

Kumbukumbu ya Coyote Arusha kufutwa na maghorofa
Arusha. Nyumba ya wageni ya Coyote, iliyokuwa ikitoa huduma za malazi kwa gharama nafuu katikati ya Jiji la Arusha, inatarajiwa kuondolewa kufuatia mpango wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa kubomoa jengo hilo na kujenga majengo mapya ya kisasa kwa ajili ya shughuli za kibiashara.
Jengo hilo, lililopo Mtaa wa Azimio, karibu na eneo lilipokuwa Soko la zamani la Madini la OTTU, limekuwa na nafasi muhimu katika historia ya biashara ya madini na utoaji wa huduma za malazi kwa wageni waliokuwa wakitembelea Jiji la Arusha kwa miaka mingi.
Akizungumza Oktoba 20, 2026, Meneja wa NHC Mkoa wa Arusha, Nistas Mvungi, alisema shirika hilo linapanga kubomoa jengo la zamani na kujenga majengo ya kisasa ya biashara yatakayokuwa na uwezo wa kuhudumia wapangaji 350, tofauti na wapangaji 43 waliokuwapo katika jengo hilo awali.
Amesema wapangaji wote walikuwa tayari wamehama na utekelezaji wa mradi huo utaanza muda wowote baada ya kukamilika kwa taratibu za kumkabidhi mkandarasi eneo hilo ili aanze kazi.
Amesema lengo la mradi huo ni kuongeza nafasi za biashara na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na uwekezaji huo.
Jengo hilo linakadiriwa kujengwa kati ya miaka ya 1950 na 1960, kabla ya kutaifishwa na Serikali na mali zake kukabidhiwa kwa Msajili wa Majumba. Baadaye, umiliki wa jengo hilo ulihamishiwa NHC kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na. 45 ya mwaka 1962.
Umaarufu wa jengo hilo uliongezeka zaidi katika miaka ya 1980, kipindi ambacho biashara ya madini ilishika kasi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Lomshuku, lenye machimbo ya madini ya ruby, na Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, ambako madini ya Tanzanite hupatikana. Wakati huo, Wilaya ya Simanjiro ilikuwa sehemu ya Mkoa wa Arusha kabla ya kuanzishwa kwa Mkoa wa Manyara.
Majengo ya Shirika la Nyumba nchini (NHC), Mtaa wa Swahili, Sokoine na Azimio jijini Arusha ambayo wapangaji wake wameshaondolewa kwaajili ujenzi wa Mradi mpya wa Sokoine Square unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Picha na Filbert Rweyemamu
Hivi karibuni mmoja wa watu wanaolifahamu jengo hilo kutokana na kufanya shughuli zake hapo, Stanley Sway amesema nyumba hiyo awali iliendeshwa na Mtanzania mwenye asili ya Asia, maarufu kama Singasinga, na kuitwa Ruby Guest House kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Coyote Guest House.
Amesema nyumba hiyo ilipokea wageni wa makundi na hadhi mbalimbali, wakiwamo wafanyabiashara wa madini waliotembelea Arusha.
“Miaka ya nyuma, Serikali ilikuwa ikipambana na wahujumu uchumi, hali hiyo ilizua hofu na baadhi ya Watanzania wenye asili ya Ulaya na Asia walikimbia. Baada ya muda, wengine walirudi na kuomba kurejea kwenye nyumba zilizokuwa zimetaifishwa,” amesema Sway.
Amesema aliyekuwa akiishi katika nyumba hiyo alikimbilia Canada na aliporejea nchini alikuta mali hiyo imeshakuwa chini ya NHC.
Baadaye alipewa sehemu ya juu ya jengo hilo, aliyoibadilisha kuwa nyumba ya wageni na kuiita Ruby.
Halima Fwady, aliyefanya kazi kwa muda mrefu katika nyumba hiyo ya wageni, amesema alianza kufanya kazi Coyote mwaka 2003 na kuendelea hadi Septemba 2026, mkataba wa mwajiri wake na mwenye nyumba ulipofikia mwisho.
“Namshukuru Mungu kwa kufanya kazi eneo hilo, limenipa maisha. Nimeweza kupiga hatua ya kuwapa elimu wanangu wawili na nina pa kuishi. Boss wangu ni mtu mwema, alikuwa anajali maslahi ya wafanyakazi wake,” amesema Fwady.
Amesema gharama ya malazi katika nyumba hiyo ilikuwa Sh25,000 kwa muda mrefu kabla ya kupanda na kufikia Sh30,000.
Amesema wageni walikuwa wakipiga simu mapema kuomba vyumba ili kuhakikisha wanapata nafasi, kutokana na kuipenda nyumba hiyo.
Kalist Juma, mkazi wa Arusha na dalali wa zamani wa madini, amesema eneo hilo lilikuwa sehemu muhimu ya maisha yao ya kiuchumi, hasa wakati nyumba za wageni zilipokuwa chache jijini humo.
Amesema Coyote ilikuwa sehemu ya kukutana kwa wafanyabiashara wa madini na wageni waliotoka maeneo mbalimbali, wakiwamo waliotembelea soko la madini la OTTU.
“Coyote haikuwa tu sehemu ya kulala, ilikuwa ni kitovu cha biashara zetu. Tulipokuwa tukitoka Soko la Madini la OTTU tukiwa na wageni kutoka vijijini kama Mererani, Coyote ndiyo ilikuwa sehemu salama na ya bei ambayo kila mtu angeweza kuimudu,” amesema Juma.
Naye Salome Chuwa, ambaye amekuwa akifanya biashara ya chakula karibu na jengo hilo kwa miaka 15, amesema mpango wa kulibomoa unatarajiwa kumuathiri kiuchumi kwa kuwa alikuwa akitegemea wateja waliokuwa wakifikia katika nyumba hiyo.
Amesema wageni waliokuwa wakilala Coyote walikuwa miongoni mwa wateja wake wakubwa, hivyo kuondoka kwao kutapunguza soko la biashara yake.
You may also like

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund

Mianya ya usajili inavyowalinda matapeli


Leave a Reply