

Zanzibar kunufaika na umeme, mabilioni ya uwekezaji Korea
Unguja. Ziara ya kikazi ya siku nne nchini Korea Kusini ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, imefungua fursa za ushirikiano katika sekta ya nishati, uwekezaji na utalii, huku Zanzibar ikipata nafasi ya kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Kimataifa la Sera za Utalii kwa Visiwa (ITOP) mwaka 2027.
Miongoni mwa matokeo ya ziara hiyo ni mazungumzo kuhusu suluhisho la kudumu la changamoto ya umeme Zanzibar, kuvutia kampuni za Korea Kusini kuwekeza katika miradi ya kimkakati na kukabidhiwa bendera ya uenyeji wa ITOP 2027.
Ziara hiyo ilianza Oktoba 27, 2026, Rais Mwinyi akiwa ameambatana na mkewe, Mama Mariam Mwinyi, na ujumbe wake. Ilikamilika Oktoba 30, 2026, jijini Seoul.
Mchambuzi wa Diplomasia na Uchumi wa Kimataifa, Haji Salum, amesema Korea Kusini ni nchi ambayo Zanzibar inaweza kujifunza uzoefu wake wa maendeleo ya viwanda na uchumi wa bahari.
“Korea Kusini imetoka kwenye umaskini hadi kuwa taifa la teknolojia kwa miaka 40 tu kwa kutumia bahari na viwanda. Zanzibar inajaribu kuiga mfumo huo. Mazungumzo ya umeme na WG Corporation na Posco yanaonesha Zanzibar inataka kujitoa kwenye utegemezi wa umeme wa Bara,” amesema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa utalii na uchumi wa buluu, Asmaa Saidi, amesema kukabidhiwa uenyeji wa ITOP 2027 ni fursa ya kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Hata hivyo, amesema ni muhimu kuhakikisha miradi ya Mice na Hospitali ya Binguni inayozungumziwa na kampuni za Heerim na Samoo inatekelezwa kwa wakati.
Naye mchambuzi wa nishati na miundombinu, Haroub Mohamed, amesema mipango ya kuimarisha upatikanaji wa umeme na kurejesha reli inaweza kusaidia kuvutia viwanda na kukuza utalii.
“Zanzibar haiwezi kuvutia viwanda na utalii wa hali ya juu kama umeme ni wa kukatika na usafiri ni wa magari tu. Kama Korea itawekeza kwenye gridi ndogo za umeme wa jua na upepo pamoja na reli ya utalii, gharama za uzalishaji zitashuka na ajira za vijana zitaongezeka,” amesema.
Kwa upande wa wananchi, mvuvi na mkulima wa mwani kutoka Paje, Ali Juma, amesema ana matumaini ushirikiano huo utasaidia kuongeza thamani ya mwani na kipato cha wakulima.
“Kama Rais ameenda Korea na kuona jinsi mwani unavyochakatwa kuwa chakula na vipodozi, basi alete huo mtambo hapa Zanzibar, tunataka bei ipande,” amesema.
Mfanyabiashara wa utalii kutoka Forodhani, Mwanaisha Khamis, amesema uenyeji wa ITOP 2027 ni fursa kwa wafanyabiashara wadogo, lakini amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma za maji na umeme kabla ya wageni kuwasili.
“Hii mikataba ya Korea ya maji na umeme itekelezwe haraka, sio makaratasi tu,” amesema.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, wakati akipeperusha bendera ya ITOP katika mkutano wa Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (27th Inter-Islands Tourism Policy Forum – ITOP 2026), ambapo Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo mwakani
Katika siku ya kwanza ya ziara, Rais Mwinyi alitembelea Jiji la viwanda la Yeosu na kufanya mazungumzo na Meya wa jiji hilo, Seo Young-hak.
Alisema Zanzibar inalenga kuimarisha ushirikiano na Korea Kusini katika utalii, uchumi wa buluu, nishati mbadala, viwanda, teknolojia na elimu.
Alieleza Zanzibar inahitaji kunufaika na uzoefu wa Korea katika uvuvi wa kisasa, ufugaji wa samaki, uhifadhi wa mazao kwa teknolojia ya ubaridi na uchakataji wa mwani ili kuongeza thamani na kipato cha wakulima na wavuvi.
Akiwa Yeosu, Rais Mwinyi alitembelea kampuni ya chuma ya Posco Gwangyang kujionea teknolojia ya uzalishaji viwandani inayozingatia utunzaji wa mazingira.
Pia alitembelea kampuni ya K-Food Goheung-gun inayozalisha na kuchakata bidhaa za mwani, kabla ya kushiriki Maonesho ya Dunia ya Visiwa 2026 (World Island Exhibition).
Suluhisho la umeme Zanzibar
Oktoba 28, Rais Mwinyi alikutana na uongozi wa kampuni ya WongWang Electric Power Corporation (WG Corporation), mjini Yeosu, kujadili uwezekano wa kushirikiana katika kutafuta suluhisho la changamoto ya umeme Zanzibar.
Alisema Zanzibar bado inategemea umeme kutoka Tanzania Bara, huku ikikabiliwa na upungufu wa nishati hiyo, hivyo Serikali inaendelea na juhudi za kuongeza uzalishaji wa ndani.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zilijadili uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati mbadala, mifumo ya gridi ndogo na teknolojia ya kuhifadhi nishati kwa matumizi ya visiwa vidogo.
Dk Mwinyi alisema kampuni hiyo imeonesha utayari wa kutuma wataalamu Zanzibar kufanya tathmini ya mahitaji ya kiufundi baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Zanzibar kuwa mwenyeji ITOP 2027
Kutoka Yeosu, Rais Mwinyi alielekea Kisiwa cha Jeju kushiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (ITOP Forum 2026).
Katika mkutano wa viongozi wa ITOP uliofanyika Jeju Stone Park, uliowakutanisha wawakilishi wa maeneo 12 wanachama na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), alisema jukwaa hilo linapaswa kuzalisha hatua za vitendo na matokeo yanayowanufaisha wananchi.
Alisema lengo la Zanzibar si kuongeza idadi ya watalii pekee, bali kuhakikisha sekta hiyo inakuza biashara za ndani na kulinda urithi wa asili na utamaduni.
Oktoba 29, Rais Mwinyi alikabidhiwa rasmi bendera ya ITOP na Gavana wa Jeju, Wi Seong-gon, ikiwa ni ishara ya Zanzibar kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo mwaka 2027.
Uenyeji huo utaipa Zanzibar nafasi ya kuwakutanisha viongozi na wadau wa utalii kutoka maeneo mbalimbali duniani na kutangaza vivutio vyake.
Katika mazungumzo na Gavana Wi, Rais Mwinyi pia alipendekeza kuanzishwa kwa ushirikiano wa kindugu kati ya Zanzibar na Jeju.
Alisema Zanzibar inaweza kujifunza kutoka Jeju katika usimamizi wa utalii, utalii wa mazingira na matumizi ya nishati ya jua na upepo, ambayo yanachangia takribani asilimia 30 ya umeme wa kisiwa hicho. Gavana huyo aliahidi kuanzisha majadiliano ya kitaalamu.
Wawekezaji wa Korea kuangalia miradi Zanzibar
Akiwa Seoul, Rais Mwinyi alikutana na viongozi wa kampuni tano za Korea Kusini ambazo ni K-FINCO, Heerim, Sejong Plant, Samoo C.M. Architects & Engineers na Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd (SSRST).
Mazungumzo yalihusu uwezekano wa kampuni hizo kushiriki katika miradi ya bandari, usafiri wa baharini, barabara, miundombinu ya mijini, nishati mbadala, utalii na viwanda.
Kampuni ya Heerim ilieleza kuwa imeandaa mpango wa maendeleo wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar (Mice).
Nayo Samoo C.M. ilionesha uwezo wake katika ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni, ambayo Rais Mwinyi alisema itahitaji vifaa tiba vya kisasa na mifumo bora ya uendeshaji ili kutoa huduma za afya na mafunzo.
Kampuni ya Sejong Plant ilionesha nia ya kushiriki katika miradi ya maji safi, usafishaji wa maji taka, kuagiza mazao ya uvuvi kutoka Zanzibar na kuwekeza katika mifumo ya uhifadhi wa mazao kwa ubaridi.
Wakati huohuo, Sung Shin Rolling Stock ilionesha nia ya kushirikiana na Serikali katika mradi wa kurejesha huduma za reli ya abiria na utalii Zanzibar.
Rais Mwinyi aliwakaribisha wawekezaji hao kutumia fursa zilizopo Zanzibar, hususan katika uchumi wa buluu, bandari, viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na masoko ya Afrika Mashariki na Soko Huru la Afrika (AfCFTA).
You may also like

Tanzania – Fire Damages Six Hotels in Zanzibar

Government scraps collateral, interest on Sh200 billion youth fund


Leave a Reply