

Njia tatu za kumfundisha mtoto maadili
Dar es Salaam. Malezi ya mtoto si suala la kumpatia chakula, mavazi, makazi na elimu pekee.
Zaidi ya mahitaji hayo, mtoto anahitaji kujengewa misingi ya maadili itakayomwongoza katika uamuzi wake, uhusiano wake na namna atakavyoishi na watu wengine katika jamii.
Katika dunia inayobadilika kwa kasi kutokana na utandawazi na maendeleo ya teknolojia, jukumu la wazazi katika malezi limezidi kuwa muhimu. Watoto wanakutana na mitazamo, tabia na vishawishi mbalimbali kupitia shule, marafiki na mitandao ya kijamii.
Hali hiyo inawataka wazazi kutafakari namna bora ya kuwafundisha watoto kutofautisha mema na mabaya.
Kwa jumla, kuna njia tatu zinazoweza kutumika katika kufundisha maadili, nidhamu na matarajio ya jamii, kutegemea taasisi za nje na malezi yanayojengwa katika misingi ya imani. Kila njia ina namna yake ya kumwelekeza mtoto, lakini nafasi ya mzazi katika mchakato huo haiwezi kupuuzwa.
Nidhamu na matarajio ya jamii
Njia ya kwanza inahusisha kumfundisha mtoto tabia zinazokubalika katika jamii anayoishi. Hapa, mtoto huelekezwa kuhusu umuhimu wa kusalimia watu, kuheshimu wengine, kuwa mwaminifu, kutenda wema, kutimiza ahadi na kusema ukweli.
Lengo ni kumsaidia mtoto kuelewa matarajio ya jamii na kuishi kwa kuzingatia mila, desturi na sheria zinazotawala maisha ya watu.
Kupitia maelekezo ya wazazi na mifano wanayoiona nyumbani, mtoto hujifunza namna ya kuwasiliana na wengine na kutambua tabia zinazoweza kuumiza au kuwakwaza watu wanaomzunguka.
Hata hivyo, malezi yanayosisitiza matarajio ya jamii pekee yanaweza kumfanya mtoto azingatie zaidi namna watu wanavyomtazama kuliko sababu za msingi za kutenda jambo jema.
Anaweza kujizuia kufanya kosa kwa sababu anaogopa kukemewa au kuaibika mbele ya watu, badala ya kuelewa kwa nini kitendo hicho si sahihi.
Ndiyo maana ni muhimu wazazi wasifundishe sheria na maelekezo pekee, bali pia waeleze sababu za maadili hayo. Mtoto anapoelewa thamani ya ukweli, uaminifu na heshima, anapata nafasi ya kuyafanya maadili hayo kuwa sehemu ya maisha yake.
Kutegemea shule na taasisi za nje.
Njia ya pili ni pale mzazi anapokabidhi kwa kiasi kikubwa jukumu la kumfundisha mtoto kwa shule na taasisi nyingine za kijamii. Taasisi hizo zinaweza kujumuisha vituo vya mafunzo, kambi za vijana, huduma za ushauri na programu mbalimbali za malezi.
Katika mfumo huu, mzazi hujikita zaidi katika mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi, ada na makazi, huku akitarajia walimu na walezi wengine wasimamie sehemu kubwa ya maendeleo ya mtoto, ikiwamo tabia na maadili.
Ni kweli kwamba shule na taasisi nyingine zina mchango mkubwa katika kujenga maarifa, nidhamu na ujuzi wa watoto. Walimu wanaweza kugundua changamoto ambazo mzazi hajaziona, huku washauri wakisaidia watoto kukabiliana na matatizo mbalimbali ya ukuaji na uhusiano.
Hata hivyo, changamoto hujitokeza pale msaada huo unapogeuka kuwa mbadala wa malezi ya mzazi. Mtoto anahitaji uangalizi wa karibu nyumbani, mazungumzo ya mara kwa mara na mtu anayefuatilia mabadiliko ya tabia yake.
Mzazi anapojiondoa katika jukumu hilo, anaweza kuchelewa kutambua changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.
Kwa hiyo, taasisi za nje zinapaswa kuonekana kama washirika wa mzazi katika malezi, si vyombo vinavyoweza kuchukua nafasi yake kikamilifu. Ushirikiano kati ya familia na shule unaweza kumsaidia mtoto kupata mwongozo unaoeleweka katika mazingira tofauti.
Imani kama msingi wa maadili
Njia ya tatu ni malezi yanayojengwa katika misingi ya imani, ambapo mtoto hufundishwa kwamba maadili si suala la kutii matarajio ya jamii pekee, bali pia ni sehemu ya wajibu wake wa kiroho.
Kwa mtazamo huu, mtoto anafundishwa kumcha Mungu, kutenda mema na kujiepusha na uovu hata wakati hakuna mtu anayemwona.
Tofauti inayosisitizwa ni kwamba mtu anaweza kujizuia kufanya jambo baya kwa kuogopa hukumu ya jamii, lakini imani inamwelekeza kutenda kwa uadilifu hata akiwa peke yake.
Malezi ya aina hii yanapotekelezwa kwa maelekezo yanayoeleweka na mifano ya vitendo, yanaweza kumsaidia mtoto kuunganisha imani yake na mwenendo wa kila siku.
Msingi wa hoja hii ni kwamba mtoto anahitaji kuelewa si tu kile kinachotarajiwa kutoka kwake, bali pia sababu za kutenda kwa uadilifu. Hapo ndipo wazazi wanapoweza kuunganisha mafundisho ya maadili ya kijamii na misingi ya imani wanayoithamini.
Kwa mtazamo huo, malezi bora yanapaswa kuanzia nyumbani, ambako mtoto hujifunza kupitia maelekezo na matendo ya wazazi. Mzazi anayefundisha uaminifu lakini mwenyewe anasema uongo mara kwa mara anaweza kutoa ujumbe unaokinzana na maelekezo anayompa mtoto.
You may also like

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund

Mianya ya usajili inavyowalinda matapeli

Leave a Reply