

Kifungo cha maisha jela chamng’ang’ania aliyemlawiti mtoto wa miaka mitatu
Arusha. Mahakama ya Rufani imethibitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa Razaki Sadiki, aliyepatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu, ikisema ushahidi uliobaki baada ya kuondoa vielelezo viwili ulitosha kuthibitisha kosa hilo.
Katika hukumu iliyotolewa Oktoba 23, 2026 na kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama, majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Mary Levira, Zainab Muruke na Lameck Mlacha, walisema dosari za kisheria katika maelezo mawili ya kukiri hazikuondoa nguvu ya ushahidi mwingine uliowasilishwa mahakamani.
Majaji hao walisema ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashtaka, pamoja na ripoti ya uchunguzi wa daktari, uliendelea kuthibitisha kosa dhidi ya mshtakiwa.
“Rufaa hii imeonekana kutokuwa na msingi na inatupiliwa mbali,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.
Awali, katika Mahakama ya Wilaya ya Kondoa, Razaki alishtakiwa kwa kosa la ulawiti kinyume na kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa kuwa Oktoba 4, 2023, katika Kijiji cha Keikei, Wilaya ya Kondoa, alimlawiti mtoto huyo.
Baada ya kusikiliza mashahidi watano wa upande wa mashtaka na watatu wa utetezi, mahakama ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha maisha jela. Alikata rufaa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, ambayo ilitupilia mbali rufaa yake.
Mama wa mtoto huyo, ambaye alikuwa shahidi wa kwanza, alieleza kuwa alikuwa akiishi katika nyumba inayomilikiwa na baba wa mrufani. Alisema siku ya tukio alipofika nyumbani, mtoto wake alimweleza ukatili aliofanyiwa.
Alipomuuliza mrufani kuhusu tukio hilo, mama huyo alisema alimjibu, “Sorry madame.”
Baadaye, mama huyo alitoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata, kisha polisi walimpa fomu ya polisi namba tatu (PF3) na kumpeleka mtoto Hospitali ya Kondoa kwa uchunguzi.
Dk Samwel George, aliyemchunguza mtoto Oktoba 5, 2023, alisema alibaini njia ya haja kubwa ikiwa imepanuka na kuwa na michubuko iliyoashiria kuingiliwa.
Katika rufaa yake, Razaki alilalamikia, pamoja na mambo mengine, kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha, tofauti ya tarehe ya tukio na uhalali wa maelezo ya kukiri yaliyotumika dhidi yake.
Jamhuri, kupitia Wakili wa Serikali, iliunga mkono rufaa hiyo kuhusu hoja ya udhaifu wa ushahidi na namna maelezo hayo yalivyoingizwa mahakamani.
Maelezo mawili yaondolewa
Katika kupitia mwenendo wa kesi na hoja za pande zote, majaji walibaini kuwa hakukuwa na ushahidi unaoonyesha Ofisa Mtendaji wa Kata aliyerekodi maelezo ya kukiri alikuwa ameteuliwa na kupewa mamlaka ya kufanya kazi kama Hakimu wa Amani katika Mahakama ya Mwanzo.
Mahakama pia ilibaini kuwa maelezo hayo yaliandikwa ofisini kwake badala ya katika eneo la mahakama.
“Kwa kuwa hakukuwa na ushahidi kwamba shahidi wa tatu aliteuliwa na kupewa mamlaka ya kufanya kazi kama Jaji wa Amani katika Mahakama ya Mwanzo, yote aliyoyafanya yalibaki kuwa kinyume cha sheria kwa sababu hakuwa na mamlaka ya kufanya kazi hiyo.”
Kwa msingi huo, mahakama iliamuru maelezo hayo yaliyokuwa kielelezo cha pili, yaondolewe kwenye kumbukumbu za kesi.
Kuhusu maelezo ya onyo yaliyoandikwa polisi, majaji walibaini kuwa kumbukumbu hazikuonyesha muda ambao Razaki aliwasili kituoni. Hali hiyo ilifanya isiwezekane kuthibitisha kama maelezo hayo yaliandikwa ndani ya muda unaotakiwa kisheria.
Majaji walisema jukumu la kuthibitisha muda huo lilikuwa kwa upande wa mashtaka, ambao haukulitekeleza, hivyo kuondoa kielelezo hicho kwenye kumbukumbu za kesi.
“Kwa kutokuwepo kwa ushahidi kuhusu muda ambao alifika katika Kituo cha Polisi, hatuwezi kukubaliana na Wakili wa Serikali kwamba maelezo ya tahadhari yaliandikwa nje ya muda uliowekwa.”
Ushahidi uliobaki wathibitisha kosa
Baada ya kuondoa vielelezo hivyo viwili, mahakama ilichunguza ushahidi mwingine uliobaki, ukiwemo maelezo ya mama wa mtoto, ushahidi wa daktari na mashahidi wengine wa upande wa mashtaka.
Majaji walisema ushahidi huo ulithibitisha umri wa mtoto, kitendo kilichofanyika na utambulisho wa aliyekitenda. Pia walibaini kuwa mtoto alimfahamu Razaki, huku mama yake akieleza namna alivyofahamishwa kuhusu tukio hilo na ushahidi wa daktari ukiunga mkono madai ya kuingiliwa kwa mtoto.
Kuhusu tofauti ya tarehe, mahakama ilisema maelezo ya mama wa mtoto yaliyotaja Oktoba 3, 2023, badala ya Oktoba 4, iliyokuwa kwenye shtaka, yalikuwa mkanganyiko mdogo ambao haukuathiri kesi ya mashtaka.
Majaji walieleza kuwa ushahidi mwingine uliweka mfuatano wa matukio ulioonyesha kosa lilitendeka Oktoba 4, 2023.
Kwa kuzingatia ushahidi huo, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa ya Razaki na kuthibitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kondoa.
You may also like

Malaria kwa wajawazito yashuka Tanzania, sababu zatajwa

Wapiga kura wa Netanyahu waanza kumgeuka


Leave a Reply