

Zanzibar kuvutia viwanda vya samani za hoteli, vyakula kutoka China
Unguja. Ukuaji wa sekta ya utalii Zanzibar umeibua fursa mpya za uwekezaji katika viwanda vinavyozalisha samani za hoteli, kusindika vyakula na bidhaa nyingine zinazohitajika katika mnyororo wa thamani wa utalii.
Kutokana na fursa hizo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewahakikishia wawekezaji kutoka China kuwa itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha kuwekeza katika sekta za viwanda, biashara na huduma.
Hayo yameelezwa jana Jumapili, Novemba mosi, 2026 na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alipokuwa akitoa hotuba katika Mkutano wa Yellow River Basin Enterprise Going Global and Comprehensive Services Exchange and Matchmaking Conference uliofanyika mjini Jinan, Jimbo la Shandong, China.
Mkutano huo uliowakutanisha wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara zaidi ya 700 kutoka maeneo mbalimbali ya Bonde la Mto Manjano, ulilenga kutekeleza Mpango wa Belt and Road Initiative (BRI) na kuunganisha rasilimali kwa kampuni zinazotaka kupanua shughuli zake kimataifa.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kitengo cha habari cha wizara hiyo, Omar amesema Zanzibar ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotumiwa katika sekta ya utalii kutokana na ongezeko la wageni wanaotembelea visiwa hivyo.
Amesema mwaka 2025 pekee, Zanzibar ilipokea watalii 917,000, idadi inayoonesha ukubwa wa soko na mahitaji ya bidhaa zinazoweza kuzalishwa ndani ya nchi.
“Vivutio vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na rasilimali watu vinaweza kutumika kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Omar.
Ameongeza kuwa fursa hizo hazipo katika utalii pekee, bali pia katika sekta za viwanda, biashara na huduma zinazohusiana na utalii pamoja na mikutano ya kimataifa (MICE).
Katika mkutano huo, Naibu Gavana wa Jimbo la Shandong, Wen Nuan, alieleza mikakati ya Serikali ya watu wa China katika kukuza uchumi kupitia mpango wa Going Global, akisema jimbo hilo ni miongoni mwa maeneo muhimu na ya kimkakati katika sekta ya viwanda nchini humo.
Shandong ni jimbo la tatu kwa ukubwa wa pato nchini China, likiwa na pato linalokadiriwa kuvuka Yuan 10 trilioni mwaka 2025.
Omar alimshukuru Naibu Gavana huyo kwa kukubali ombi la kuandaa misafara ya wawekezaji kutoka China kutembelea Zanzibar ili kujionea hatua zilizofikiwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Omar yupo nchini China kwa ziara ya kikazi ya siku 10, iliyoanza Oktoba 26 na inatarajiwa kukamilika Novemba 4, 2026, kufuatia mwaliko rasmi kutoka Serikali ya Jimbo la Shandong na waandaaji wa mkutano huo.
Katika kuendeleza ushirikiano huo, anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Manispaa ya Jinan, kutembelea maeneo mbalimbali ya viwanda (Industrial Parks) na kukutana na wamiliki wa viwanda.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa ziara hiyo imeanza kuonesha matokeo, baada ya baadhi ya wawekezaji kuonesha kuvutiwa na fursa za biashara na uwekezaji Zanzibar, hususan katika sekta za viwanda na huduma zinazohusiana na mnyororo wa thamani wa utalii.
You may also like

Tanesco yatekeleza agizo la Ndejembi la Novemba 15

Chadema issues conditions before reconciliation

Leave a Reply