

Siku tatu za mateso ya usafiri Mbeya, wananchi wapaza sauti
Mbeya. Siku tatu za usumbufu wa usafiri jijini Mbeya zimeibua kilio kwa wananchi wanaotegemea bajaji kufika kazini, kufanya biashara na kusafirisha bidhaa, huku wakiiomba Serikali kuwashirikisha wadau kabla ya kufanya maamuzi yanayoweza kuathiri shughuli zao za kila siku.
Wamesisitiza kuwa maamuzi kuhusu matumizi ya barabara yanapaswa kuzingatia mahitaji ya wananchi, hali halisi ya miundombinu na mchango wa bajaji katika kurahisisha usafiri wa mijini.
Kauli hizo zimekuja wakati huduma za bajaji zikianza kurejea katika barabara kuu leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, baada ya kusimama kwa siku kadhaa kufuatia mgogoro kuhusu matumizi ya barabara hizo na utaratibu wa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na madereva bajaji.
Mgogoro huo ulifuatia maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, Oktoba 12, 2026, kwa viongozi wa Jiji la Mbeya na wilaya husika kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya madereva bajaji na wafanyabiashara wadogo wanaojulikana kama machinga.
Maguta yakishusha abilia katika stendi ya Kabwe jijini Mbeya kufuatia changamoto ya usafiri baada ya bajaji kuondolewa katika barabara kuu.
Hata hivyo, utekelezaji wa maelekezo hayo ulizua sintofahamu na mvutano, huku kukiwa na taarifa za vurugu na uharibifu wa vyombo vya moto, vikiwemo daladala.
Wakizungumza na Mwananchi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, baadhi ya wananchi wamepongeza hatua ya Serikali kusikiliza malalamiko ya madereva, lakini wakataka mazungumzo ya aina hiyo yafanyike mapema ili kuepusha migogoro inayoweza kusimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Tausi Azory, mkazi wa Nonde, amesema ni muhimu Serikali kutumia busara katika kushughulikia changamoto za usafiri kwa kuzingatia athari zinazoweza kuwakumba wananchi pale huduma hizo zinaposimama.
“Tunapongeza hatua ya Serikali kutumia busara kusikiliza kilio cha madereva, lakini ni vyema suala hili liangaliwe kwa jicho la kipekee na hatua zichukuliwe mapema ili kuepusha athari kwa shughuli za kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuwashirikisha watumiaji wa vyombo hivyo kabla ya kufanya maamuzi yanayowahusu, akieleza kuwa maoni yao yanaweza kusaidia kupata suluhisho linalokubalika na kupunguza uwezekano wa migogoro kujirudia.
Kwa upande wake, David David, dereva wa magari makubwa anayefanya safari kutoka Zambia kwenda Malawi, amesema pamoja na umuhimu wa kuweka utaratibu wa matumizi ya barabara, Serikali inapaswa kuzingatia hali ya miundombinu na kutoa elimu kwa madereva kuhusu mpangilio wa usafiri jijini.
Amesema changamoto za miundombinu zinapaswa kushughulikiwa sambamba na mazungumzo kati ya Serikali na madereva ili kuepusha migongano inayoweza kuathiri watumiaji wengine wa barabara.
Naye Francis Joel dereva bajaji, amesema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa miundombinu rafiki katika maeneo wanayopaswa kutumia, hali inayozidisha ugumu wa shughuli zao hasa wakati wa mvua.
Amesema madereva hawapingi utaratibu wa matumizi ya barabara, lakini wanahitaji kuonyeshwa njia mbadala zinazofikika zenye miundombinu salama zinazoweza kutumiwa ili kulinda vyombo hivyo.
“Si kwamba tunataka tuendelee kutumia barabara kuu ya Tanzam bila utaratibu. Changamoto ni kwamba hakuna miundombinu ya kutosha katika maeneo tunayotakiwa kupita. Serikali ituangalie kwa jicho la tofauti kwa sababu tunachangia mapato na sisi ni sehemu ya jamii,” amesema.
Kuhusu athari za kiuchumi, amesema kimsingi maisha yao yamegeuka mateso kutokana na kukosa fedha za kujikimu na kutoa malengo kwa wamiliki wa vyombo hivyo.
“Asilimia kubwa bajaji sio mali yetu tumepewa mkataka wa kila siku kupeleka kwa tajiri Sh30,000 au Sh20,000 kulingana na makubaliano,”amesema.
Akizungumzia hatua zinazo chukuliwa dhidi ya madereva bajaji wanaoshikiliwa, Mwenyekiti wa Umoja wa Bajaji Mkoa, Lucas Mwakyusa amesema hawawezi kwenda kinyume na sheria, huku akibainisha kuwa kuna taratibu zinazoendelea kushughulikia suala hilo.
Amesema hali ya usafiri kwa sasa imeanza kuimarika, huku baadhi ya madereva wa bajaji wakirejea barabarani kutoa huduma na hakuna matarajio ya kutokea kwa vurugu.
Maguta yakishusha abilia katika stendi ya Kabwe jijini Mbeya kufuatia changamoto ya usafiri baada ya bajaji kuondolewa katika barabara kuu
“Hali kwa sasa iko shwari, baadhi ya madereva wameingia barabarani kutoa huduma na hatutarajii kutokea vurugu za aina yoyote. Wakati Serikali ikiendelea na hatua mbalimbali, pia wanatoa elimu kuhusu umuhimu wa kutii sheria,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mwakyusa amewataka madereva wa bajaji kujiendesha katika mfumo rasmi ili watambulike kisheria, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa takwimu sahihi za vyombo hivyo jijini Mbeya.
Ameeleza kuwa tangu mwaka 2012, takwimu zinaonyesha kuwa kuna bajaji 4,600, huku madereva 5,000 wakiwa wamesajiliwa, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuwepo kwa mfumo rasmi wa usajili na utambuzi wa madereva pamoja na vyombo vyao.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply