

Wataalamu 300 kukutana Arusha, TMA yazungumzia El Nino
Arusha. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa utakaowakutanisha wataalamu 300 wa sayansi ya mabadiliko ya tabianchi kutoka nchi 75, wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitoa tahadhari ya kuimarika kwa mfumo wa El Nino na kuongezeka kwa mvua katika miezi ya Novemba na Desemba.
Mkutano huo unaotarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kesho Jumatatu, Novemba 2, 2026, utajadili masuala ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, sababu zake, athari na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana nayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumapili, Novemba mosi, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a, amesema mkutano huo utafanyika jijini Arusha kuanzia Novemba 2 hadi 6, 2026.
Akizungumzia hali ya hewa, Dk Chang’a amesema mfumo wa El Nino upo na unaendelea kuimarika, kama ilivyoelezwa katika utabiri uliotolewa na mamlaka hiyo Agosti 18 na Oktoba 23, mwaka huu.
“Tunaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa tunazozitoa na kuzingatia tahadhari ambazo tutaendelea kuzitoa kwa nyakati tofauti kadri itakavyohitajika. Kazi yetu ni ya kisayansi na usahihi wa taarifa zetu ni zaidi ya asilimia 88,” amesema.
Amesema takwimu za asubuhi ya jana zilionesha maeneo mbalimbali yakiendelea kupata mvua, akitolea mfano kituo cha Tanga kilichopima milimita 57.
Dk Chang’a amesema utabiri wa Oktoba ulionesha mvua zingekuwa zimeanza kunyesha katika Ukanda wa Ziwa Victoria, unaojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza na Mara, kuanzia wiki ya nne ya Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba.
Amesema mvua hizo zimeanza kunyesha kama ilivyotabiriwa, huku baadhi ya maeneo yakipata kiasi kilichozidi wastani, ikiwemo Bukoba mkoani Kagera.
Pia, katika Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, unaojumuisha Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Mafia, Unguja, Pemba na kaskazini mwa Morogoro, mvua zilitarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba, zikiwa za wastani au juu ya wastani.
Amesema mvua zimeendelea kunyesha katika maeneo hayo kwa mujibu wa utabiri na zinatarajiwa kuongezeka zaidi mwezi huu na kuelekea Desemba.
Kwa mujibu wa Dk Chang’a, utabiri uliotolewa Oktoba 23 ulihusu pia maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, kuanzia Novemba hadi Aprili.
Maeneo hayo ni Ukanda wa Magharibi unaojumuisha Tabora, Kigoma na Katavi pamoja na maeneo ya kusini, na Nyanda za Juu Kusini Magharibi zinazojumuisha Iringa, Njombe, Songwe na Mbeya.
Amesema katika Ukanda wa Magharibi mvua zilitabiriwa kuanza wiki ya nne ya Oktoba na wiki ya kwanza ya Novemba, huku katika Nyanda za Juu Kusini Magharibi zikitarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba.
“Kwa hiyo, sasa tuko katika msimu wa mvua nchini kote. Tunatarajia mvua kuendelea kuimarika hata katika maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka. Katika maeneo mengine ambayo tayari mvua zimeanza kunyesha, tunatarajia zitaendelea kuimarika mwezi huu wa Novemba kuelekea Desemba,” amesema.
Wataalamu kujadili tathmini ya tabianchi
Akizungumzia mkutano huo, Dk Chang’a amesema Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa wanasayansi bingwa wa mabadiliko ya tabianchi kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa ndani.
Amesema mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya Tathmini ya Saba ya Kisayansi ya Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), inayochunguza mwenendo wa mabadiliko ya tabianchi duniani, sababu zake na athari zinazoweza kujitokeza katika siku zijazo.
IPCC lilianzishwa mwaka 1988 na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) pamoja na Programu ya Umoja wa Mataifa ya Mazingira (UNEP), likiwa na jukumu la kutathmini ushahidi wa kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Tathmini zake hutumiwa na nchi mbalimbali kuandaa sera na kuchukua hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi joto, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.
Dk Chang’a amesema Tathmini ya Saba (AR7) inahusisha masuala mbalimbali, ikiwamo ongezeko la joto duniani, uzalishaji wa gesi joto na matukio makubwa ya hali ya hewa kama mvua kubwa, upepo mkali, joto kali, ukame, mafuriko na mifumo ya El Nino.
“Mojawapo ya masuala yanayofanyiwa tathmini ni matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo joto kali, upepo mkali, mvua kubwa, ukame, mafuriko na mifumo ya El Nino, ambayo wataalamu wanachunguza iwapo yataendelea kuongezeka na kwa kiwango gani,” amesema.
Amesema tathmini hiyo itachunguza pia mwenendo wa uzalishaji wa gesi joto kadri shughuli za maendeleo zinavyoendelea na matokeo yake yanatarajiwa kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka 2029.
“Hii ni tathmini ya muda mrefu, si tathmini ya mwaka mmoja mmoja. Masuala haya yote yanafanyiwa tathmini ya kina na wanasayansi bingwa duniani,” amesema.
Wananchi wataka taarifa kwa wakati
Mmoja wa wakazi wa Arusha, Neema Saitoti, amesema utabiri wa hali ya hewa ni muhimu kwa sababu huwapa wananchi nafasi ya kujiandaa kabla ya mvua kubwa au majanga mengine kutokea.
“Tunapopata taarifa mapema, tunaweza kuchukua tahadhari za kulinda familia zetu na mali zetu badala ya kusubiri madhara yatokee,” amesema.
Amesema taarifa za mvua huwasaidia pia wakulima kupanga shughuli zao, hasa wakati wa kupanda na kuvuna mazao, ili kuepuka hasara zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi au ukame.
Ameshauri mamlaka kuendelea kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati na kwa lugha rahisi ili ziweze kueleweka na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
You may also like

Tanzania – Fire Damages Six Hotels in Zanzibar

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund


Leave a Reply