

Mtanzania abuni mfumo wa kurahisisha mawasiliano kwa wasiosikia
Dar es Salaam. Changamoto ya mawasiliano aliyokuwa akiiona kwa rafiki yake mwenye ulemavu wa kusikia imemchochea kijana Sharifu Ally kutumia teknolojia kubuni mfumo unaolenga kurahisisha upatikanaji wa elimu na taarifa kwa watu wenye mahitaji maalumu.
Ally, mwanzilishi wa Signedu Africa na mbunifu wa programu za kompyuta, anasema wazo la mfumo huo lilimjia mwaka 2023 alipokuwa kidato cha nne, baada ya kushuhudia changamoto zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia katika kufuatilia masomo darasani.
Mfumo huo hutumia teknolojia ya avatar kutafsiri lugha ya ishara kuwa maandishi na sauti. Pia, avatar inaweza kuwasilisha mazungumzo ya mtu anayezungumza kwa lugha ya ishara ili mtu mwenye ulemavu wa kusikia aweze kuelewa ujumbe unaotolewa.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano, Oktoba 21, 2026, katika maonyesho ya ubunifu wa biashara ya Tanzania Startup Week 2026 yanayofanyika jijini Dar es Salaam, Ally amesema wazo hilo lilitokana na uzoefu wake wa kusoma na rafiki yake katika Shule ya Sekondari ya Azania, aliyekuwa na uwezo mkubwa kitaaluma lakini alikabiliwa na changamoto ya kusikia.
“Nilikuwa naona changamoto anazopitia kila siku. Mwalimu anapofundisha, alikuwa akitumia nguvu kubwa kumwelewa. Nilijiuliza kama ninaweza kutumia teknolojia kutatua tatizo hili,” amesema.
Ally amesema baadaye alikutana na wanafunzi wengine wenye changamoto zinazofanana wakati wa mashindano yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Benjamin, Kariakoo, jambo lililompa msukumo zaidi wa kutafuta suluhisho.
Amesema msaada alioupata kutoka kwa walimu na shule ulimwezesha kupata zana na rasilimali zilizomsaidia kuendeleza wazo hilo akiwa bado mwanafunzi.
“Mfumo wetu wa elimu ni mzuri, lakini tunahitaji kuhakikisha unajumuisha wanafunzi wote ili kila mmoja apate fursa sawa ya kujifunza,” amesema.
Ally amesema Signedu Africa ni mfumo wa kiteknolojia unaoweza kufikiwa kupitia simu janja na unaolenga kurahisisha mawasiliano kati ya watu wanaotumia lugha ya ishara na wasioutumia.
Kupitia mfumo huo, ishara zinazotolewa na mtu zinaweza kutafsiriwa kuwa maandishi na sauti. Vilevile, mazungumzo ya mtu yanaweza kuwasilishwa kwa lugha ya ishara kupitia avatar ili mtumiaji mwenye ulemavu wa kusikia aweze kufuatilia ujumbe.
Amesema teknolojia hiyo inalenga kupunguza vikwazo vya mawasiliano na kuwezesha watu wenye ulemavu wa kusikia kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kielimu.
Katika mazingira ya shule, mfumo unaweza kutumiwa kupitia kompyuta kibao au skrini darasani ili kusaidia kuwasilisha maelezo ya mwalimu kwa lugha ya ishara.
Kwa mujibu wa Ally, matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kupanuliwa hadi kwenye mikutano, makongamano, viwanja vya ndege na vituo vikubwa vya mabasi, ambako matangazo na taarifa hutolewa mara nyingi kwa njia ya sauti.
Amesema wakati wa mikutano na majadiliano kuhusu teknolojia na ubunifu, amekuwa akijiuliza namna watu wenye ulemavu wa kusikia wanavyopata taarifa zinazowasilishwa kwa sauti pekee.
“Je, kuna mtu ambaye hasikii vizuri na anapataje taarifa hizo? Kama kungekuwa na skrini inayotafsiri mazungumzo kwa lugha ya ishara, hata wao wangeweza kufuatilia,” amesema.
Ally amesema mfumo huo umeshawasaidia zaidi ya wanafunzi 65 wenye changamoto za kusikia, huku watu zaidi ya 100 wakinufaika kwa kujifunza lugha ya ishara.
Amesema mfumo huo pia unaweza kuwasaidia wazazi na walezi kujifunza lugha hiyo ili kurahisisha mawasiliano na watoto wao wenye ulemavu wa kusikia au kuzungumza.
Hata hivyo, amesema Signedu Africa bado iko katika hatua ya majaribio na tayari inafanyiwa majaribio katika Shule ya Sekondari ya Azania.
Ameeleza kuwa mfumo huo umeunganishwa na mifumo miwili, mmoja unaohusiana na ushirikishwaji wa wazazi katika shughuli za shule na mwingine unaohusika na tafsiri ya lugha ya ishara.
Kwa sasa, programu ya simu inayotumika kuufikia mfumo huo bado haijawekwa rasmi katika maduka ya programu ya Google Play Store au Apple App Store.
Ally amesema watu wanaotaka kuujaribu mfumo huo wanaweza kuwasiliana naye moja kwa moja.
Licha ya hatua alizofikia, Ally amesema anahitaji mwekezaji atakayekuwa tayari kuunga mkono wazo lake na kusaidia kukuza ubunifu huo ili uwafikie watu wengi zaidi.
Amesema lengo lake ni kutumia teknolojia kupunguza vikwazo vya mawasiliano na kuongeza ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalumu katika elimu na huduma nyingine za kijamii.
Kwa Ally, ubunifu huo ulioanza akiwa mwanafunzi wa sekondari ni juhudi za kutafuta suluhisho la changamoto aliyoshuhudia kwa rafiki yake, huku akilenga kuupanua mfumo huo ili uweze kutumiwa na watu wengi zaidi.
You may also like


Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade


Leave a Reply