

Waongoza watalii walalamikia kipato duni, ukosefu wa mafao
Arusha. Katibu Mkuu wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TTGA), Robert Marks amesema changamoto kubwa inayowakabili waongoza watalii ni masilahi duni, hali inayowafanya baadhi yao kumaliza miaka mingi ya utumishi bila kuwa na akiba, mafao au malipo ya uzeeni.
Amesema pamoja na kuitwa mabalozi wa utalii, kundi hilo halinufaiki ipasavyo na mapato yanayotokana na shughuli wanazofanya.
“Tunaitwa mabalozi wa utalii na kupewa majina makubwa, lakini inapofika suala la kipato, fedha nyingi zinabaki nje ya nchi au kwenye kampuni kubwa. Tunafanya kazi miaka 10, 20 hadi 30, lakini mwisho wa siku tunastaafu bila kuwa na kiinua mgongo wala mapato yoyote,” amesema.
Marks amesema hayo leo Jumanne 24, 2026 katika mkutano wa Kimataifa wa Waongoza Watalii Barani Afrika (Pan Africa Tour Guides Conference 2026) unaofanyika jijini hapa.
Amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa muda mrefu bila kuwa na uhakika wa mafao baada ya kustaafu, hivyo wanahitaji mifumo itakayohakikisha sehemu ya mapato ya utalii inawanufaisha moja kwa moja.
Marks amesema wana matumaini mamlaka husika itasaidia kuibua na kuwasilisha changamoto hizo ili kuwepo kwa mfumo utakaowezesha mapato yanayotokana na utalii kubaki ndani ya Afrika na kuwanufaisha wadau wa ndani.
“Tunaiomba Pan Africa Tourism Board itusaidie kuhakikisha mapato yanayopatikana kutokana na utalii yanabaki hapa Afrika na kuwanufaisha Waafrika badala ya kuzifanya kampuni za kigeni kuwa tajiri,” amesema.
Wakati changamoto hizo za masilahi zikiendelea kuibuliwa, nchi za Afrika pia zimetakiwa kuoanisha viwango vya kitaaluma na mifumo ya utoaji na utambuzi wa leseni za waongoza watalii ili kuwawezesha kufanya kazi katika mataifa mbalimbali ya bara hilo.
Hatua hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya kiutendaji vinavyozuia waongoza watalii kufanya kazi katika nchi tofauti, kupanua fursa za ajira na kuimarisha ushindani wa Afrika katika soko la utalii duniani.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dk Eblate Mjingo, aliyemwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, katika Mkutano wa Kimataifa wa Waongoza Watalii Barani Afrika.
Dk Mjingo amesema moja ya changamoto zinazokwamisha ukuaji wa utalii barani Afrika ni mataifa kujitangaza na kujiendesha kama maeneo tofauti ya utalii badala ya kuunganisha vivutio vyao na kujenga soko moja la kikanda.
Amesema hali hiyo inatofautiana na maeneo mengine duniani ambako watalii wanaweza kuvuka mipaka ya nchi kadhaa na kutembelea vivutio mbalimbali katika safari moja.
“Tunapaswa kuifanya Afrika kuwa eneo moja lililounganishwa na lenye ushindani katika sekta ya utalii. Mgeni anayesafiri kwenda Tanzania anapaswa kuwa na fursa ya kutembelea na kugundua vivutio pamoja na maeneo mengine ya utalii katika nchi mbalimbali za Afrika,” amesema.
Dk Mjingo amesema kufanikisha azma hiyo kunahitaji mifumo ya pamoja ya utalii na viwango vinavyolingana vya kitaaluma, hususan kwa waongoza watalii ambao ni sehemu muhimu ya huduma zinazotolewa kwa wageni.
Ametoa mfano kuwa mwongoza watalii mwenye sifa na leseni zinazotambulika Tanzania anapaswa kuwa na uwezo wa kutambulika pia katika nchi nyingine, ikiwemo Ghana na Kenya, ili kurahisisha utoaji wa huduma katika mataifa hayo.
Dk Mjingo amesema kuoanisha viwango hivyo kutasaidia kupanua soko la ajira kwa waongoza watalii, kuongeza fursa za kutangaza vivutio vya Afrika kwa pamoja, kuboresha muunganiko wa usafiri na kuhamasisha Waafrika kusafiri ndani ya bara lao.
Aidha, amezitaka taasisi za kikanda na Umoja wa Afrika (AU) kushirikiana na Serikali za nchi wanachama katika kuoanisha viwango vya taaluma, kutambua sifa zinazotolewa katika mataifa mbalimbali na kuweka mifumo ya kubadilishana maarifa.
Dk Mjingo amesema ni muhimu pia kuimarisha mafunzo na kujenga uwezo wa waongoza watalii ili kukabiliana na mabadiliko ya sekta hiyo, yakiwemo matumizi ya teknolojia na mahitaji mapya ya wageni.
Katika hatua nyingine, Dk Mjingo amesema Afrika inapaswa kuimarisha mikakati ya kuitangaza kimataifa kwa kutumia simulizi zinazotokana na historia, utamaduni, mafanikio ya uhifadhi na utajiri wa vivutio vyake.
“Ni wakati sasa wa sisi wenyewe kusimulia hadithi za Afrika badala ya kuacha watu wengine watusimulie hadithi zisizo zetu. Tunapaswa kujiandaa na kuwa na umiliki mkubwa zaidi wa simulizi zinazohusu bara letu,” amesema.
Amesema waongoza watalii wana nafasi muhimu katika kutekeleza jukumu hilo kwa kuwa wanakutana moja kwa moja na wageni na kupata fursa ya kueleza historia, utamaduni na utambulisho wa mataifa yao.
Awali, Rais wa Pan Africa Tourism Board, Mariam Lesian, amesema waongoza watalii ni mabalozi na walinzi wa urithi wa utalii barani Afrika kutokana na mchango wao katika kueleza historia, utamaduni na thamani ya vivutio kwa wageni.
Amesema bila waongoza watalii, wageni wanaweza kukosa uelewa wa kina kuhusu maeneo wanayotembelea, kwa kuwa kundi hilo lina nafasi ya kuwaeleza historia na utambulisho wa vivutio hivyo.
Kwa ujumla, hoja zilizojadiliwa katika mkutano huo zimeweka pamoja changamoto za maslahi ya waongoza watalii na umuhimu wa kuunganisha mifumo ya kitaaluma barani Afrika, ili kuhakikisha ukuaji wa utalii unapanua fursa za ajira na manufaa ya kiuchumi kwa wadau wa ndani.
You may also like


IMF yatoa neno mageuzi ya kiuchumi Tanzania


Leave a Reply