

Jeshi la Polisi lawasaka watuhumiwa wengine wizi wa betri za CT Scan
Simiyu. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linaendelea kuwatafuta watu wengine wanaodaiwa kuhusika na wizi wa betri 40 za mashine ya CT Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, likisema halitataja majina ya waliokamatwa kwa sasa ili kutoharibu mwenendo wa upelelezi.
Tukio hilo limeibua maswali kuhusu usalama wa vifaa vya hospitali na uwajibikaji wa watumishi katika taasisi za umma.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya uchunguzi leo Jumatano Oktoba 21, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe amesema polisi wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine kwa kutumia taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu waliokamatwa.
Amesema operesheni hiyo inalenga kuwabaini wote wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, huku jeshi hilo likiepuka kutoa taarifa zinazoweza kuathiri uchunguzi unaoendelea.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa mpya kuhusu idadi ya watu waliokamatwa tangu kutolewa kwa taarifa ya awali ya Kamanda wa Polisi Mkoa huo, wala halijataja majina ya wanaoshikiliwa.
Hata hivyo, wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea, baadhi ya wananchi wanaopata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu wamesema wameanza kuona mabadiliko katika namna wanavyopokelewa na kuhudumiwa na watumishi.
James Jilala amesema awali baadhi ya watumishi, hasa katika kitengo cha malipo, walitumia lugha kali walipowahudumia wananchi, lakini kwa sasa ameona mabadiliko katika namna wanavyozungumza na wagonjwa.
“Siku za nyuma watumishi wa hospitali hii, hasa wa kitengo cha malipo, walikuwa na lugha kali. Kwa sasa lugha imebadilika na wanatumia lugha zenye utu,” amesema.
Amesema mabadiliko hayo ni muhimu kwa kuwa hospitali ni mahali ambako wananchi wanahitaji kupokelewa kwa heshima na kupewa maelekezo yanayowawezesha kupata huduma bila kuongeza msongo wa mawazo unaoweza kutokana na hali zao za kiafya.
Mariam Mahona amesema naye amebaini mabadiliko katika namna wananchi wanavyosikilizwa wanapofika hospitalini, tofauti na hali aliyodai kuizoea hapo awali.
“Kwa sasa unasikilizwa vizuri, hakuna blabla za kipindi cha nyuma,” amesema.
Kwa upande wake, Neema Zabulon amesema, “kitendo cha watumishi wa Serikali kutimiza majukumu yao ya kitaaluma hadi aseme kiongozi mkuu si utendaji mzuri, hasa katika eneo la kutolea huduma kama hospitalini,” amesema.
You may also like


Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade


Leave a Reply