

Moto wateketeza vibanda 26 soko la Veterinary Dar
Dar es Salaam. Vibanda 26 kati ya 230 vilivyopo katika Soko la Veterinary, Temeke, vimeteketea kwa moto usiku wa kuamkia Oktoba 24, 2026, huku wafanyabiashara walioathirika wakikabiliwa na hasara baada ya mali zao kuteketea.
Moto huo umeathiri vibanda vilivyojengwa kwa mbao na kuezekwa kwa mabati, huku mpangilio wake wa kuungana kwa karibu ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizorahisisha moto kusambaa kutoka banda moja kwenda jingine.
Akizungumza na Mwananchi Oktoba 24, 2026, Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Temeke, Boniphace Adhiri, amesema vikosi vya zimamoto vilifanikiwa kuzima moto huo saa 9 usiku, huku baadhi ya askari wakiendelea kufuatilia hali ya eneo hilo ili kuhakikisha moto hauzuki tena.
“Hadi asubuhi, jeshi hilo lilikuwa limeacha gari la zimamoto eneo hilo kwa ajili ya kuendelea na zoezi la kupoza mabaki ya moto na kufuatilia uwezekano wa kuwapo kwa moshi unaoweza kusababisha moto kuwaka tena,” amesema Adhiri.
Amesema vibanda vilivyoteketea vilijengwa kwa mbao na kuezekwa kwa mabati, huku vikiwa vimeunganishwa kwa karibu, hali iliyochangia urahisi wa moto kusambaa kutoka banda moja kwenda jingine.
Magdalena Lyimo aliyefunga khanga akiangalia stoo ya vinywaji iliyoteketea kwa moto usiku wa kuamkia Oktoba 24,2026 katika soko la Veterinary, Temeke, jijini Dar es Salaam
Amesema mpangilio huo wa vibanda ulifanya moto kusambaa kwa haraka kwa kuwa hakukuwa na nafasi ya kutosha inayoweza kuzuia moto kuhamia katika vibanda vingine.
Hata hivyo, Kamanda Adhiri amesema jitihada za kuzima moto zilifanyika hadi moto ulipodhibitiwa, huku jeshi hilo likiendelea kuchukua tahadhari ili kuhakikisha hakuna uwezekano wa moto kujirudia.
Kwa upande wake, Salim Jumaa, mfanyabiashara wa eneo hilo, amesema taarifa za moto zilimfikia akiwa nyumbani baada ya wafanyabiashara wenzake kumpigia simu na kumjulisha kuwa kibanda chake kimeungua.
“Nilipata taarifa nikiwa nyumbani, nikatoka kwenda sokoni, lakini nilipofika nilikuta hali si nzuri, hakuna nilichoweza kuokoa zaidi ya nyundo pekee,” amesema Jumaa.
Amesema biashara yake ya milango na fremu za mbao ndiyo iliyokuwa ikimpatia kipato, hivyo kuungua kwa kibanda na bidhaa zake kumemweka katika wakati mgumu wa kutafuta namna ya kuanza upya.
Naye, Magdalena Lyimo, ambaye biashara yake inahusisha uuzaji wa vinywaji kwa jumla, amesema alipigiwa simu saa 10 alfajiri na kupewa taarifa kuwa stoo yake ilikuwa inaungua, lakini kutokana na kuishi Kimara, alishindwa kuwahi kufika kabla moto haujaharibu mali zake.
Amesema alifika eneo la tukio saa mbili asubuhi na kukuta stoo nzima imeteketea, bila kufanikiwa kuokoa bidhaa zozote zilizokuwamo ndani.
“Tukio hili limeniweka katika wakati mgumu. Nimepoteza bidhaa nilizokuwa nazitegemea kuendesha biashara yangu, hivyo nahitaji msaada wa kurejesha mtaji na kuanza upya,” amesema Magdalena.
Ameomba wafanyabiashara waliopoteza mali zao wapewe mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuanzisha upya shughuli zao bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni.
“Wafanyabiashara wengi hutegemea biashara zao kujipatia kipato cha kila siku, hivyo wanapokumbwa na majanga kama hayo hukabiliwa na changamoto za kuendeleza maisha na kurejesha mitaji iliyopotea,” amesema Magdalena.
Magdalena amesema msaada wa kifedha unapaswa kuzingatia uwezo wa wafanyabiashara kurejesha shughuli zao, huku akieleza kuwa uwezeshaji huo unaweza kuwasaidia kuinuka tena na kuendelea kuchangia uchumi wa familia zao.



Leave a Reply