

Pwani yalenga kuwafikia wananchi milioni moja msaada wa kisheria
Kibaha. Mkoa wa Pwani unalenga kuwafikia wananchi milioni moja kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), awamu ya pili, sawa na asilimia 50 ya wakazi wa mkoa huo wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni mbili.
Lengo hilo ni mara tano ya wananchi 200,000 waliofikiwa katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo mwaka 2025, huku migogoro ya ardhi ikiwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji wananchi kupata elimu na msaada wa kisheria.
Kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 28, 2026, huku huduma zikianza kutolewa Oktoba 29 kwa muda wa siku 10 katika kata 136 za Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 23, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo amesema matarajio ya awamu hii ni kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kisheria na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Huduma zitakazotolewa bila malipo ni pamoja na ushauri wa kisheria, elimu kuhusu masuala ya sheria na uandaaji wa nyaraka za kisheria.
Wananchi pia watapata huduma za usajili wa matukio muhimu ya binadamu, yakiwamo vyeti vya kuzaliwa na vifo, kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
Aidha, wenye mashauri mahakamani au katika vyombo vya utoaji haki watanufaika na huduma za uwakili kupitia mawakili wa kujitegemea na wa Serikali walioidhinishwa kutekeleza jukumu hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Uzingatiaji Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Osbora Paissi amesema wananchi wanapaswa kutarajia kupata huduma hizo kwa uhakika, akieleza kuwa wataalamu wamejiandaa kuwahudumia wakati wa utekelezaji wa kampeni hiyo.
Amesema maandalizi yamefanyika ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msaada wa kisheria wanazohitaji katika kipindi cha kampeni hiyo.
Kupitia kampeni hiyo, wananchi wenye changamoto za kisheria watapata fursa ya kupata ushauri kuhusu haki zao, taratibu za kisheria na hatua wanazoweza kuchukua kutatua migogoro inayowakabili.
Kampeni hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao na kupunguza changamoto zinazotokana na gharama za kupata huduma hizo.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations

Leave a Reply