

Kituo cha kulea watoto kubadili maisha ya mama lishe Mwanjelwa
Mbeya. Maisha ya mama lishe katika Soko la Mwanjelwa jijini Mbeya yanatarajiwa kubadilika kufuatia mpango wa kujenga kituo cha malezi na kunyonyeshea watoto, kitakachowawezesha kuendelea na shughuli zao za kiuchumi katika mazingira rafiki.
Hatua hiyo inafuatia Halmashauri ya Jiji la Mbeya kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, ambacho pamoja na huduma za malezi, watoto watapata elimu ya maadili kutoka kwa wataalamu.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Mbunge wa Mbeya mjini, Patrick Mwalunenge, aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akiahidi kuboresha mazingira ya wafanyabiashara, wakiwamo mama lishe.
Mwananchi ilipotembelea soko hilo Oktoba 26, 2026, ilikuta eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi huo, huku wafanyabiashara wa kuku wakihamishiwa upande mwingine na eneo la chakula likiboreshwa kwa kuwekwa meza.
Baadhi ya mama lishe wamepongeza hatua hiyo, wakisema itawapunguzia changamoto ya kulea watoto huku wakipika na kuwahudumia wateja. Hata hivyo, wameomba ujenzi uanze na kukamilika kwa wakati.
Aines Mwakilasa amesema kubeba mtoto, kumpikia chakula, kumnyonyesha na kumtuliza anapolia kunaweza kuathiri ufanisi wa biashara zao.
Muonekano wa eneo lililotengwa maalumu kwa ajili ya malezi na kunyonyeshea watoto katika soko la Mwanjelwa jijini Mbeya kuwasaidia Mama Lishe kufanya majukumu yao kwa ufanisi.
“Watoto tunawapenda na hakuna anayeweza kuchoka kubeba mwanaye, lakini kuna muda wanasumbua, huku unapika, unanyonyesha, mara umbebe kumbembeleza asilie ni shida sana,” amesema.
Amesema kituo hicho kitawasaidia kufanya kazi katika mazingira bora na safi, huku akisisitiza umuhimu wa mradi kukamilika haraka.
Batilda Methew amesema huduma hiyo itawapa nguvu ya kuendeleza biashara zao, kuongeza kipato na kuvutia wateja.
“Tunashukuru kwa hatua hii, japokuwa hatujafahamu kama tutalipia kulaza watoto wetu au ni bure, lakini tunaamini hali ya biashara itabadilika na kuvutia wateja, ushindani utaongezeka,” amesema.
Kwa upande wake, James Mbeki amesema kituo hicho kitawanufaisha pia wateja kwa kupunguza muda wa kusubiri huduma.
Amesema mama lishe anapokuwa akipika huku amembeba au akimnyonyesha mtoto, wakati mwingine mteja hulazimika kusubiri kwa muda mrefu.
Katibu wa Taasisi ya Lete Mabadiliko Chanya (LeMaCHu) Mkoa wa Mbeya, George Henry, amesema kituo hicho kitasaidia kuboresha mazingira ya soko na usalama wa watoto.
Ameshauri huduma hiyo isambazwe katika masoko mengine kwa kuwa mahitaji ya vituo vya malezi ni muhimu kwa wafanyabiashara wenye watoto wadogo.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mwalunenge amesema uamuzi wa kujenga kituo hicho ulitokana na kutembelea masoko mbalimbali na kubaini changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
Amesema ujenzi unatarajiwa kuanza kabla ya Novemba 15, 2026, huku kituo kikiwa na uwezo wa kuhudumia watoto 150 kwa siku.
Ameeleza kuwa watoto watapata malezi kutoka kwa wataalamu wa ustawi wa jamii na elimu ya dini, kwa lengo la kuwajengea maadili mema.
“Kituo kitakuwa na uwezo wa kubeba watoto 150 kwa siku, mama lishe wataweza kulipia kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000 kwa ajili ya kusaidia kidogo huduma inayotolewa. Hii naamini itasaidia kuwapa nafasi kundi hilo kufanya kazi zao vizuri,” amesema.
Mwalunenge, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, amesema Sh150 milioni zinatarajiwa kutumika kujenga kituo hicho, ambapo yeye atachangia Sh50 milioni.
Muonekano wa eneo lililotengwa maalumu kwa ajili ya malezi na kunyonyeshea watoto katika soko la Mwanjelwa jijini Mbeya kuwasaidia Mama Lishe kufanya majukumu yao kwa ufanisi,
Amesema mradi huo unalenga kuboresha mazingira ya wafanyabiashara, akieleza kuwa wamekubaliana na halmashauri kutumia sehemu ya fedha za mikopo kwa makundi maalumu kuboresha mazingira yao ya biashara.
Ameongeza kuwa mkakati wake ni kuhakikisha masoko yote yanakuwa na vituo vya malezi ya watoto, akibainisha kuwa tayari ameelekeza eneo la Soko la Matola linalojengwa kutengwa kwa ajili ya huduma hiyo.
You may also like

Arusha steps up Ebola screening at Kenya border

TBS yaonya wanaochanganya pombe msimu wa sikukuu


Leave a Reply