

Upinzani Malawi wataka maelezo Rais Mutharika kukaa Afrika Kusini
Lilongwe. Chama kikuu cha upinzani nchini Malawi, Malawi Congress Party (MCP), kimeitaka Serikali kueleza sababu za Rais Peter Mutharika kukaa muda mrefu Afrika Kusini, huku wananchi wakikabiliwa na uhaba wa mafuta, kukatika kwa umeme na upatikanaji mgumu wa dawa katika hospitali za umma.
Mutharika, mwenye umri wa miaka 86, aliondoka nchini humo Oktoba 6, 2026, kwa kile maofisa wa Serikali walichokitaja kuwa safari binafsi.
Hii ni safari yake ya tano nchini Afrika Kusini mwaka huu, huku Serikali ikitoa taarifa chache kuhusu ziara hizo.
Alhamisi, Oktoba 22, 2026, mkurugenzi wa kampeni wa MCP, Moses Kunkuyu, aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Lilongwe, chama hicho hakipingi haki ya Rais kusafiri kwa sababu binafsi, bali kinataka hatua zichukuliwe kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi.
Kunkuyu alitaka Makamu wa Rais, Jane Ansah, alizungumzie taifa kuhusu hali ya nchi na kutoa ufafanuzi wa namna Serikali inavyosimamia shughuli zake wakati Rais akiwa nje ya nchi.
“Malawi iko katika wakati muhimu, na kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti,” amesema MCP katika taarifa yake.
Kunkuyu amesema wananchi wanastahili kufahamu nani anayesimamia shughuli za Serikali wakati Rais akiwa nje ya nchi, hasa kutokana na kuongezeka kwa matatizo ya kiuchumi na huduma za msingi.
“Hoja si kwamba Rais amesafiri. Hoja ni kwamba watu wanateseka na wanataka kuhakikishiwa kuwa kuna mtu anayesimamia mambo,” amesema.
Amezitaka mamlaka kueleza mikakati ya kukabiliana na uhaba wa mafuta, kukatika kwa umeme mara kwa mara, upungufu wa dawa muhimu katika hospitali za umma na changamoto za upatikanaji wa fedha za kigeni.
Waziri wa Habari, Shadric Namalomba, amepuuzia madai kwamba kutokuwepo kwa Rais nchini kumesababisha pengo la uongozi, akisisitiza kuwa Mutharika anaendelea kusimamia shughuli za Serikali.
“Rais wa nchi huwa anasimamia mambo wakati wote, popote alipo,” amesema Namalomba alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari vya ndani.
Alipoulizwa kuhusu madhumuni ya safari hiyo, waziri huyo alisema: “Safari binafsi ni ya binafsi.”
Namalomba aliishutumu kambi ya upinzani kwa kutumia changamoto zinazoikabili nchi kisiasa, akidai kuwa baadhi ya matatizo hayo yalitokana na utawala uliopita.
“Hiyo ndiyo sababu Wamalawi waliwapigia kura na kutuingiza madarakani sisi, si wao. Naomba wafunge midomo yao tunaposhughulikia matatizo waliyoyasababisha na kushindwa kuyatatua,” amesema.
Alhamisi, Mutharika alimpa jukumu Waziri wa Biashara kuongoza ujumbe wa Malawi katika mkutano wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) uliofanyika Zimbabwe.
Mapema mwezi huu, maofisa wa Serikali walikanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilizodai kuwa Mutharika alikuwa ametoka Afrika Kusini na kwenda India kwa matibabu.
Katibu Mkuu wa Serikali, Justin Saidi, alisema Rais alikuwa bado nchini Afrika Kusini na kuwataka wananchi kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa.
Awali, Mutharika amewahi kupuuza uvumi kuhusu afya yake, akieleza madai hayo kuwa ya kipuuzi na ya kuchekesha, huku akisisitiza kuwa anaendelea vizuri.
Malawi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni, hali iliyovuruga uagizaji wa mafuta kutoka nje na kuchangia kupanda kwa gharama za usafiri.
Uhaba huo umesababisha foleni ndefu katika vituo vya mafuta, huku huduma zisizotabirika za umeme na upungufu wa dawa vikiongeza malalamiko ya wananchi.
Mutharika alirejea madarakani Oktoba mwaka jana baada ya kumshinda aliyekuwa Rais, Lazarus Chakwera. Awali, aliiongoza Malawi kuanzia mwaka 2014 hadi 2020.
Kutokuwepo kwake nchini kwa muda mrefu kumeongeza uchunguzi wa umma kuhusu safari zake za mara kwa mara nchini Afrika Kusini na kiwango cha taarifa zinazotolewa na Serikali kuhusu ziara hizo.
You may also like

Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade

Samia to inaugurate Sh700bn Government City on October 30


Leave a Reply