

Tanga kupiga marufuku madalali kununua machungwa shambani
Tanga. Serikali imeweka mikakati mipya ya kuimarisha kilimo cha machungwa katika wilaya za Muheza, Korogwe na Handeni mkoani Tanga, ikiwemo kuanzisha vituo maalumu vya kukusanyia mazao hayo ili kudhibiti biashara ya mashambani inayosababisha wakulima kupata kipato kidogo.
Akizungumza katika kikao cha viongozi wa mkoa na wilaya kilichofanyika leo Jumapili, Novemba 1, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian, amesema utaratibu wa madalali kwenda mashambani kununua machungwa utabadilishwa na wanunuzi wote wataelekezwa kufanya biashara katika vituo maalumu vitakavyoanzishwa.
“Tutapiga marufuku kununua mazao shambani. Madalali watafanya shughuli zao kwenye vituo vya kukusanyia machungwa,” amesema Burian.
Amesema Mkoa wa Tanga una zaidi ya wakulima 45,000 wanaojishughulisha na kilimo cha machungwa, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mfumo utakaowawezesha kunufaika na zao hilo badala ya sehemu kubwa ya faida kwenda kwa madalali.
Dk Burian amesema kwa wastani mkoa huo huzalisha takribani tani 67,000 za machungwa kwa mwaka, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji, uhifadhi na masoko ili kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza kipato cha wakulima.
Ameongeza changamoto nyingine ni kuwepo kwa mashamba yenye miti ya machungwa yenye umri wa miaka 20 hadi 30, hali inayohitaji wakulima kuanza kuhuisha mashamba yao kwa kung’oa miti ya zamani na kupanda mipya kwa awamu. Amesema mkoa pia unahitaji wawekezaji wa viwanda vya kuchakata machungwa ili kuongeza thamani ya zao hilo kupitia uzalishaji wa juisi, jamu na bidhaa nyingine.
“Machungwa ya Tanga yanafaa kwa ajili ya kutengeneza juisi na jamu, lakini hata maganda yake yana thamani kubwa kwa kuwa yanaweza kuzalisha mafuta na bidhaa nyingine,” amesema.
Mbunge wa Jimbo la Muheza, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), akizungumza kuhusu umuhimu wa kuwalinda wakulima wa machungwa dhidi ya unyonyaji wa madalali na kuboresha masoko ya zao hilo. Picha na Mbonea Herman.
Kwa upande wake, Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma, maarufu Mwana FA, amesema vituo hivyo vitasaidia kuondoa mazingira yanayowafanya wakulima kudhulumiwa, hasa wanapokuwa katika hali ngumu ya kiuchumi na kulazimika kuuza mazao yao kwa bei ndogo.
Amesema wakulima watapata nafasi ya kuuza mazao yao kwa pamoja badala ya kujadiliana na wanunuzi mmoja mmoja.
“Tunataka wakulima wetu wanufaike na jasho lao. Tusikubali hali zao za kiuchumi ziendelee kutumiwa kama fursa ya kuwanyonya,” amesema Mwinjuma.
Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, amesema taasisi hiyo imejipanga kujenga vituo vinne vya kuanzia katika maeneo ya uzalishaji wa machungwa, huku kukiwa na mpango wa kuongeza vingine kulingana na mahitaji.
Amesema vituo hivyo vitakuwa na utaratibu wa kupokea, kupima, kupanga madaraja na kuweka bei za mazao. Pia vitasaidia wakulima kuvuna kupitia vikundi vya vijana vitakavyowezeshwa kwa mikopo.
“Mkulima atapata bei nzuri zaidi kwa sababu machungwa yatapitia mfumo wa ukusanyaji, upimaji na upangaji wa madaraja kabla ya kuuzwa,” amesema Mlola.
Akisoma maazimio ya kikao hicho, Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Tanga, George Mbaga, amesema miongoni mwa maazimio ni kuharakisha ujenzi wa vituo vya kukusanyia na kuuza machungwa, kuandaa mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuongeza thamani ya zao hilo na kuimarisha usimamizi wa mikataba kati ya wakulima na wanunuzi.
“Tutahakikisha taratibu za ujenzi wa vituo hivyo zinakamilika kwa haraka na wakulima wanawezeshwa kuhusu mbinu bora za kilimo na udhibiti wa visumbufu vya machungwa,” amesema Mbaga.
Naye Juma Rashidi amesema kuanzishwa kwa vituo hivyo ni muhimu kwa kuwa kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakinyonywa na madalali wanaonunua machungwa mashambani kwa bei ndogo na kuyauza kwa faida kubwa.
Amesema mfumo mpya utawapa wakulima nafasi ya kupata bei inayolingana na thamani halisi ya mazao yao.
You may also like

Tanzania – Fire Damages Six Hotels in Zanzibar

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund


Leave a Reply