

Wabeba mizigo hatarini kupata matatizo ya mgongo, nyonga
Mbeya. Vijana wanaojishughulisha na ubebaji wa mizigo mizito kwa kutumia mgongo, mabega na kichwa maarufu ‘makuli’ wako hatarini kupata matatizo ya mifupa na viungo, ikiwamo pingili za mgongo.
Wakati wataalamu wa afya wakisema hivyo, makuli wenyewe wanasema baadhi yao hawana elimu kuhusu hatari tarajiwa ya kazi zao na hata wanapohisi maumivu ya mgongo wengi hukimbilia kwa waganga wa jadi wakidhani wamerogwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Oktoba 25, 2026, katika banda la Maonyesho ya Biashara na Uwekezaji Kusini (KITF), Ofisa Muuguzi na Meneja wa Wagonjwa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Judith Ndege, amesema kubeba mizigo mizito mara kwa mara kunaweza kuathiri mifupa na viungo.
“Ubebaji wa mizigo mizito huweka athari kwenye mifupa na viungo. Kadiri mwili unavyoendelea kukabiliwa na hali hiyo, mtu anaweza kupata matatizo ya pingili za mgongo na viungo vingine,” amesema.
Ndege, amesema ingawa matatizo ya mifupa na viungo yanaweza kuonekana zaidi kwa watu wenye umri mkubwa, vijana wanaofanya kazi zinazohusisha mizigo mizito nao wanapaswa kuchukua tahadhari.
Amesema elimu kuhusu njia salama za kubeba na kusafirisha mizigo ni muhimu ili kuwasaidia vijana kujikinga, badala ya kusubiri hadi waanze kupata maumivu au kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Akizungumzia huduma za taasisi hiyo, Ndege amesema MOI inatoa matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya pingili za mgongo, nyonga na magoti, ikiwamo kubadilisha viungo vilivyosagika na kuweka viungo bandia.
Amesema huduma hizo zinawasaidia wagonjwa kurejea katika shughuli zao za kila siku, kulingana na aina ya tatizo walilonalo na matokeo ya matibabu wanayopata.
“MOI tumeongeza ubobezi katika utoaji wa huduma za mifupa na viungo. Kwa wagonjwa wanaostahili, tunatoa huduma za kubadilisha viungo vilivyosagika na kuweka bandia ili waweze kuendelea na maisha yao,” amesema.
Ameongeza baadhi ya wagonjwa wanaweza kutibiwa bila kufanyiwa upasuaji mkubwa, kutegemea aina na kiwango cha tatizo baada ya kufanyiwa uchunguzi na wataalamu.
Mtaalamu wa Viungo Bandia na Vifaa Tiba Saidizi MOI, Charles Mahua, akionyesha mfumo wa baadhi ya viungo bandia ambavyo husaidia watu waliopata ulemavu kutokana na ajali za barabarani, kisukari au kuzaliwa nao. Picha na Hawa Mathias.
Wazazi wahimizwa kuwahi matibabu
Ndege, amesema MOI pia inatoa huduma kwa watoto wenye changamoto zinazohusisha ukuaji wa mifupa na viungo, ikiwamo vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Amesema baadhi ya watoto hao hukosa fursa za matibabu kutokana na imani potofu zinazowafanya wazazi kuwaficha majumbani badala ya kuwapeleka hospitalini kwa uchunguzi.
“Kuna dhana katika jamii kwamba mtoto anapozaliwa na changamoto hizi, baadhi huzihusisha na imani za kishirikina. Matokeo yake, watoto hufichwa na kunyimwa fursa ya kupata matibabu,” amesema.
Amesisitiza wazazi kuwapeleka watoto hospitali mapema ili wataalamu wafanye uchunguzi na kutoa matibabu yanayofaa, akibainisha kuwa matokeo hutegemea aina ya tatizo na hali ya mgonjwa.
Kuhusu kinga, amewahimiza wanawake wanaopanga kupata ujauzito na wajawazito kuzingatia lishe bora na ushauri wa wataalamu, ikiwamo matumizi ya virutubisho vinavyopendekezwa wakati wa ujauzito.
Ofisa Muuguzi na Meneja wa Kitengo cha Huduma za Wagonjwa wa Nje MOI, Judith Ndege, akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Oktoba 25, 2026 kwenye banda la Maonyesho ya Biashara, Uwekezaji Kusini kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Gombe Uyole. Picha na Hawa Mathias.
Ajali zaongeza mahitaji ya viungo bandia
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Viungo Bandia na Vifaa Tiba Saidizi wa MOI, Charles Mahua, amesema taasisi hiyo hupokea wagonjwa wanaohitaji vifaa hivyo, wengi wao wakiwa wamepata ajali.
Amesema vifaa hivyo huwasaidia watu waliopoteza viungo kutokana na ajali au sababu nyingine za kiafya kurejea katika shughuli zao, huku wengine wakiwa na changamoto walizozaliwa nazo.
“Vifaatiba saidizi ni mbadala wa viungo vilivyopotea kutokana na ajali au sababu nyingine za kiafya. Mtu anapopatiwa kifaa kinachomfaa, anaweza kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kila siku,” amesema.
Mahua, amesema kwa mujibu wa takwimu za huduma walizonazo, MOI hupokea takribani wagonjwa 61 kwa mwezi wanaohitaji huduma zinazohusiana na vifaa hivyo, huku wanaume wengi wanaohitaji miguu bandia wakihusishwa na ajali.
Amesema wanawake nao huhitaji huduma hizo kutokana na sababu mbalimbali za kiafya, ikiwamo saratani na madhara ya magonjwa mengine.
Ameongeza kuwa kupitia kambi za matibabu zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Serikali na wadau, wagonjwa wengi wamepata huduma. Amesema zaidi ya watu 600 walinufaika na kambi hizo mwaka uliopita.
Mahua, amewataka watu wanaohitaji viungo bandia na vifaa saidizi kufika katika vituo vya huduma badala ya kujitenga, akieleza kuwa baadhi wanaweza kusaidiwa na Serikali na wadau.
Amesema ushiriki wa MOI katika maonyesho ya KITF unalenga kuongeza uelewa kuhusu huduma za mifupa, ubongo, mishipa ya fahamu na vifaa tiba saidizi, pamoja na kuwafikia wanaohitaji matibabu.
Kwa upande wake, Athon Saimoni, kijana anayefanya kazi ya kubeba mizigo katika Kituo cha Mabasi cha Kabwe, amesema uelewa mdogo kuhusu matatizo ya pingili za mgongo ni changamoto miongoni mwa wafanyakazi hao.
Amesema baadhi ya makuli wanapopata maumivu ya mgongo hukimbilia kwa waganga wa tiba asili, wakihusisha hali hiyo na kulogwa badala ya kutafuta uchunguzi hospitalini.
“Hizi kazi za ukuli, kijana akipata changamoto ya pingili za mgongo, baadhi hukimbilia kuagua kwa imani kuwa wamerogwa. Wanahitaji elimu zaidi kuhusu athari za kubeba mizigo mizito,” amesema.
Ameshauri Serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza elimu kwa vijana wanaobeba mizigo, ili wajue namna ya kujikinga, kutumia mikokoteni na kutafuta matibabu mapema wanapoanza kupata dalili za matatizo ya mgongo.
You may also like

Wadau washauri Oktoba 29 iwe siku ya kusaka amani

Moto wateketeza maduka 20 stendi mpya ya Buza Dar


Leave a Reply