

NEMC yapendekeza mabadiliko ya sheria kuanzisha Nema
Dodoma. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limependekeza mabadiliko ya sheria yatakayowezesha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (Nema), kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa mazingira na kurahisisha biashara na uwekezaji nchini.
Pendekezo hilo limewasilishwa leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, mbele ya kamati za kudumu za Bunge ikijumuisha Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya Maji na Mazingira, katika kikao kilichofanyika bungeni, Dodoma.
Katika wasilisho hilo, NEMC pia iliwasilisha masuala yanayohusu usimamizi wa taka ngumu na fursa za kiuchumi zinazoweza kupatikana kupitia urejelezaji na uchakataji wa taka.
Ilielezwa kuwa kuimarisha usimamizi wa taka ngumu ni muhimu katika kulinda afya ya jamii na mazingira, huku taka zikichukuliwa kama rasilimali zinazoweza kutumika kuzalisha fursa za kiuchumi.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi, amesema mabadiliko ya sheria yanayopendekezwa yanalenga kuiwezesha taasisi hiyo kuwa mamlaka kamili inayokwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwezesha biashara na uwekezaji, pamoja na kukuza uchumi endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira.
Amefafanua kuwa mabadiliko hayo yanahusisha kubadilisha jina la taasisi kutoka NEMC kwenda Nema na kuimarisha vipengele vya kisheria ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Immaculate Semesi akichangia
Kwa mujibu wa Dk Semesi, lengo ni kuifanya taasisi hiyo kuwa mwezeshaji badala ya kuwa kikwazo kwa wawekezaji, hususan katika kutimiza masharti ya kisheria na kupata vibali vinavyohitajika.
Amesema kuimarishwa kwa mfumo wa kisheria kutasaidia kusawazisha mahitaji ya uwekezaji na wajibu wa kulinda mazingira, bila kuathiri matakwa ya sheria zinazohusu utunzaji wa mazingira.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga amesema tayari Serikali kupitia Bunge imeridhia kutungwa kwa sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Mazingira, hatua inayolenga kuipa NEMC nguvu zaidi za kisheria katika kusimamia uhifadhi wa mazingira nchini.
Amesema hatua hiyo inatokana na kuendelea kwa uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayohitaji kuimarishwa kwa usimamizi na udhibiti wa shughuli zinazohatarisha mazingira.
Kiswaga amesema kumekuwa na mwingiliano katika utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa mazingira, jambo linalochangia kukosekana kwa ufanisi katika udhibiti wa uharibifu wa mazingira.
Amesema Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 ya mwaka 2004, inazipa Serikali za Mitaa jukumu la kusimamia masuala ya mazingira, lakini kukosekana kwa usimamizi wa kutosha kutoka kwa chombo kingine kunachangia changamoto katika utekelezaji wa majukumu hayo.
Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa Nema, kutaiwezesha NEMC kuwa na nguvu za kisheria za kusimamia masuala ya mazingira katika maeneo yote nchini, hatua itakayosaidia kuimarisha udhibiti na kuongeza ufanisi katika uhifadhi wa mazingira.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply