

TMA yatabiri mvua kubwa, yatahadharisha mafuriko msimu wa Novemba-Aprili
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mbalimbali nchini katika msimu wa Novemba 2026 hadi Aprili 2027, huku ikionya kuhusu uwezekano wa mafuriko, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu.
Kwa mujibu wa utabiri uliotolewa leo, Oktoba 23, 2026, mvua nyingi zaidi zinatarajiwa kunyesha katika nusu ya kwanza ya msimu, kuanzia Novemba hadi Januari, ikilinganishwa na kipindi cha Februari hadi Aprili mwakani.
Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladslaus Chang’a, amesema mwenendo huo wa mvua unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, inayohusishwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali kufuatilia utabiri wa kila siku, siku 10 na kila mwezi ili kupata taarifa zinazozingatia mabadiliko ya hali ya hewa katika maeneo yao.
Katika utabiri huo, mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa, pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro, inatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani.
Kwa upande mwingine, mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
“Mvua za msimu zinatarajiwa kuanza kusambaa katika maeneo mengi mwezi Novemba, ingawa baadhi ya maeneo ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara yanatarajiwa kuanza kupata mvua hizo kuanzia wiki ya nne ya Oktoba na wiki ya kwanza ya Novemba.”
TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika maeneo mengi kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili 2027, huku baadhi ya maeneo ya magharibi na nyanda za juu kusini magharibi yakitarajiwa kuendelea kupata mvua hadi wiki ya kwanza ya Mei.
Katika Kanda ya Kati, inayojumuisha Dodoma na Singida, mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili na ya tatu ya Novemba na kuisha mwishoni mwa Aprili.
Kwa Mkoa wa Ruvuma, mvua zinatarajiwa kuanza baadaye, katika wiki ya kwanza na ya pili ya Desemba, na kuisha mwishoni mwa Aprili.
El Niño kuongeza uwezekano wa mvua
Wakati huo huo, Dk Chang’a amebainisha kuwa mifumo ya bahari na upepo inatarajiwa kuimarisha hali ya mvua nchini, ikiwemo upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo kuelekea maeneo ya magharibi na Kanda ya Kati.
“Pia, joto la bahari katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa juu ya wastani ikilinganishwa na eneo la mashariki, hususan katika nusu ya kwanza ya msimu,” amesema.
Amesema hali hiyo inatarajiwa kusaidia kuimarisha mifumo inayosababisha mvua katika maeneo mengi ya nchi.
Amesema mvua za Vuli katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, yakiwemo maeneo ya Ziwa Victoria, kaskazini mwa nchi na ukanda wa pwani, zimeanza kunyesha katika baadhi ya maeneo kama ilivyotabiriwa.
“Ongezeko la mvua hizo linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Desemba 2026, huku mvua za nje ya msimu zikitarajiwa kuendelea Januari 2027.”
Katika sekta ya kilimo, TMA imeonya kuwa unyevunyevu mwingi kwenye udongo, maji kutuama na mafuriko vinaweza kuathiri ukuaji wa mazao na kuharibu miundombinu ya kilimo.
“Hali hiyo inaweza kuongeza magonjwa ya mazao yanayosababishwa na fangasi, bakteria na virusi, na kuathiri uzalishaji wa viazi mviringo, alizeti, maharagwe, ufuta, matunda na mboga mboga,” amesema.
Amesema mvua za muda mrefu zinaweza pia kuathiri uvunaji, ukaushaji, usafirishaji na uhifadhi wa mazao, na hivyo kuongeza upotevu wa chakula baada ya kuvuna.
TMA imewashauri wakulima kuandaa mashamba na kupanda kwa wakati, kutumia mbegu zinazofaa kwa mazingira yao na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani.
“Pia wanashauriwa kuweka mifereji ya maji, kutumia matuta na mbinu za kilimo cha kontua ili kupunguza kutuama kwa maji, mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba,” amesema.
Kwa wafugaji, amesema mvua zinatarajiwa kuongeza upatikanaji wa malisho na maji, lakini unyevunyevu mwingi unaweza kuongeza hatari ya magonjwa ya mifugo, yakiwemo homa ya bonde la ufa na kuoza kwa kwato.
Mafuriko kuhatarisha miundombinu
Dk Chang’a pia amesema mvua nyingi zinaweza kuongeza kina cha maji katika mito na mabwawa, huku uchafuzi wa maji ukiongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko.
“Katika sekta ya usafiri, athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuharibika kwa barabara, kuporomoka kwa kingo, kuharibika kwa madaraja na njia za reli, pamoja na kuchelewa kwa huduma za usafiri wa anga na majini.
“Mvua kubwa, radi na upepo mkali vinaweza kupunguza uono kwa marubani na kuathiri ratiba za safari za ndege,” amesema.
Kwa upande wa ujenzi, amesema mvua zinaweza kuchelewesha miradi, kuongeza gharama, kuharibu vifaa na kuhatarisha usalama wa wafanyakazi na watumiaji wa miundombinu.
TMA imeshauri wakandarasi kuzingatia utabiri katika kupanga kazi, kuhamisha mitambo kutoka maeneo ya mabonde na chemchemi na kuhifadhi vifaa vinavyoweza kuharibika vikilowa, kama saruji, katika sehemu salama.
Katika maeneo ya uchimbaji madini, hasa migodi midogo, mamlaka hiyo imeonya kuwa mvua nyingi zinaweza kuongeza hatari ya maporomoko ya ardhi na kuporomoka kwa mashimo yasiyo imara.
Wananchi watakiwa kujiandaa
Kutokana na hali hiyo, TMA imezitaka mamlaka za serikali za mitaa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji, kuelimisha wananchi na kuimarisha kamati za maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata, vijiji na mitaa.
Katika sekta ya afya, imeshauri kuimarisha udhibiti wa mazalia ya mbu, kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kuandaa mipango mbadala ya kuendelea kutoa huduma pale miundombinu ya usafiri inapoharibika.
Mamlaka hiyo pia imesema mvua zinaweza kuathiri wanyamapori, shughuli za utalii na kusababisha wanyama kuingia katika makazi ya watu, hali inayoweza kuongeza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
TMA imewataka wananchi na wadau kutumia taarifa rasmi za hali ya hewa katika kupanga shughuli zao na kufuatilia tahadhari zinazotolewa kadiri hali inavyobadilika.
You may also like

Moto wateketeza maduka 20 stendi mpya ya Buza Dar

Wabeba mizigo hatarini kupata matatizo ya mgongo, nyonga


Leave a Reply