

Rais Samia amtwisha zigo mkurugenzi mpya TTB
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kutumia mikutano ya kimataifa inayofanyika nchini kama fursa ya kuongeza idadi ya watalii, kwa kuwahamasisha wageni wanaohudhuria mikutano hiyo kutembelea vivutio mbalimbali.
Amesema bodi hiyo inapaswa kuimarisha uratibu na ushirikiano na wadau wa sekta ya utalii ili kuitangaza Tanzania na kuongeza manufaa ya kiuchumi yanayotokana na wageni wanaoingia nchini.
“Utalii sasa ndiyo kichocheo kikubwa cha uchumi wetu,” amesema Rais Samia.
Ametoa maelekezo hayo leo Novemba 25, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akiwaapisha wakuu wa taasisi za umma na mabalozi aliowateua hivi karibuni.
Wakuu wa taasisi walioapishwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dk Thereza Mugobi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Said Mndeme na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Ezekiel Goboro.
Mabalozi walioapishwa ni Talha Waziri, Lucas Aaron Mayanga na Miraji Ukuti.
Akizungumzia sekta ya utalii, Rais Samia amesisitiza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kushirikiana na waendeshaji wa shughuli za utalii kuhakikisha wageni wanaokuja nchini kwa shughuli za mikutano, makongamano na matukio ya kimataifa wanapata fursa ya kutembelea vivutio vya asili, utamaduni na maeneo mengine ya utalii.
Mkakati huo unaweza kuongeza muda wa wageni kukaa nchini na matumizi yao katika hoteli, usafiri, migahawa, kampuni za utalii na biashara nyingine zinazotegemea wageni.
Takwimu za sekta ya utalii zinaonyesha Tanzania ilipokea watalii wa kimataifa 2,294,495 mwaka 2025, kutoka 2,141,895 mwaka 2024.
Katika kipindi hicho, mapato ya utalii yaliongezeka kwa asilimia 13 hadi Dola za Marekani bilioni 4.41, kutoka Dola bilioni 3.9 mwaka 2024.
Ukuaji huo unaonyesha umuhimu wa kuimarisha mikakati ya kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuhakikisha wageni wanaofika nchini wanatumia fursa mbalimbali za utalii, ikiwemo vivutio vya asili, utamaduni na mikutano ya kimataifa.
Utalii wa mikutano, unaojumuisha mikutano, maonyesho na makongamano ya kimataifa, ni miongoni mwa fursa zinazoweza kuongeza idadi ya wageni na mapato kwa hoteli, usafiri, migahawa na biashara nyingine zinazohusiana na sekta hiyo.
Katika eneo la usimamizi wa mali za umma, Rais Samia ameitaka TBA kutambua na kutunza majengo ya Serikali, pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika kuyaendeleza.
Amesema majengo yasiyotumika yanapaswa kuangaliwa kama fursa za uwekezaji na matumizi yenye tija, sambamba na kuanzisha miradi mipya kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Wakala wa Majengo Tanzania una jukumu la kusimamia maendeleo na matengenezo ya majengo ya Serikali, kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu katika miradi ya ujenzi na kuhifadhi kanzidata ya viwanja na majengo ya Serikali.
Pia, wakala huo unasimamia upangishaji wa nyumba za Serikali kwa matumizi ya kibiashara na huduma nyingine za usimamizi wa milki.
Hatua ya kushirikisha sekta binafsi ina umuhimu katika kuongeza thamani ya mali hizo na kupunguza uwezekano wa ardhi na majengo ya umma kubaki bila matumizi ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), TBA umetangaza fursa 38 za uwekezaji kupitia ubia na sekta binafsi, zikiwemo eneo la ekari 630 Nzuguni, Dodoma, lililotengwa kwa ajili ya maendeleo ya makazi na biashara.
Fursa nyingine zimetambuliwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Morogoro na Mwanza.
Kwa upande wa uhifadhi, Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania kuimarisha juhudi za kulinda rasilimali za wanyamapori, kukabiliana na ujangili na kutoa elimu kwa jamii zinazoishi katika maeneo yanayozunguka hifadhi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka mabalozi aliowaapisha kutumia uzoefu wao kuiwakilisha Tanzania vizuri nje ya nchi na kutekeleza dhamana zao kwa uadilifu na uwajibikaji.
“Nendeni mkafanye kazi kwa weledi na uwajibikaji, mnapaswa kuthibitisha imani mliyopewa kwa kuwatumikia vyema Watanzania.”
You may also like

Ndejembi aagiza tathimini mahitaji ya wafamasia



Leave a Reply