

Zanzibar kukutanisha wataalamu kujadili uchumi wa buluu, tabianchi
Unguja. Wataalamu wa mazingira kutoka Tanzania na nchi mbalimbali wanatarajiwa kukutana Zanzibar kujadili fursa za uchumi wa buluu, changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.
Jukwaa hilo lililoandaliwa na Jumuiko la Taasisi za Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (Zacca), linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia kesho Jumamosi Oktoba 24 hadi 26, 2026.
Akizungumza leo Ijumaa, Oktoba 23, 2026, mjini Unguja, Mkurugenzi Mtendaji wa Zacca, Mahfoud Haji amesema jukwaa hilo litawakutanisha wadau kutoka serikalini, sekta binafsi, asasi za kiraia na wanaharakati wa mazingira kwa lengo la kujadili changamoto za sekta hiyo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.
“Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa mikakati ya uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya fursa zinazotokana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Amesema washiriki kutoka Tanzania na nchi nyingine, zikiwemo Ujerumani, Ethiopia na Kenya, watashiriki majadiliano yatakayojikita katika masuala ya kimkakati kuhusu mazingira, uchumi wa buluu na maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Haji, katika siku hizo tatu kutakuwa na maonyesho ya shughuli za taasisi zinazojihusisha na mazingira, pamoja na vipindi 12 vya majadiliano vitakavyowakutanisha wataalamu kutoka serikalini, wizara na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Amesema mada zitakazojadiliwa ni pamoja na namna ya kuendeleza uchumi wa buluu kwa njia endelevu, kutumia taka kama chanzo cha fursa za kiuchumi na kuimarisha matumizi ya nishati safi.
Amesisitiza kuwa uchumi wa buluu ni muhimu kwa Zanzibar kutokana na fursa zilizopo katika rasilimali za bahari, hivyo shughuli za kiuchumi zinapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira.
Kuhusu usimamizi wa taka, Haji amesema majadiliano yataangazia namna ya kuzibadili kuwa bidhaa zenye thamani, zikiwemo mbolea, ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi.
Ameeleza kuwa jukwaa hilo litakuwa na vipengele vitatu vikuu ambavyo ni maonyesho ya shughuli za wadau wa mazingira, majadiliano ya kitaalamu na utoaji wa tuzo kwa vinara wa mazingira Zanzibar.
Amesema shughuli hizo zitahitimishwa Oktoba 26 kwa kufanyika kwa usiku wa tuzo za vinara wa mazingira, utakaolenga kutambua mchango wa wadau katika uhifadhi wa mazingira na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Mjini, Mohammed Ibrahim Hassanali, maarufu Razalee, ameipongeza Zacca na wadau wengine kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kudhibiti taka na kuboresha usafi wa miji.
Amesema jukwaa hilo litatoa fursa kwa taasisi za Serikali, ikiwemo manispaa, kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kusimamia taka na kuzitumia kama fursa za kiuchumi.
Razalee amesema ubunifu wa kuzalisha mbolea na bidhaa nyingine kutokana na taka unaweza kuongeza shughuli za uzalishaji na kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato.
Ameongeza kuwa Manispaa ya Mjini ina mikakati ya kuimarisha usafi wa mazingira sambamba na uwekezaji unaofanywa na Serikali Kuu.
Akitaja baadhi ya mikakati hiyo, amesema manispaa inashirikiana na vikosi vya Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), pamoja na kutafuta mwekezaji mwenye uwezo wa kusafisha, kukusanya na kusarifu taka ili kupunguza kero ya uchafu katika maeneo ya manispaa hiyo.
You may also like


Tanzania: Dar, Nairobi Step Up Efforts to Ease Crossborder Trade


Leave a Reply