

Madalali Njombe kikaangoni | Mwananchi
Njombe. Madalali mkoani Njombe watakaobainika kufanya shughuli zao kinyume na taratibu na miongozo iliyowekwa watachukuliwa hatua, huku kila mmoja akitakiwa kuwa na kitambulisho na namba maalumu kwa ajili ya utambulisho.
Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Masoko (Madalali) Mkoa wa Njombe, Naman Hongoli, aliyesema hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa shughuli za udalali, kuongeza uwajibikaji na kudhibiti vitendo vya udanganyifu.
Hongoli ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Novemba 24, 2026, baada ya kupokea leseni na vyeti vya usajili wa ofisi ya chama hicho kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Njombe.
Amesema usajili huo ni hatua muhimu katika kuwaweka madalali kwenye mfumo rasmi wa utendaji, utakaowezesha kila mmoja kuwajibika kwa matendo yake.
“Kuanzia sasa kila dalali atakuwa na kitambulisho na namba maalumu ya utambulisho ili iwe rahisi kumtambua. Yeyote atakayebainika kufanya kazi kinyume na taratibu tulizoweka tutamchukulia hatua,” amesema Hongoli.
Ameongeza kuwa utaratibu huo utasaidia kuondoa watu wanaotumia jina la udalali kujihusisha na vitendo visivyo vya uaminifu, huku ukijenga imani ya wananchi kwa madalali wanaotoa huduma zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Njombe, ASP Haruna Mlumba Mtove, amesema madalali wana nafasi muhimu katika jamii, hivyo wanapaswa kutumia umoja wao kuimarisha amani na usalama.
Amesema ushirikiano wao na vyombo vya ulinzi na usalama utasaidia kuzuia uhalifu na kutoa taarifa muhimu zinazoweza kulinda jamii.
“Madalali ni sehemu muhimu ya jamii. Ni vyema mkadumisha umoja, mshirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama na kuhakikisha shughuli zenu zinafanyika kwa kuzingatia sheria na maadili,” amesema Mtove.
Naye mmoja wa madalali, Gifta Mhagama (Mlalo), amesema kuanzishwa kwa chama hicho kutasaidia kuimarisha utendaji wao na kudhibiti vitendo vinavyoweza kuchafua taswira ya kada hiyo.
“Umoja huu utatoa fursa ya kutambua madalali wanaofanya kazi kwa uaminifu na kuwabaini wale wanaokiuka makubaliano na taratibu za kazi,” amesema Mhagama.
You may also like


IMF yatoa neno mageuzi ya kiuchumi Tanzania


Leave a Reply