama malengo yanayokinzana. Badala yake, mpaka salama hujenga imani inayohitajika ili biashara halali, uwekezaji na usafiri wa watu viweze kukua,” amesema.
Ameongeza kuwa usimamizi madhubuti wa mipaka ni muhimu katika kuongeza biashara baina ya nchi wanachama na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na soko la kikanda lenye watu zaidi ya milioni 300.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Japan nchini Tanzania, Jin Hashimoto, amesema msaada huo ni sehemu ya juhudi za nchi yake kuunga mkono amani, usalama na maendeleo endelevu barani Afrika.
Hashimoto amesema usimamizi wa mipaka ni changamoto kwa nchi nyingi za Afrika, kutokana na kuwepo kwa mipaka mirefu ya nchi kavu inayopakana na mataifa kadhaa jirani.
Amesisitiza kuwa udhibiti madhubuti wa mipaka unahitajika ili kuzuia shughuli haramu, kulinda usalama na kurahisisha biashara halali pamoja na usafiri wa watu.
Ameahidi kuwa Japan itaendelea kushirikiana na EAC kuimarisha usimamizi wa mipaka na maeneo mengine yenye maslahi ya pamoja.
Naye Mkurugenzi wa Ofisi za UNOPS za Afrika Mashariki na Kusini, Massimo Diana, amesema mafanikio ya mradi huo hayatapimwa kwa idadi ya magari yaliyokabidhiwa pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuimarisha usalama wa jamii na kurahisisha biashara ya kikanda.
Diana amesisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali ili kuhakikisha magari hayo yanaleta manufaa ya kudumu kwa jamii za mipakani na uchumi wa kikanda.
You may also like

Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade

Samia to inaugurate Sh700bn Government City on October 30


Leave a Reply