

Green Catalyst kufungua dirisha jipya la ufadhili wa biashara za misitu
Iringa. Mradi wa Green Catalyst unaofadhiliwa na Serikali ya Finland na kutekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), umezindua dirisha la tatu la maombi ya ufadhili kwa biashara zinazojihusisha na mnyororo wa thamani wa misitu, hatua inayolenga kuongeza uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi wa kijani nchini.
Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 25, 2026, mjini Mafinga, mkoani Iringa, sambamba na kutambulishwa kwa biashara zilizochaguliwa kunufaika na ufadhili katika awamu ya pili ya mradi huo unaotekelezwa kupitia Programu ya Ubunifu ya FUNGUO.
Taarifa ya mradi inaeleza kuwa katika awamu mbili zilizopita, jumla ya Sh1.45 bilioni zimetengwa kufadhili biashara 19 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi.
Meneja wa Programu ya FUNGUO, UNDP Tanzania, Joseph Manirakiza akizungumza na wageni waalikwa mjini Mafinga mkoani Iringa wakati wa uzinduzi wa dirisha la tatu la maombi ya Mradi wa Green Catalyst unaofadhiliwa na serikali ya Finland na kutekelezwa na UNDP Tanzania chini ya Programu ya Ubunifu ya FUNGUO.
Ukuaji wa mwitikio kutoka kwa waombaji pia umeonekana, ambapo idadi ya maombi imeongezeka kutoka 187 katika awamu ya kwanza hadi 1,178 katika awamu ya pili, ishara ya kuongezeka kwa mahitaji ya mitaji na fursa za uwekezaji katika sekta ya misitu.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Atupele Mwakibete, amesema rasilimali za misitu zina nafasi kubwa katika kukuza viwanda, kuongeza uwekezaji na kutengeneza ajira, hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Amesema kuongeza thamani ya mazao ya misitu kupitia biashara za ndani kutasaidia kuhakikisha manufaa ya kiuchumi yanayotokana na rasilimali hizo yanawanufaisha zaidi wananchi na kuchochea maendeleo endelevu.
“Rasilimali za misitu tulizonazo zina fursa kubwa za kukuza viwanda, uwekezaji na ajira. Kwa kuimarisha biashara za ndani na kuongeza thamani ya mazao ya misitu, tunaweza kuhakikisha kuwa sehemu kubwa zaidi ya manufaa ya kiuchumi inabaki katika jamii zetu,” amesema Mwakibete.
Kupitia mradi huo, uwekezaji unaelekezwa katika maeneo mbalimbali ya mnyororo wa thamani wa misitu, yakiwamo uchakataji wa mbao, matumizi ya mabaki ya mbao, ufugaji nyuki na uzalishaji endelevu wa mazao ya misitu.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani, kuboresha ubora wa bidhaa, kupunguza upotevu wa rasilimali na kupanua fursa za masoko kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na sekta hiyo.
Aidha, mradi unalenga kupanua fursa za ajira na kuongeza kipato kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, makundi yanayotajwa kuwa miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji unaofanyika katika maeneo hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Kimaendeleo katika Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, Sanna-Liisa Taivalmaa, amesema ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unalenga kuimarisha sekta ya misitu kwa kuoanisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema Serikali ya Finland inaunga mkono uwekezaji unaowawezesha wajasiriamali wa vijijini kukuza biashara zao, kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kuboresha maisha ya wananchi bila kuhatarisha uendelevu wa rasilimali zilizopo.
“Kupitia Green Catalyst, tunaunga mkono uwekezaji unaoleta uwiano kati ya utunzaji wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi, hasa kwa wajasiriamali wa vijijini wanaojishughulisha na shughuli za mnyororo wa thamani wa misitu,” amesema Taivalmaa.
Mbali na ufadhili wa kifedha, Green Catalyst pia hutoa msaada wa kitaalamu kwa biashara zinazoshiriki katika mradi huo, ikiwamo kuzijengea uwezo wa kuvutia uwekezaji na kuziunganisha na masoko.
Msaada huo unalenga kukabiliana na changamoto zinazokwamisha ukuaji na ushindani wa biashara za ndani, hasa zile zinazohitaji mitaji, teknolojia na ujuzi wa kuendeleza shughuli zao.
Meneja wa Programu ya FUNGUO, Joseph Manirakiza, amesema mafanikio ya uwekezaji huo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya biashara zinazopata fedha pekee, bali pia kwa mchango wake katika kutengeneza fursa za kiuchumi na kuimarisha uzalishaji wa ndani.
Amesema kuimarisha biashara hizo kutasaidia kuongeza ajira, kukuza minyororo ya thamani na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka sekta binafsi.
“Thamani halisi ya uwekezaji huu haipimwi kwa idadi ya biashara zinazopata ufadhili pekee, bali pia kwa fursa za kiuchumi zinazoweza kutengenezwa kupitia biashara hizo,” amesema Manirakiza.
Uzinduzi wa dirisha la tatu unatarajiwa kutoa nafasi kwa biashara nyingine zenye ubunifu katika mnyororo wa thamani wa misitu kuomba ufadhili na kunufaika na huduma za ukuzaji biashara katika mikoa minne inayolengwa na mradi.
Wajasiriamali wanaotaka kupata maelezo kuhusu masharti na utaratibu wa maombi wanaweza kutembelea tovuti ya www.funguo.org.
Green Catalyst ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Finland na kutekelezwa na UNDP Tanzania kupitia Programu ya Ubunifu ya FUNGUO.
Mradi huo unalenga kuongeza ajira kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa misitu, kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kukuza uchumi endelevu.
Pia, unachangia juhudi za mradi wa FORLAND (Misitu, Matumizi ya Ardhi na Minyororo ya Thamani) katika kuongeza ajira vijijini kupitia ubunifu, ukuzaji wa ujuzi, uendelezaji wa biashara na upatikanaji wa mitaji.
You may also like

Kaya tano kati ya 54 zilizoathiriwa mvua Ushetu zapatiwa msaada

Wadau waibana Serikali kuhusu kalenda ya ufadhili


Leave a Reply