

Moto wateketeza maduka 20 stendi mpya ya Buza Dar
Dar es Salaam. Maduka 20 kati ya 64 yameteketea kwa moto katika Stendi Mpya ya Buza kwa Mama Kibonge, Wilaya ya Temeke, asubuhi ya Oktoba 25, 2026, siku moja baada ya moto mwingine kuteketeza vibanda 26 katika Soko la Veterinary wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Oktoba 25, 2026, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Temeke, Boniphace Adhiri, amesema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokana na kuunganisha waya wa mashine ya kusaga juisi ya miwa katika duka la vipodozi, na kusababisha moto kusambaa kwenye maduka mengine.
“Tulipata taarifa saa 4 asubuhi kuna moto katika soko la Buza. Tuliwahi eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti usienee kwenye maduka mengi, huku tukiokoa maduka 44,” amesema Adhiri.
Amesema kutokana na tukio hilo, Oktoba 26, 2026, wanatarajia kufika katika eneo hilo kuzungumza na wafanyabiashara na kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na vizimamoto, vinavyoweza kusaidia kudhibiti moto katika hatua za awali kabla haujasambaa.
Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kikizima moto kwenye maduka yaliyoteketea katika eneo la Stendi Mpya ya Buza kwa Mama Kibonge,Temeke, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa eneo hilo, Khatibu Kitu, amesema moto huo umetokea wakati wafanyabiashara wengi wakiwa wamefunga maduka yao kwa kuwa hawana utaratibu wa kufungua biashara siku za Jumapili.
Amesema taarifa za awali alizopata zinaeleza kuwa moto ulianza baada ya muuza juisi ya miwa kuunganisha waya wa umeme kwenye duka la vipodozi.
“Kwa taarifa nilizopata, muuza juisi ya miwa aliunganisha waya kwenye duka la vipodozi, ndipo moto ulipoanza na kusambaa katika maduka mengine,” amesema Kitu.
Amesema tukio hilo limewasababishia wafanyabiashara hasara na kuonyesha umuhimu wa kuimarisha usalama wa mifumo ya umeme katika maeneo ya biashara.
Kuhusu mwenye duka lililoungua, Kitu amesema wamejaribu kumtafuta kwa simu bila mafanikio tangu tukio hilo litokee, hata muuza juisi ya miwa hajapatikana.
Mashine inayodaiwa kuwa chanzo cha moto ulioteketeza maduka 20 ikiwa mbele ya duka iliyounganishiwa waya, eneo la Stendi mpya ya Buza kwa Mama Kibonge, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam
“Mmiliki wa duka hadi sasa hapatikani. Tumemtafuta muda mrefu kwa sababu Jumapili hafiki ofisini, kwa hiyo tumeongea na muuza juisi, naye kasema hampati,” amesema.
Kitu amesema wafanyabiashara wanahitaji kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na viongozi wa maeneo yao ili kupata elimu na kuchukua tahadhari za kuzuia majanga kama hayo.
Moto huo umetokea siku moja baada ya tukio jingine katika Soko la Veterinary, Temeke, ambako vibanda 26 kati ya 230 viliteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana Oktoba 24, 2026.
Baadhi ya bidhaa ambazo zimeokolewa kwenye maduka yaliyoteketea kwa moto katika stendi mpya ya Buza kwa Mama Kibonge, Temeke, jijini Dar es Salaam.
Mfanyabiashara Sabrina Hussein amesema alipigiwa simu akiwa nyumbani na kuarifiwa kuwa maduka yalikuwa yakiungua, hivyo akawahi kufika eneo la tukio na kufanikiwa kuokoa bidhaa zake.
“Nimefanikiwa kutoa vitu vyangu maana sikuwepo hapa. Nikapigiwa simu nikiwa nyumbani, nikawahi kuja kutoa vitu na duka langu lipo jirani na moja ya duka lililoungua,” amesema.
You may also like

DC avunja sherehe ya mahari ya mwanafunzi Bariadi

Mtanzania atwaa tuzo ya vijana 100 wa Jumuiya ya Madola


Leave a Reply