

RC Sagini ataka vijana kuchangamkia mikopo ya Serikali kujiajiri
Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amewataka vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali nchini kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali ili kuanzisha miradi ya kiuchumi na kujiajiri, badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na changamoto ya upatikanaji wa ajira nchini, huku akiwahimiza vijana kutumia elimu na ujuzi walioupata kujiendeleza kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Sagini ameyasema hayo leo Jumamosi, Novemba 7, 2026, katika mahafali ya 11 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki (CUoM), Mkoa wa Mbeya, ambapo jumla ya wanafunzi 4,096 wamehitimu katika ngazi mbalimbali za elimu.
Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika kukuza sekta ya elimu, hususan katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wanaosaidia kutekeleza majukumu mbalimbali ya maendeleo ya taifa.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira yanayowezesha vijana kupata fursa za kiuchumi, ikiwemo kushiriki katika zabuni na manunuzi ya umma kupitia utaratibu unaotenga asilimia 30 ya manunuzi kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Kwa kujua uwepo wa fursa hii, wahitimu wanapaswa kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika nayo. Mnaporejea kwenye jamii, nendeni katika ofisi za maendeleo ya jamii kupata nafasi na maelekezo ya ushirikiano,” amesema.
Amesema fursa hizo hazipo katika ngazi ya Serikali Kuu pekee, bali pia katika halmashauri na mikoa, hivyo kuwataka vijana kuzitumia kujenga msingi wa kujitegemea kiuchumi.
“Vijana wahitimu, kutokana na changamoto ya soko la ajira nchini, tumieni fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kuanzisha miradi itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Pia amewataka kutumia fursa hiyo ili kupata asilimia 30 kupitia mfumo wa manunuzi ya Serikali kwa kujiunga katika vikundi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewataka wahitimu kuitumia elimu waliyoipata kama nyenzo muhimu ya kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.
Itunda amesisitiza umuhimu wa wahitimu kumtanguliza Mungu katika kila hatua wanayochukua wanaporejea katika jamii, huku wakitumia maarifa na ujuzi wao kwa manufaa ya wengine.
Akisoma taarifa ya chuo, Makamu Mkuu wa CUoM, Profesa Romuald Haule, amesema mahafali hayo ni ya 11 na kwamba jumla ya wanafunzi 4,096 wamehitimu, wakiwemo wanawake 2,175.
Amewataka wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata kwa manufaa yao, jamii na taifa, huku akiwapongeza wazazi, walezi, ndugu, jamaa na wadau mbalimbali waliochangia safari yao ya elimu.
Pia ameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya elimu ya juu, pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa juhudi za kuboresha sekta hiyo.
Profesa Haule amesema chuo kinaendelea kuboresha programu za elimu ya juu, miundombinu ya majengo na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), sambamba na kuimarisha tafiti zinazolenga kutatua changamoto za jamii na taifa.
Amewahimiza wahitimu kumtanguliza Mungu katika kila jambo, kutumia elimu yao kwa uadilifu na kuwa wazalendo katika kulitumikia taifa.
Mmoja wa wahitimu Monica Daudi amesema kwa mwaka huu mwamko wanawake katika chuo hicho umekuwa mkubwa kutokana na mazingira wezeshi yaliyofanywa na Serikali katika elimu ya vyuo vikuu nchini.
You may also like

Sh2.04 trilioni zilivyogusa kilimo,elimu,afya na ajira



Leave a Reply