

Mabunge Afrika yatakiwa kuwapa wanawake nguvu ya uamuzi
Dar es Salaam. Mabunge ya nchi za ukanda wa Maziwa Makuu yametakiwa kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa kisiasa, ujenzi wa amani na usimamizi wa rasilimali za nchi zao, badala ya kuwapa nafasi za uwakilishi zisizoambatana na mamlaka ya kushawishi uaamuzi.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Novemba 2, 2026, katika ufunguzi wa mkutano wa wabunge wanawake wa nchi za ukanda wa maziwa makuu unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Novemba 2,2026 katika mkutano huo, Spika wa Bunge la Angola na Rais wa Jukwaa la Mabunge la Ukanda wa Maziwa Makuu, Adao de Almeida, amesema ushiriki wa wanawake unapaswa kuvuka hatua ya kuwapa nafasi katika meza za uamuzi na kuwawezesha kushawishi ajenda, kutoa mapendekezo na kushiriki katika uamuzi unaoathiri maisha ya jamii.
Amesema mabunge yanapaswa pia kujitathmini kuona kama mifumo na taratibu zake zinawawezesha wanawake wabunge kutekeleza kikamilifu majukumu yao na kushika nafasi za uongozi.
“Ni muhimu kutoka katika uwakilishi kwenda kwenye ushiriki, kutoka ushiriki kwenda kwenye ushawishi na kutoka ushawishi kwenda kwenye uongozi,” amesema.
Amesema ili kufanikisha hilo, mabunge yanapaswa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika michakato ya kuzuia migogoro, kuhakikisha ahadi za usawa wa kijinsia zinaingizwa kwenye bajeti za Serikali na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wake.
Baadhi ya viongozi walioshiriki katika Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mabunge ya nchi wanachama kupitia kubadilishana uzoefu na kuimarisha mahusiano na asasi za kiraia, hususan mashirika ya wanawake yanayofanya kazi katika jamii.
Amesema Jukwaa la Mabunge la ICGLR lina nafasi ya kuunganisha ahadi za kikanda na mahitaji halisi ya wananchi kwa kuimarisha mazungumzo kati ya mabunge na kufuatilia utekelezaji wa uamuzi unaofikiwa.
“Amani haipaswi kutafsiriwa kama kusimama kwa mapigano pekee, bali ni utamaduni unaojengwa kupitia elimu, mazungumzo, uvumilivu, ushirikishwaji na kuheshimu tofauti zilizopo katika jamii. Wanawake wanapaswa kuwa washiriki kamili na wanufaika wa moja kwa moja wa matumizi ya rasilimali za asili za Afrika,” amesema.
Amesema moja ya changamoto kubwa zinazolikabili bara la Afrika ni namna ya kubadilisha utajiri wa rasilimali zilizopo kuwa manufaa halisi ya kiuchumi na kuhakikisha unachangia maendeleo endelevu.
Ameeleza kuwa katika mchakato huo, wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu na kupata fursa za elimu, mafunzo ya ufundi, ardhi, mitaji, teknolojia na ajira zenye staha.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azan Zungu, amesema ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani na usalama ni msingi wa maendeleo endelevu, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sauti na changamoto zao katika sheria, sera na uamuzi wa umma.
Baadhi ya viongozi walioshiriki katika Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Amesema wanawake wana nafasi kubwa katika jamii kupitia majukumu yao kama wajenzi wa uchumi, viongozi wa jamii na walezi, hivyo ushiriki wao katika michakato ya amani haupaswi kuchukuliwa kama jambo la hiari.
“Diplomasia ya kibunge ina nafasi muhimu katika kusaidia nchi kujenga uwezo kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuhakikisha mahitaji ya wanawake na wasichana yanajumuishwa katika mifumo ya utawala,” amesema.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa nchini, Zungu amesema Bunge lina dhamira ya kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, akitaja kamati saba za kudumu za Bunge zinazoongozwa na wanawake.
Amezitaja kuwa ni Kamati za Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; Hesabu za Serikali; Nishati na Madini; Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge; Sheria Ndogo; Elimu, Utamaduni na Michezo; pamoja na Ustawi na Maendeleo ya Jamii.
Amesema Tanzania pia imeendelea kuunga mkono utekelezaji wa Azimio Namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake, amani na usalama, lililopitishwa mwaka 2000.
Azimio hilo linatambua umuhimu wa wanawake kushiriki katika kuzuia migogoro, mazungumzo ya amani, utatuzi wa migogoro na shughuli za kujenga upya jamii baada ya machafuko.
Zungu amesema kutowashirikisha wanawake katika masuala ya amani na usalama hakuathiri wanawake pekee, bali kunadhoofisha jamii nzima.
“Uwekezaji kwa wanawake ni uwekezaji kwa jamii imara na mataifa yenye ustawi. Ni vyema pia wajumbe wa mkutano huu kutumia fursa hii kuimarisha mikakati ya pamoja ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani na usalama wa ukanda wa Maziwa Makuu,” amesema Zungu.
You may also like

Tanzania – Fire Damages Six Hotels in Zanzibar

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund


Leave a Reply