

Mwenyekiti wa Handeni aanguka, afariki ghafla
Tanga. Kifo cha ghafla cha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Mussa Mwanyumbu, kimeacha pengo kubwa katika halmashauri hiyo, huku viongozi, watumishi na wananchi wakikumbuka mchango wake katika kusimamia shughuli za maendeleo.
Mwanyumbu ambaye alikuwa Diwani wa Mkata alianguka ghafla jioni ya jana Jumapili, Novemba 1, 2026, katika ofisi za CCM Mkoa wa Tanga, alipokuwa akihudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho, kilichohusisha pia utambulisho wa mlezi mpya wa CCM mkoani humo, Rabia Abdallah.
Akizungumzia kifo hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Saitoti Steven, alisema utendaji wake, uchapakazi na usimamizi wa miradi ya maendeleo ni miongoni mwa mambo yatakayokumbukwa kutokana na mchango alioutoa wakati wa uhai wake.
“Kwa halmashauri yetu, msiba huu ni mkubwa sana. Mwenyekiti wetu hakuwa na changamoto yoyote ya kiafya na alikuwa akitekeleza majukumu yake bila shida. Kusikia kwamba ameanguka ghafla na baadaye kufariki dunia kumetushtua sana,” alisema Steven.
Kwa upande wake, Katibu wa Uenezi, Siasa na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Tanga, Samweli Mngazija, alisema marehemu alihudhuria kikao hicho bila kuonyesha dalili zozote za tatizo, lakini baada ya kikao kumalizika alianguka ghafla.
Alisema kifo hicho ni pigo kwa chama kutokana na mchango wa Mwanyumbu katika shughuli zake, akimtaja kuwa mwanachama mwaminifu na mtiifu katika vikao, aliyekuwa akitoa mawazo yaliyosaidia kukijenga chama na kuimarisha huduma kwa wananchi.
Naye Shaban Alfan, mmoja wa wananchi wa kata aliyokuwa akiitumikia marehemu kama diwani, alisema wataendelea kuukumbuka mchango wake katika kusimamia shughuli za maendeleo na kutetea mahitaji ya wananchi wa eneo hilo.
You may also like

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund

Mianya ya usajili inavyowalinda matapeli


Leave a Reply