

IMF yatoa neno mageuzi ya kiuchumi Tanzania
Dar es Salaam. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeitaka Tanzania kuharakisha mageuzi ya sekta binafsi, kuongeza uwekezaji katika elimu na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kudumisha ukuaji wa uchumi na kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia ajira zenye mishahara bora.
IMF inakadiria uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 5.9 katika mwaka wa fedha 2026/27, huku ukuaji ukitarajiwa kufikia wastani wa asilimia sita katika kipindi cha muda wa kati, ukichochewa na sekta za madini, kilimo na utalii.
Hata hivyo, katika tathmini yake chini ya kifungu cha nne (Article IV), shirika hilo limeonya kuwa uzalishaji mdogo, uwekezaji usiotosheleza katika rasilimali watu na vikwazo kwa uwekezaji binafsi vinaweza kudhoofisha ukuaji jumuishi wa uchumi.
Ujumbe huo wa IMF, unaoongozwa na Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa Ujumbe nchini, Nicolas Blancher, umefika nchini tangu Novemba 11, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumanne, Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Blancher amesema vipaumbele ni kuongeza fedha kwa ajili ya elimu, afya na ulinzi wa jamii, pamoja na kuimarisha sekta binafsi ili iwe chanzo kikuu cha ajira endelevu.
“Katika bajeti ya 2026/27, Serikali ya Tanzania inalenga nakisi ya asilimia 2.8 ya Pato la Taifa (GDP), huku matumizi ya huduma za kijamii yakiwa takribani asilimia saba ya GDP,” amesema Blancher.
Amesema shirika hilo linaitaka Serikali kuongeza mapato kwa kupanua wigo wa kodi, kupunguza misamaha na kuimarisha ulipaji wa kodi na udhibiti wa forodha, badala ya kutegemea zaidi mikopo.
Pia, limependekeza kuboresha usimamizi wa uwekezaji wa umma na uwazi wa taarifa za madeni na wajibu wa kifedha wa mashirika ya umma.
Kuhusu elimu, Blancher amesema IMF imesema mgao wa takribani asilimia 3.1 ya GDP hautoshi kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la watu.
Blancher ametaja upungufu wa walimu, vifaa vya kujifunzia na shule katika maeneo ya mbali, akisisitiza umuhimu wa kuajiri walimu, kuboresha maslahi yao na miundombinu.
Hata hivyo, IMF imeeleza wasiwasi kuhusu uendelevu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kutokana na rasilimali chache na utegemezi wa ufadhili wa nje.
“Katika ajira, takribani asilimia 90 ya ajira nchini zinatokana na shughuli zenye uzalishaji mdogo,” amesema.
Blancher amesema biashara ndogo na za kati zina nafasi kubwa katika kutengeneza ajira zenye mishahara bora kuliko kuongeza ajira serikalini.
Ametaja tozo nyingi, mwingiliano wa majukumu ya taasisi za udhibiti na urasimu kuwa vikwazo kwa wafanyabiashara.
IMF imependekeza kutekeleza mpango kabambe wa mageuzi ya udhibiti wa biashara, kuboresha upatikanaji wa mikopo na kuweka utabirika wa sera za kodi.
Pia, imehimiza uwazi kuhusu sera za kodi, ikibainisha kuwa kutokuchapishwa kwa ripoti ya Tume ya Rais ya Kodi kunazua maswali kwa wawekezaji kuhusu mwelekeo wa mapendekezo yake.
Katika sera ya fedha, IMF imependekeza kudhibiti ukuaji wa fedha katika uchumi. Blancher amesema mikopo kwa sekta binafsi inakua kwa zaidi ya asilimia 30, huku ukwasi ukiwa mkubwa. Ameonya kuwa misukosuko ya nje inaweza kuongeza mfumuko wa bei, licha ya sasa kubaki ndani ya lengo la asilimia tatu hadi tano.
IMF pia imehimiza kubadilika zaidi kwa thamani ya shilingi na kujenga upya akiba ya fedha za kigeni. Nakisi ya urari wa malipo ya nje inatarajiwa kufikia asilimia 2.9 ya GDP mwaka 2026/27.
Kuhusu ununuzi wa mafuta, Blancher amesema mfumo wa pamoja ulisaidia kuhakikisha upatikanaji wa nishati, lakini wadau wameibua changamoto za uwazi katika upangaji wa bei. Mazungumzo kati ya Serikali na sekta binafsi yanaweza kusababisha kulegezwa kwa mfumo huo katika miezi ijayo.
IMF imesema deni la umma bado lina kiwango cha wastani cha hatari, lakini imesisitiza nidhamu ya bajeti na matumizi bora ya fedha za umma.
Amesema: “Tanzania ina uwezo mkubwa wa kiuchumi, lakini kuufikia kunahitaji kutekeleza mageuzi, kuimarisha uwajibikaji na kuweka mazingira yatakayovutia uwekezaji na kupanua fursa za biashara.”
You may also like


Madalali Njombe kikaangoni | Mwananchi


Leave a Reply