

Mikoa yaongeza kasi usajili Bima ya Afya kwa Wote
Dar/mikoani. Mikoa mbalimbali nchini imeongeza juhudi za kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii, usajili wa walengwa na upatikanaji wa huduma bora za matibabu.
Katika uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango huo uliofanyika leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara, viongozi wameelekeza mamlaka za serikali za mitaa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha wananchi wanafikiwa na taarifa na kujiunga na mpango huo.
Wamesema mafanikio ya bima hiyo hayatapimwa kwa idadi ya waliojiandikisha pekee, bali pia uwezo wa vituo vya kutolea huduma za afya kutoa matibabu kwa wakati, kuwa na dawa na vifaa tiba na kuhudumia wananchi kwa ubora unaotarajiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Salum Hamduni, amesema hatakubali utekelezaji wa mpango huo kuwa jukumu la wataalamu wa afya pekee, akiwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kusimamia usajili na kutoa elimu kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Salum Hamduni akizindua awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Mwanza, Oktoba 22, 2026.
Amesema bado kuna wananchi wanaofika ofisini kwake siku za kusikiliza kero wakiomba kusaidiwa gharama za matibabu, hali inayoonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kuwasaidia kupata huduma za afya.
“Sitakubali mpango huu basi kuwa ni jambo la wataalamu wa afya pekee yake, kwa sababu afya ya wananchi ndiyo msingi wa maendeleo,” amesema Hamduni.
Ameelekeza kila halmashauri kuweka malengo ya usajili, muda wa utekelezaji na utaratibu wa kufuatilia maendeleo, akitaka elimu iwafikie wananchi kupitia viongozi wa kata na vijiji, vikundi vya wajasiriamali, wavuvi, Saccos na waendesha bodaboda.
Mara, Mwanza wapaza sauti
Katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha elimu na usajili wa wanufaika wa mpango unafanyika nyumba kwa nyumba ili kufikia asilimia 100 ya lengo, baada ya mkoa huo kusajili asilimia 41 pekee katika awamu ya kwanza.
Mtambi amesema hayo mjini Musoma wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango huo, akieleza kuwa kiwango hicho cha usajili ni kidogo ikilinganishwa na baadhi ya mikoa iliyofikia asilimia 97 ya malengo yake.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa taifa wa bima ya afya kwa wote awamu ya pili mkoani humo. Picha na Beldina Nyakeke
“Hamasisha hii ifanyike nyumba kwa nyumba ili usajili ufanyike kwa asilimia 100. Haiwezekani tukasajili kwa asilimia 41 pekee wakati mikoa mingine imesajili hadi asilimia 97 ya malengo,” amesema.
Amesema kutofikiwa kwa malengo katika awamu ya kwanza huenda kulitokana na kutowajibika kwa baadhi ya viongozi na uratibu usioridhisha, akitaka changamoto hizo zichunguzwe na kufanyiwa kazi ili kuhakikisha awamu ya pili inafanikiwa.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mara, Kuhunga Msambichaka, kaya 21,273 zenye wanufaika 44,786 zinatarajiwa kusajiliwa katika awamu ya pili.
Amesema katika awamu ya kwanza, mkoa ulisajili asilimia 41 ya lengo la kaya 14,148 zilizokuwa na wanufaika 62,256.
Msambichaka amesema Serikali imelipia bima za walengwa wa awamu ya pili kama ilivyofanya katika awamu ya kwanza, huku NHIF ikijiandaa kuimarisha uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na mpango huo.
Wananchi wa Mara wameunga mkono mpango huo, lakini wakasisitiza umuhimu wa kuhakikisha bima hiyo inaambatana na huduma bora za afya.
Emmanuel Kobiro amesema upatikanaji wa bima unapaswa kwenda sambamba na huduma bora ili wananchi wanufaike na mpango huo, huku Anasatazia Balagaye akitaka kufanyika kwa uchunguzi kubaini sababu zilizowafanya baadhi ya walengwa kutosajiliwa katika awamu ya kwanza.
Kwa upande wa Mkoa wa Mwanza, Meneja wa NHIF mkoani humo, Isaack Katemba amesema kaya 14,589 zilisajiliwa katika awamu ya kwanza kati ya 19,345 zilizolengwa, sawa na asilimia 75.4.
Amesema kati ya wanufaika 84,963 waliolengwa, 42,315 walisajiliwa.
Katika awamu ya pili, Katemba amesema mkoa unalenga kusajili kaya 35,642, lakini hadi wakati wa taarifa hiyo, kaya 1,790 zilikuwa zimesajiliwa, sawa na asilimia tano.
Kwa upande wa wanufaika, kati ya 90,981 waliolengwa, ni 2,870 tu waliokuwa wamesajiliwa, sawa na asilimia 3.2.
Katemba amesema NHIF itaendelea kushirikiana na viongozi wa Serikali na wataalamu wa afya kuhamasisha wananchi kujisajili ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Naye mnufaika wa mpango huo, Simoni Makolele, amewahimiza wananchi kujiunga, akisema yeye pamoja na watoto wake wamekuwa wakipata matibabu kupitia bima hiyo.
Mkoani Dodoma, Mkuu wa Mkoa huo, Rosemary Senyamule amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu inayoeleweka kuhusu namna ya kujiunga, faida za mpango huo, mafao na masharti ya kupata huduma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri akizungumza na wananchi wa mkoa wa Dodoma kwenye uzinduzi wa mpango wa bima ya afya kwa wote alipomwakilisha mkuu wa mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule
Kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, Senyamule amesema elimu inapaswa kuwafikia wajasiriamali, mama lishe, bodaboda, wakulima, wafugaji, watu wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Dodoma, Irene Kataraihya, amesema kaya 111,000 zimeingizwa katika mpango huo na kugharamiwa na Serikali kutokana na kuishi katika mazingira magumu.
Amesema kifurushi cha Sh150,000 kwa kaya yenye watu wasiozidi sita kinamwezesha mwananchi kupata huduma kuanzia zahanati hadi Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa. Pia, wanafunzi wanatakiwa kulipia Sh50, 400, huku shule 1,000 zikiwa zimejiunga.
Mmoja wa wanufaika, Ally Seif amesema bima hiyo imemsaidia kupata matibabu bila kutumia fedha nyingi, baada ya awali kulazimika kuuza baadhi ya mali zake kugharamia matibabu.
Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila amesema wanapanga kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na taasisi binafsi ili kuhakikisha kila mkazi anafikiwa.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Projest Mtasingwa amesema katika awamu ya kwanza mkoa ulilenga kaya 950 zenye wanufaika 4,232, lakini hadi wakati wa taarifa kaya 780 zenye wanufaika 2,483 zilikuwa zimesajiliwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martine Shigela, amesema mafanikio ya mpango huo yatapimwa kwa upatikanaji wa huduma kwa wakati na ubora wa matibabu, si takwimu za usajili pekee.
Akizindua awamu ya pili katika Kituo cha Afya Naberera, wilayani Simanjiro, Shigela amewaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi na waganga wakuu kuhakikisha wananchi wanapata elimu na huduma zinazostahili.
Amesisitiza kuwa hakuna mwananchi anayepaswa kunyimwa huduma za dharura kwa sababu ya majadiliano ya malipo au uhakiki wa bima.
Mkazi wa Naberera, Neema Kitoi, amesema mpango huo utasaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Salum Hamduni akizindua awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Mwanza, Oktoba 22, 2026.
Mkoani Lindi, Mkuu wa Mkoa Adam Malima, amewataka wakurugenzi wa halmashauri, waganga wafawidhi na wasimamizi wote wa sekta ya afya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kunyanyasika pindi wanapofika vituoni.
Malima amesema kwa sasa Mkoa wa Lindi umepunguza vifo vya kinamama wajawazito kutoka 38 hadi 29 kwa kila akinamama laki moja, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka vifo 272 kwa mwaka 2023 hadi vifo 209 kwa mwaka 2025.
Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya(NHIF) Mkoa wa Lindi Radhia Makono amesema kuwa Mkoa wa Lindi unalenga kusajili kaya 19,821 zenye jumla ya wanufaika 37,411 kutoka katika kaya zisizo na uwezo wa kugharamia huduma za afya, kupitia awamu ya pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Imeandikwa na Nasra Abdallah (Dar),Joseph Lyimo (Manyara), Saada Amir (Mwanza), Rachel Chibwete (Dodoma) na Beldina Nyakeke (Mara) na Bahati Mwatesa (Lindi).
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply