

Lugangira ataka maridhiano, ushirikiano wa kisiasa Arumeru
Arumeru. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ametoa wito wa kuimarishwa kwa maridhiano, ushirikiano na mshikamano kati ya Serikali na vyama vya siasa, akisema mawasiliano ya pande hizo ni muhimu katika kutatua changamoto za wananchi na kuharakisha maendeleo.
Lugangira ameyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa vyama vya upinzani ofisini kwake, ikiwa ni sehemu ya hatua zake za awali za kutekeleza majukumu katika wilaya hiyo.
Amesisitiza kuwa tofauti za kiitikadi hazipaswi kuzuia ushirikiano katika masuala yanayogusa maisha ya wananchi, ikiwamo kuboresha huduma, kudumisha amani na kuhakikisha jamii inanufaika na fursa za maendeleo.
Amesema dhamira yake ni kushirikiana na wadau wote bila kujali misimamo au tofauti za vyama vyao vya siasa, akieleza kuwa hatua hiyo inaendana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu misingi ya 4R inayosisitiza maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, akiwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wilayani humo, alipofanya nao mazungumzo. Vyama hivyo ni CCK, DP, CHAUMMA, SAU, ADA TADEA, UPDP, UMD, CUF, NRA, Demokrasia Makini, ACT Wazalendo, AAFP, UDP, TLP, CHADEMA na NLD.
Mazungumzo hayo yanaashiria mwanzo wa mawasiliano kati ya uongozi wa wilaya na wawakilishi wa vyama vya upinzani, katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kuendeleza masuala ya maendeleo ya wananchi.
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Arumeru Mashariki, Pallangyo Penzila, amempongeza Lugangira kwa kuanza majukumu yake kwa kujifunza na kufahamu wilaya pamoja na wananchi wake.
Penzila amesema kuifahamu jamii anayoiongoza ni hatua muhimu kwa kiongozi anayeanza majukumu katika eneo jipya, kwa kuwa humwezesha kuelewa mahitaji ya wananchi na kufanya maamuzi yanayozingatia hali halisi ya eneo husika.
Ameeleza kuwa elimu, uzoefu na wito wa Lugangira katika utumishi wa umma vinaweza kuchangia maendeleo ya wananchi wa Meru iwapo kutakuwa na ushirikiano wa dhati kati ya uongozi wa Serikali na wadau wengine, bila kujali tofauti za kisiasa.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, akiwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wilayani humo, alipofanya nao mazungumzo. Vyama hivyo ni CCK, DP, CHAUMMA, SAU, ADA TADEA, UPDP, UMD, CUF, NRA, Demokrasia Makini, ACT Wazalendo, AAFP, UDP, TLP, CHADEMA na NLD.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP) wa Arumeru Mashariki, Magdalena Masaka, amemshukuru Lugangira kwa kukutana na wawakilishi wa vyama vya siasa mwanzoni mwa utekelezaji wa majukumu yake.
Masaka amesema hatua hiyo inaonyesha utayari wa kujenga ushirikiano kati ya Serikali na vyama vya siasa, akisisitiza kuwa jukumu la vyama hivyo halipaswi kuishia katika kipindi cha uchaguzi pekee.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira
Vyama vingine vilivyoshiriki mazungumzo hayo ni CCK, DP, CHAUMMA, SAU, ADA TADEA, UMD, CUF, NRA, Demokrasia Makini, ACT-Wazalendo, AAFP, UDP, TLP na NLD.
You may also like

Chadema yamwandikia Ruto kuhusu Mwaipaya

Wadau wa jinsia, Osha waonya unyanyasaji, hatari kazini

Leave a Reply