

Naberera walalamikia tembo kuua mtoto na kuharibu mazao
Simanjiro. Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Naberera wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba Serikali kuwadhibiti tembo wanaovamia makazi yao, kwani wamesababisha kifo cha mtoto mdogo na kuharibu mazao.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Emmanuel Mollel (Hugo) akizungumza leo Alhamsi, Oktoba 22, 2026 amesema ni vyema Serikali kuingilia kati na kuwadhibiti tembo hao ili wasisababishe madhara zaidi.
Hugo amesema tukio la Simon Mbototo kijana wa miaka 16 kuuawa na tembo limesababisha uchungu na simanzi katika eneo lao kwani hilo ni tukio la tatu la vifo hivi karibuni vinavyosababishwa na tembo.
Amesema tukio hilo la kijana huyo kuuawa na tembo lilitokea Oktoba 18, 2026 saa 10 jioni akiwa machungani kwenye kitongoji cha Kosiki kijiji cha Naberera.
Baadhi ya vyombo vya mkazi wa kijiji cha Naberera wilayani Simanjiro mkoani Manyara, vilivyokanyagwa na tembo waliofika nyumbani kwake usiku
“Tunaomba serikali ichukue hatua kwani mwezi Agosti kulitokea tena vifo viwili vya wakazi wa Nabebera vilivyosababishwa na tembo,” amesema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo Sokoine Sakita amesema tembo hao wamefika hadi nyumbani kwake usiku na kuharibu baadhi ya vyombo vyake.
Sakita amesema wanaiomba Serikali iweke mkazo kwenye changamoto hiyo, kwani tembo hao wamesababisha madhara ya kifo na pia wamekuwa waharibifu wa mazao kwenye mashamba.
Hata hivyo, ofisa wanyamapori wa Wilaya ya Simanjiro, Aloyce Olodonjilalo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la tembo kusababisha kifo cha kijana huyo wa Nabebera.
Olodonjilalo amesema Oktoba 18, 2026 alipigiwa simu na Mwenyekiti wa kijiji cha Naberera na kupewa malalamiko ya tembo kufanya mauaji kitongoji cha Kosiki.
Amesema walituma kikosi cha doria kilichokuwa maeneo ya Komolo kilifika usiku huo na kuendelea na msako wa tembo hao na hadi sasa bado wanaendelea na doria.
“Tunawapa pole wafiwa ila hatua nyingine zinaendelea ikiwemo mchakato wa kifuta machozi, hatua ya ngazi ya kijiji na wilaya zimekamilika ili kutumwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua zaidi,” amesema.
Amesema halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa) wameweka mikakati ya kupambana na tembo wilayani Simanjiro.
Ametaja mikakati ya kupambana ni kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano ya ya vitongoji, vijiji na nyumba za ibada kwa kuwapa mbinu na zana za kupambana na tembo.
Amesema wanajenga vituo vya kupambana na wanyamapori waharibifu kwa kuanzia kijiji cha Kandasikira na kingine kitajengwa kijiji cha Naberera.
Amesema ndege nyuki moja imeshapatikana kupitia Tawa kwa ajili ya kufukuza na kuhamisha tembo pia askari wameongezwa baada ya kupatiwa mafunzo na wengine kupelekwa chuo cha Sekamaganga Tabora.
“Tuendelee kutoa ushirikiano na kuwa na subira wakati haya yakiendelea kutokea, kwani Serikali inawajali na ina mikakati mingi kwa ajili ya kusaidia jamii kupunguza changamoto ya tembo,” amesema.
You may also like


Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade

Leave a Reply