

Wafugaji 43 Kilosa wadaiwa kuchochea migogoro
Kilosa. Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka ameagiza kukamatwa wafugaji 43 wanaotuhumiwa kuchochea migogoro kati yao na wakulima huku wakidaiwa kuwakatisha watoto masomo yao kwa ajili ya shughuli zao.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Shaka amesema watuhumiwa hao, pia wamekuwa vinara wa kuzururisha mifugo na kulisha kwenye mashamba ya wakulima hasa ya mahindi, mpunga na mbaazi.
Amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na Serikali ya wilaya kwa miezi sita, umebaini kuwa, wapo watoto 94, kutoka jamii za kifugaji hasa wamaasai na wasukuma, wamekatishwa masomo na kupewa jukumu la kuchunga mifugo.
“Watoto hawa wana umri chini ya miaka 18 na wapo ambao wanachunga mifugo ya wazazi wao lakini wapo ambao wanachunga kwa ujira, yaani wameajiriwa na wengi wao wanatoka mikoa ya jirani na tayari wameelekezwa na waajiri wao kupiga wakulima, kutoa lugha chafu za matusi na za kukera kwa wakulima na hata viongozi wa vijiji. Sitakubali hili,” amesema Shaka.
“Migogoro ya wakulima na wafugaji inafanya hali ya uhusiano wa makundi haya isiwe nzuri. Sisi viongozi muda wote tumekuwa tukifanya oparesheni na doria za mara kwa mara kuhakikisha kila mwananchi wa Kilosa anafanya shughuli zake kwa amani na usalama.”
Shaka amesema kitendo cha wafugaji hao wanaojiita ‘wakubwa’ kulisha kwenye mashamba ya wakulima, kimesababisha ofisi yake ndani ya miezi sita ipokee malalamiko ya wakulima 187 huku ekari 312 za mahindi, mpunga, mbaazi na mazao mengine zikiharibiwa na mifugo na kusababisha hasara kwa wakulima.
Mifugo ikiwa imeingizwa kwenye shamba na kusababisha hasara Kwa mkulima mwenye shamba hilo. Picha Hamida Shariff
“Ifahamike kuwa Wilaya ya Kilosa ina wakazi zaidi ya 700,000, kati ya hao, asilimia 80 wanajihusisha na kutegemea kilimo kama nyezo ya uchumi huku asilimia tisa hadi 10 ndio wanaotegemea ufugaji, hivyo lazima makundi haya yote yameshimiane,” amesema Shaka.
Amesema kwa sasa migogoro ya wakulima na wafugaji ipo kwenye kata 10 kati ya 40 zilizopo wilayani humo, tayari vinara wa migogoro hiyo wamewabaini kwa majina na idadi ya mifugo waliyonayo ipo mikakati iliyowekwa kukomesha migogoro hiyo.
“Nimeliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha wafugaji hao vinara wa migogoro na wanaowatumikisha watoto kuchunga mifugo, wanakamatwa,” amesema Shaka.
“Ni marufuku kuwapa watoto mifugo wakachunge.”
Baadhi ya wafugaji wilayani humo wamesema kutumia sheria bila ya kuboresha miundombinu ya wafugaji ikiwamo malisho na marambo kutawafanya wafugaji hao wawe maskini kutokana na faini watakazolipishwa.
Mfugaji kutoka Kata ya Kitete, Lepapa Kidole amesema vijiji vingi havina miundombinu ya wafugaji hali inayosababisha kutembeza mifugo yao kutafuta malisho na maji hasa kiangazi.
Mkuu wa wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka (aliyeshika kofia mkononi) akiongoza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, wataalamu wa Halmashauri viongozi wa kata na vijiji kwenye oparesheni ya kuondoa mifugo kwenye mashamba ya wakulima, vyanzo vya maji na maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo misitu. Picha Hamida Shariff
“Hizi sheria zinazotaka kutumika kwetu ni ‘ngumu kumeza’ maana hatuna miundombinu, tunalazimika kutembeza mifugo kwenda kulisha na kunywesha maji. Kama ambavyo wenzetu wakulima wanawekewa miundombinu ya kilimo na kupewa elimu, basi na sisi tuangaliwe,” amesema.
Mwenyekiti wa wafugaji Kata ya Tindiga, Phelemoni Karao amesema amekuwa akiwakanya wafugaji wanaovunja sheria.
“Kuna wafugaji hawaheshimu hata viongozi wao wa kikabila, wamekuwa wakiingia kwa nguvu kwenye mashamba na kuuawa wakulima. Mimi nimezaliwa hapa Kilosa, Kijiji cha Malangali, wananchi wananiheshimu kwa sababu mifugo yangu haiingii kwenye shamba la mtu,” amesema Karao.
Wafugaji wa jamii ya kimaasai wakazi wa Kilosa wakiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuingiza mifugo kwenda mashamba na maeneo yaliyokatazwa kisheria, wa kwanza kushoto ni mkuu wa wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka aliyeongoza msako huo. Picha Hamida Shariff
Mmoja wa wakulima wilayani humo, Abdalah Rashid amesema sehemu kubwa ya wilaya hiyo inatumika kwa kilimo, hata hivyo viongozi wa vijiji wamekuwa wakiuza maeneo hayo kwa wafugaji wanaotoka nje ya Kilosa na kusababisha uvunjivu wa amani.
Ameishauri Serikali kuwarejesha wafugaji kwenye vijiji vyao vilivyotengwa na kuwawekea miundombinu ya ufugaji na iwape elimu ya kupunguza mifugo kwa kuuza na kuwekeza kwenye biashara nyingine.




Leave a Reply