

Utoro kazini wasumbua tume, yajipa siku 60 kufanya utafiti
Dodoma. Utoro kazini umeendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazojitokeza katika mashauri ya watumishi wa umma, hali iliyosababisha Tume ya Utumishi wa Umma kuamua kufanya utafiti ili kubaini namna bora ya kukabiliana na tatizo hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo, Alhamisi, Oktoba 22, 2026 na Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Nolasco Kipanda wakati akitoa taarifa ya mkutano wa kwanza wa Tume kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Hamisa Kalombola, ulifanyika kuanzia Septemba 21 hadi Oktoba 16, 2026, katika ofisi za Tume zilizopo Mji wa Serikali wa Mtumba, jijini Dodoma.
Kipanda amesema katika mkutano huo Tume ilipokea rufaa na malalamiko 74, huku utoro kazini ukiwa miongoni mwa masuala yaliyojitokeza kwa wingi na kuifanya Tume kuamua kufanya utafiti ili kupata mapendekezo yatakayosaidia kuzishauri mamlaka husika.
“Tulichukua maeneo matano ambayo tunaona yana shida. Katika hayo, utoro kazini unaongoza, ukifuatiwa na kushindwa kutekeleza majukumu, wizi wa mali za umma na rushwa, kughushi vyeti na kutoa taarifa za uongo,” amesema Kipanda.
Amesema malalamiko yaliyowasilishwa na kuamuliwa na Tume yalihusu kupinga kutenguliwa katika cheo, kutorudishwa kazini, kusitishiwa ajira, kuondolewa kwenye orodha ya mishahara na kutopandishwa cheo.
Kwa mujibu wa Kipanda, kati ya mashauri yaliyopokewa, rufaa zilikuwa 57 na malalamiko 17.
Amesema katika kipindi hicho, warufani 18 na mrufaniwa mmoja walifika mbele ya Tume kusikilizwa, huku mamlaka mbili za nidhamu zikialikwa na kufika mbele ya Tume kuhojiwa kutokana na ukiukwaji wa sheria katika kushughulikia mashauri ya watumishi walio chini yao.
“Aidha, Tume katika kipindi hiki cha mkutano ilifanya ziara katika taasisi 14 za Serikali zilizopo mkoani Dodoma kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala ya utumishi wa umma,” amesema.
Kiongozi huyo amezitaka mamlaka za ajira na nidhamu kuzingatia sheria wakati wa kushughulikia malalamiko na mashauri ya kinidhamu ya watumishi, ili kuhakikisha haki inatendeka na inaonekana kutendeka.
Kuhusu utafiti wa kubaini namna ya kukabiliana na utoro kazini, Kipanda amesema Tume imejiwekea kipindi cha miezi miwili, sawa na siku 60 kuanzia Oktoba 22, 2026, ili kukamilisha kazi hiyo na kuweka hadharani matokeo yatakayopatikana kabla ya kuishauri mamlaka husika hatua za kuchukua.
Amesema lengo la Tume ni kuona malalamiko na rufaa za watumishi wa umma yanapungua kwa kiasi kikubwa, akieleza kuwa hilo linawezekana iwapo waajiri na waajiriwa watazingatia sheria na taratibu za utumishi wa umma.
You may also like


Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade


Leave a Reply