

Ulevi wa gongo kwa vijana Rombo, Moshi waibua hofu
Kilimanjaro. Unywaji wa pombe kupita kiasi, ikiwamo gongo kwa baadhi ya vijana wilaya za Rombo na Moshi mkoani Kilimanjaro, umeibua hofu kwa wadau, wakisema hali hiyo inaathiri afya, kipato na mustakabali wa familia.
Wakizungumza hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa dini na wananchi wamesema vijana wanaotumia muda mwingi kunywa pombe wanashindwa kujishughulisha na shughuli za maendeleo, kuhudumia familia na kuanzisha ndoa, hali inayoweza kuwa na athari kwa jamii kwa muda mrefu.
Msaidizi wa masuala ya kisheria Wilaya ya Rombo, Temmy Shirima amesema hali hiyo inatia wasiwasi kutokana na baadhi ya vijana kuanza kunywa pombe asubuhi badala ya kutafuta njia za kujipatia kipato.
“Asilimia kubwa ya vijana huku Rombo wameishia kwenye gongo, waliobaki ni wachache sana wanaojitambua. Sasa sijui ni kukata tamaa au ni nini kimetokea, maana wanakunywa pombe kali ili walewe mapema,” amesema.
Shirima anahusisha hali hiyo na kukata tamaa, akisema baadhi ya vijana wanapopata fedha kwa kufanya vibarua huzitumia kununua pombe badala ya kukidhi mahitaji yao.
“Ukiwaona saa 11 alfajiri unakuta wanaenda kuamsha watu madukani ili wapate pombe. Hali hii imekuwa maisha yao ya kila siku,” amesema.
Amesema athari za unywaji huo zinaonekana pia katika maisha ya familia na ndoa.
Shirima amesema katika eneo linalomzunguka kwa takribani miaka miwili hajashuhudia ndoa ikifungwa, hali anayoihusisha na changamoto zinazowakabili vijana.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Kilimanjaro, Jones Mola amesema unywaji wa pombe kupita kiasi ni changamoto inayopaswa kupewa kipaumbele kutokana na athari zake kwa familia na jamii.
Amesema matumizi ya gongo na pombe nyingine ambazo, kwa mujibu wake, hazijathibitishwa ubora wake na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), yanaongeza wasiwasi kuhusu afya za watumiaji.
“Taifa linapoteza nguvu kazi. Vijana wanazeeka mapema, wamechoka na hawana watoto. Tutafika mahali darasa lenye uwezo wa kuwa na wanafunzi 45 likakosa wanafunzi wa kutosha,” amesema.
Mtaalamu wa afya ya akili na mtafiti, Dk Kilaye Karino amesema unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kuathiri uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.
Amesema pombe huathiri mfumo wa fahamu na mawasiliano kati ya ubongo na sehemu nyingine za mwili, hali inayoweza kupunguza mwitikio wa mwili na kuathiri utendaji wa kijinsia.
“Unywaji wa pombe kupita kiasi unapunguza kasi ya mawasiliano kwenye ubongo na maeneo mengine ya mwili. Mfumo wa fahamu unapokuwa hauko katika hali nzuri, uwezo wa mwili kuitikia msisimko unaweza kupungua,” amesema.
Dk Karino ameongeza kuwa pombe inaweza kuathiri mtiririko wa damu na viwango vya homoni, ikiwamo testosterone, hali inayoweza kupunguza hamu ya tendo la ndoa na kuathiri utendaji wa kijinsia.
You may also like

Kauli ya Ubalozi wa Tanzania madai ya Mwaipaya kutekwa Nairobi

Police expose dangerous traffic violations


Leave a Reply