

Sorecu yataja sababu za kupaa kwa uzalishaji kahawa, yageukia mbaazi
Mbeya. Uzalishaji wa kahawa katika Kanda ya Mbeya umeongezeka hadi tani 27,000 kutoka 24,000, huku bei ikifikia Sh15,250 kwa kilo, hali iliyoongeza manufaa ya zao hilo kwa wakulima na kuchochea Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Songwe (Sorecu) kuimarisha mikakati ya mazao mengine.
Chama hicho kimetaja uhakika wa soko, bei nzuri, upatikanaji wa mbolea ya ruzuku na elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia ongezeko la uzalishaji wa kahawa.
Pia, kimeanza mchakato wa kuingiza zao la mbaazi katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuwawezesha wakulima kuzalisha na kuuza kwa tija zaidi, kama ilivyo kwa zao la ufuta.
Kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Kahawa, uzalishaji katika Kanda ya Mbeya, inayojumuisha mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya, umeongezeka kutoka tani 24,000 hadi tani 27,000 katika kipindi cha miaka miwili.
Akizungumza na Mwananchi Novemba 26, 2026, Mwenyekiti wa Sorecu, Daniel Shija, amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa soko na bei, ruzuku ya mbolea na elimu inayotolewa kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu.
Amesema kutokana na matokeo hayo, chama kinaendelea na mchakato wa kuongeza mbaazi katika mfumo wa stakabadhi ghalani unaosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), kwa lengo la kuwawezesha wakulima kunufaika na mazao yao.
“Tumeboresha na kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo hadi sasa, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wangu, hakuna mkulima anayedai fedha zake za mauzo ya mazao,” amesema.
Shija amesema mafanikio hayo pia yametokana na mabadiliko ya kiutendaji, ikiwemo kuajiri wataalamu, kuboresha mazingira ya kazi, ofisi na usafiri, pamoja na kuimarisha ushirikiano na Ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Songwe.
Amesema ili kudumisha mafanikio hayo, Sorecu imejipanga kuviimarisha vyama vya msingi ili viweze kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea ushuru wa mazao kila msimu.
Ameongeza kuwa vyama vya msingi vimenunua mabomba na kuchimba visima kwa ajili ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kuwawezesha wakulima kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji.
Kwa upande wake, Meneja wa Sorecu, Daud Andrew, amesema chama hicho kimeanza kutumia mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wakulima, ikiwemo matumizi ya mizani ya kisasa inayohifadhi taarifa za mazao.
Amesema wakati mchakato wa kuingiza mbaazi katika mfumo wa stakabadhi ghalani ukiendelea, chama kimenunua tani 1.5 za mbegu za zao hilo kwa ajili ya kuwagawia wakulima katika msimu ujao.
“Awali tulitumia mizani ya zamani ya kuning’iniza, lakini kwa sasa tumenunua mizani ya kisasa iliyounganishwa na mifumo, ambapo mkulima anapata taarifa zake za makusanyo ya mazao,” amesema.
Ameongeza kuwa chama kimenunua mizani zaidi ya 120 yenye thamani ya Sh300 milioni, hatua aliyosema inalenga kuongeza usahihi wa taarifa na kuhakikisha wakulima wanapata malipo yanayostahili.
Kuhusu ufuta, Andrew amesema uzalishaji wake bado uko katika kiwango kizuri, huku chama kikikusanya tani 13,000 msimu uliopita na tani 10,000 mwaka huu.
Mkulima wa kahawa katika Chama cha Msingi cha Ushirika (Amcos) cha Igale, mkoani Songwe, Geofrey Shura, amesema msimu huu umekuwa wa mafanikio kutokana na ongezeko la uzalishaji, soko na bei nzuri.
Amesema wakulima wengi wameanza kufikiria kuongeza mashamba ya kahawa kutokana na manufaa wanayopata, huku akishukuru Serikali kwa ruzuku ya mbolea na Sorecu kwa kusimamia maslahi yao.
“Jinsi soko linavyopamba moto, wapo baadhi ya wakulima wanaofikiria kupanda kahawa zaidi ikilinganishwa na mahindi na mazao mengine. Kila mkulima amechimba mashimo kwenye shamba kwa ajili ya kupanda kahawa,” amesema.
“Uchumi kwa sasa umeanza kupanda kwa kuwa waliokuwa hawana nyumba wanajenga, wananunua usafiri kama pikipiki. Tunashukuru pia ujenzi wa barabara ya Igale ambayo itaturahisishia usafirishaji wa mazao,” amesema.
You may also like

Kaya tano kati ya 54 zilizoathiriwa mvua Ushetu zapatiwa msaada



Leave a Reply