

Naibu Katibu Mkuu CUF ajiweka kando, Nassor akaimu
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Said Miraji, amejiweka kando na wadhifa huo alioutumikia kwa miezi mitano tangu kuteuliwa kwake na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho.
Kutoridhishwa na mwenendo wa mambo yanayoendelea ndani ya chama hicho, ikiwemo mivutano ya kiuongozi, ni miongoni mwa sababu zinazodaiwa kuchangia uamuzi wake, ambao umewashangaza baadhi ya wafuasi wa CUF.
Hata hivyo, chama hicho kimekanusha madai hayo, kikisema uamuzi wa Miraji kujiweka kando umetokana na sababu zake binafsi, ikiwemo kuona kuwa aina ya siasa zinazofanyika sasa ni tofauti na zile zilizokuwa zikifanyika zamani.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa CUF, Yusuf Mirambo, amemkaimisha Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi wa chama hicho, Nassoro Masoud Nassor, kushika nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho hadi vikao vya Baraza Kuu vitakapofanyika.
Alipotafutwa kwa simu leo, Oktoba 24, 2026, ili kueleza sababu za uamuzi wake, Miraji amesema hana cha kuzungumza na kumtaka mwandishi amtafute Mwenyekiti Mirambo, akisema ndiye msemaji wa chama hicho.
Mwananchi lilipomtafuta Mirambo, amethibitisha kuwa Miraji amejiweka kando, akisema katika barua aliyowasilisha kwake alieleza kuwa anaona mambo hayaendi vizuri ndani ya chama hicho.
“Ni kweli amejiweka kando. Nilipokea barua yake na sababu aliyoitaja ni kwamba anaona mambo hayaendi vizuri ndani ya chama. Hatuna la kufanya; kikubwa ni kuhakikisha kazi zinaendelea. Chama kina wanachama wengi wanaoweza kushika nafasi hiyo,” amesema.
Mirambo amesema nafasi hiyo tayari imekaimiwa na Nassor kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, hatua inayolenga kuhakikisha sekretarieti inaendelea kuwa imara na kutekeleza majukumu ya chama kila siku.
Amesema CUF kwa sasa ni imara na inaendelea kutekeleza majukumu yake, huku viongozi wakiendelea na kazi zao.
Amewataka wanachama kuendelea kukiamini chama hicho katika jitihada za kutimiza dhamira yake ya kushika dola.
“Kuna propaganda nyingi zinazopigwa kwa lengo la kuwaondoa wanachama kwenye malengo yao ya kukijenga chama na kuhakikisha kinapambana kushika dola ili kuwakomboa wananchi dhidi ya changamoto wanazopitia,” amesema.
Mirambo amesisitiza kuwa dhamira yake ni kukifanya chama hicho kiwe imara na kuwaunganisha wanachama ili iwe rahisi kutimiza azma ya kukijenga na kukirudisha katika hali yake ya zamani.
Tangu Mirambo achaguliwe kuongoza CUF Februari mwaka huu, Miraji amekuwa kiongozi wa pili kujiweka kando. Wa kwanza alikuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Mohamed Ngulangwa.
Juni 28 mwaka huu, Ngulangwa alijiweka kando pamoja na viongozi wengine 16 wa ngazi ya wilaya upande wa Zanzibar kutokana na kutoridhishwa na mfumo wa uongozi na migogoro ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, nafasi ya Ngulangwa kwa sasa inashikiliwa na Kanali Shughuli, aliyeteuliwa na Mirambo. Mwenyekiti huyo amesema anaamini uwezo na ushawishi wa Shughuli unamfaa kutekeleza majukumu ya wadhifa huo.
You may also like

Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade

Samia to inaugurate Sh700bn Government City on October 30


Leave a Reply