

Jengo laporomoka Nairobi, watu wahofiwa kufukiwa
Nairobi, Kenya. Watu kadhaa wanahofiwa kufukiwa chini ya vifusi baada ya jengo kuporomoka katika eneo la Eastleigh, jijini Nairobi, Kenya, leo Oktoba 23, 2026.
Tukio hilo limetokea kando ya Barabara ya Yusuf Haji, karibu na duka la Day to Day, Mtaa wa 9, ambako vikosi vya uokoaji vimewasili kuanza shughuli za kutafuta manusura.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, limethibitisha kuwa timu zake za kukabiliana na dharura zipo eneo la tukio, zikishirikiana na mamlaka nyingine kuokoa watu wanaoweza kuwa wamenasa kwenye vifusi.
Kupitia taarifa yake, shirika hilo limewaomba wananchi kuepuka eneo hilo ili kuruhusu waokoaji kutekeleza majukumu yao kwa usalama, bila kuingiliwa na umati wa watu wanaofuatilia tukio hilo.
“Tunawaomba wananchi wakae mbali na eneo hilo ili kuruhusu timu za dharura kufanya kazi kwa usalama,” ilisema Kenya Red Cross katika taarifa yake.
Timu za kukabiliana na dharura za Serikali ya Kaunti ya Nairobi pia zimewasili eneo hilo, huku juhudi za kuondoa vifusi na kutafuta watu wanaoweza kuwa wamekwama zikiendelea.
Katika taarifa yake, Serikali ya kaunti imesema mitambo imepelekwa kusaidia kuondoa vifusi na kufungua njia kwa waokoaji kuwafikia watu wanaoweza kuwa wameathiriwa na kuporomoka kwa jengo hilo.
Aidha, Ofisa wa Misaada, amearifiwa kuhusu tukio hilo, huku juhudi za kutafuta rasilimali zaidi za kusaidia shughuli za uokoaji zikiendelea.
Hata hivyo, hadi taarifa hii inaandaliwa, idadi kamili ya watu waliokuwa ndani ya jengo hilo wakati linaporomoka na hali zao haikuwa imewekwa wazi.
Polisi watumia mabomu ya machozi
Kamanda wa Polisi wa Nairobi, Issa Mohamed, amesema polisi walitumia mabomu ya machozi kutawanya watu waliokuwa wamekusanyika kutazama tukio hilo, ili kutoa nafasi kwa waokoaji kufanya kazi.
Amesema hatua hiyo pia ililenga kuzuia uporaji wa maduka yaliyopo karibu na eneo la tukio, baada ya baadhi ya vijana kuripotiwa kujaribu kuchukua vyuma chakavu kutoka kwenye vifusi.
Akizungumza na The Daily Nation, Mohamed amesema vikosi vya dharura vinaendelea na shughuli za kutafuta manusura, huku polisi zaidi wakitumwa kusaidia kuratibu operesheni hiyo.
Ameongeza kuwa maafisa hao watasaidia kuimarisha usalama na kuhakikisha timu mbalimbali zinazoshiriki shughuli za uokoaji zinafanya kazi kwa uratibu.
Kwa sasa, juhudi zinaendelea eneo la tukio, huku wananchi wakitakiwa kuepuka kukaribia vifusi na kuacha njia wazi kwa magari na vikosi vya dharura.
You may also like

Mtanzania atwaa tuzo ya vijana 100 wa Jumuiya ya Madola

Tanzania mwenyeji mkutano waa maadili ya biashara Afrika

Leave a Reply