

Ndejembi aagiza tathimini mahitaji ya wafamasia
Mwanza. Serikali imeagiza kufanyika kwa tathimini ya mahitaji halisi ya wafamasia nchini ili kubaini upungufu wa wataalamu hao na kupanga ajira za awamu kulingana na uwezo wa bajeti.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ambapo aliielekeza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kufanya tathimini hiyo katika ngazi zote za utoaji huduma za afya.
Pia, ameitaka Wizara ya Afya kukamilisha mchakato wa kuanzisha kurugenzi ya dawa na kuweka miundo ya kiutumishi inayofaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali za kanda na hospitali maalumu ili kuimarisha usimamizi wa huduma za dawa.
Ndejembi ametoa maagizo hayo leo, Novemba 25, 2026, wakati akifungua mkutano mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania pamoja na kongamano la kisayansi jijini Mwanza.
Amesema kuongeza vitanda katika vituo vya kutolea huduma za afya hakutoshi kuboresha huduma ikiwa idadi ya wataalamu haitalingana na mahitaji ya wananchi.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania na Kongamano la Kisayansi wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika mkoani Mwanza.
Ameitaka Wizara ya Afya kushirikiana na Ofisi ya Rais, Utumishi, kukamilisha maboresho ya ikama ili wataalamu wa famasia watambuliwe kulingana na utaalamu na majukumu yao katika mfumo wa utoaji huduma za afya.
Amesema tathimini hiyo inapaswa kubaini maeneo yenye upungufu wa wafamasia na wataalamu wa teknolojia ya dawa, namna kazi hizo zinavyofanyika sasa na hatua za ajira zinazoweza kutekelezwa kwa awamu.
Akizungumzia kuanzishwa kwa kurugenzi ya dawa, Ndejembi amesema ongezeko la wataalamu wa famasia nchini na mabadiliko ya taaluma hiyo yanahitaji Serikali kufanya mapitio ya miundo yake ya kiutumishi.
Amesema awali idadi ya wafamasia ilikuwa ndogo, lakini mageuzi katika mfumo wa elimu kuanzia mwaka 2010 na kuruhusu vyuo vingine kutoa mafunzo ya famasia yamesababisha ongezeko la wataalamu hao.
“Leo kama Serikali tuna Mfamasia Mkuu wa Serikali kwa sababu tumetambua taaluma hii ya dawa kuwa ni kada muhimu katika kufikia azma ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa mwananchi. Sasa sioni kwa nini muundo usibadilike na kuwa pia na kurugenzi maalumu ya dawa,” amesema.
Katika hatua nyingine, amewataka wafamasia kusimamia maadili ya taaluma yao na kupambana na wizi na ubadhirifu wa dawa za Serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Amesema ni wajibu wao kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote na kujenga imani ya wananchi kwa kusimamia misingi na miiko ya taaluma hiyo.
Aidha, ameitaka Wizara ya Afya kushirikiana na wadau wa sekta ya ardhi kuhakikisha Chama cha Wafamasia Tanzania kinapatiwa eneo la ekari 400 katika eneo la Hospitali ya Mloganzila kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa.
Awali, Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, amesema Serikali imetenga ekari 400 Mloganzila kwa ajili ya kongani ya viwanda vya dawa. Amesema viwanda sita viko katika hatua za ujenzi na baadhi vinatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2027.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Fadhil Hezekiah, ameiomba Serikali kuhakikisha mapitio ya ikama yanazingatia majukumu ya sasa ya wafamasia, yakiwemo kutoa huduma katika kliniki za magonjwa sugu, kusimamia ugavi na kufuatilia usalama wa dawa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Salum Hamduni, amesema bajeti ya kuboresha huduma za afya mkoani humo imeongezeka kutoka Sh51.2 bilioni mwaka 2024/25 hadi Sh74.5 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 45.2.
Amesema mkoa umepokea zaidi ya Sh65 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya, huku upatikanaji wa dawa ukifikia asilimia 93.3 na utoshelevu wa dawa ukiwa asilimia 85.5.
Ameongeza kuwa watumishi 1,718 wameajiriwa katika sekta ya afya mkoani Mwanza tangu mwaka 2021.
You may also like


Wadau waibana Serikali kuhusu kalenda ya ufadhili

Leave a Reply