

Kaya tano kati ya 54 zilizoathiriwa mvua Ushetu zapatiwa msaada
Kahama. Kaya tano kati ya 54 zilizoathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika Kijiji cha Imalabupina, Kata ya Nyankende, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, zimepatiwa msaada wa vifaa vya ujenzi ili kurejesha makazi yao.
Mvua hiyo iliyonyesha Novemba 16, 2026, ilisababisha nyumba kadhaa kuezuliwa mapaa na nyingine kubomoka kabisa, huku baadhi ya waathirika wakikosa makazi na chakula baada ya vyakula vilivyohifadhiwa ndani ya nyumba kuharibika kutokana na maji.
Akizungumza leo Novemba 25,2026 Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyankende, Yusuph Daudi, amesema juhudi za kuwasaidia waathirika zinaendelea, ikiwemo kuwaunganisha na ndugu na majirani ili kupata hifadhi wakati wakisubiri kurejeshewa makazi yao.
Amesema tathimini iliyofanywa kwa kushirikiana na Mbunge wa Ushetu, Emanuel Cherehani, imebaini kaya tano zenye hali mbaya zaidi, ambazo zimepewa vifaa vya ujenzi.
“Jitihada za awali tuliwaunganisha hawa watu na ndugu zao na wengine tuliwaombea kwa majirani ili waweze kujistiri. Mvua hii iliezua mapaa kwa baadhi ya nyumba na nyingine zilianguka kabisa. Leo tukiwa na mbunge tumepitia na kubaini kaya tano ndizo zina hali mbaya zaidi na zimepatiwa msaada wa vifaa vya ujenzi,” amesema.
Moja ya nyumba zilizoathiriwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali iloyonyesha Novemba 16, 2026, katika kijiji cha Imalabupina kata ya Nyankende, Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama na kuathiri nyumba zaidi ya 54.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Cherehani amesema lengo ni kuwawezesha waathirika kujenga makazi ya muda mfupi ili waweze kujisitiri.
Amesema vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mabati na mbao, huku akiwataka wataalamu wa halmashauri kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ujenzi wa nyumba bora zinazoweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tumeangalia nyumba ambazo hali ni mbaya sana, hakuna hata pa kuwaweka watoto, wajawazito wanahangaika. Wananchi wabadilike sasa wajenge nyumba bora zitakazohimili mitikisiko katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Mmoja wa waathirika, Hamisi Maganga, mkazi wa Imalabupina, amesema alipokuwa shambani mvua ilianza kunyesha kwa upepo mkali, na aliporejea nyumbani alikuta nyumba zake mbili zimeanguka kabisa.
Amesema kwa sasa amelazimika kurejea kwenye nyumba ya nyasi inayovuja, huku akishukuru kwa msaada alioupata.
Ameiomba Serikali kuendelea kuwasaidia waathirika wengine ambao bado wanaishi katika mazingira magumu.
Moja ya nyumba zilizoathiriwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali iloyonyesha Novemba 16, 2026, katika kijiji cha Imalabupina kata ya Nyankende, Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama na kuathiri nyumba zaidi ya 54.
Naye Lusia Salehe amesema paa la nyumba yake liliezuliwa wakati akiwa ndani, na muda mfupi baadaye nyumba hiyo ikaanguka kabisa.
Amesema kwa sasa analazimika kuishi katika nyumba ndogo pamoja na watoto wake, huku chakula chao, ikiwemo mahindi, kikiwa kimeharibika kwa kulowana.
Kwa upande wake, Mashaka Charles ameiomba Serikali kufikisha huduma za dharura, zikiwemo mahema na chakula, kwa wananchi walioathiriwa ili kuwasaidia kujisitiri na kukabiliana na athari za mvua.
Amesema baadhi ya familia zinalazimika kulala kwa kupokezana kutokana na uhaba wa makazi, huku magodoro yakilowana na chakula kuharibika.
“Hiki ni kipindi cha mvua, kwa hiyo tunaiomba Serikali iangalie namna ya kutufikishia mahema ili tuendelee kujistiri kwa sababu mvua za namna hii zinaweza kurudi tena. Chakula kimeharibika, magodoro yamelowana, tunalala kwa kupokezana,” amesema.
You may also like

Mwabunguru alivyoibuka rais mpya Tucta katikati mgawanyiko

Tanzania PM Nchemba to lead World AIDS Day commemorations in Dodoma


Leave a Reply