

Wafanyabiashara Soko la Dampo walalama gharama za vyoo, Meya ajibu
Mwanza. Wafanyabiashara wa Soko la Dampo, lililopo Buhongwa jijini Mwanza, wameiomba Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuboresha huduma za usafi na kupunguza gharama za matumizi ya vyoo, wakieleza kuwa hali hiyo inawaongezea gharama za uendeshaji wa biashara zao zenye mitaji midogo.
Wafanyabiashara hao wametoa malalamiko hayo leo Jumatano Oktoba 21, 2026, wakati wa ziara ya Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima, aliyefika sokoni hapo kusikiliza kero zao na kutafuta namna ya kuzitatua.
Miongoni mwa changamoto walizozitaja ni magari ya kuzoa taka kufika sokoni wakati wa mchana, uchafu unaozidi kuwa kero wakati wa mvua na gharama za matumizi ya vyoo, ambazo wanasema ni kubwa kwa uwezo wao.
Mfanyabiashara, Mganisi Joseph amesema magari ya kuzoa taka yamekuwa yakifika wakati wafanyabiashara wakiendelea na shughuli zao, hali inayowasumbua na kuathiri hata muda wao wa kula.
“Yanakuja muda wa mchana tunapokuwa tunafanya biashara na ukitazama kwa miji mikuu yote huwa wanaondoa taka usiku, siyo mchana. Tunashindwa kula,” amesema.
Ameongeza kuwa uchafu katika soko hilo huwa kero zaidi wakati wa mvua, hivyo akaitaka halmashauri kuchukua hatua za kuboresha usafi na mazingira ya soko.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Mwajuma Abdallah amesema ada ya Sh300 kwa kila matumizi ya choo ni kubwa kwa wafanyabiashara wenye mitaji midogo, hasa wale wanaotumia huduma hiyo mara kadhaa kwa siku pamoja na watoto wanaokuja nao sokoni.
Amesema gharama hizo zinawaongezea mzigo wa matumizi ya kila siku, huku akiiomba Serikali kupunguza ada hiyo hadi Sh200 kwa kila matumizi.
“Mitaji yetu midogo na tunafanya biashara kwa kushinda humu na watoto. Watoto wakienda ni Sh300, wewe mkubwa ukienda ni Sh300, unakuta hata mara tatu. Inafika sehemu hata wewe hujala,” amesema.
Ameongeza: “Tunaomba Serikali itusaidie kutufanyia utaratibu wa kutupunguzia bei ya choo, angalau watufanyie hata Sh200 kwa kila huduma ya choo inayopatikana kwa mfanyabiashara.”
Mfanyabiashara wa Soko la Dampo, Mganisi Joseph akimweleza Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima kero ya magari ya kuzoa taka kufika sokoni wakati wa mchana wafanyabiashara wanapoendelea na shughuli zao.
Akijibu kero hizo, Sima amemtaka Mtendaji wa Kata kuongeza usimamizi kwa mzabuni anayehusika na ukusanyaji wa taka ili kuhakikisha huduma hiyo inafika katika maeneo yote yaliyokusudiwa, yakiwemo yale ambayo hayapati huduma hiyo ipasavyo.
Kuhusu mpango wa kuwahamisha wafanyabiashara hao, Sima amesema hatua hiyo inatokana na sababu za kiafya, akisisitiza kuwa wafanyabiashara waliopo wanapaswa kupewa kipaumbele katika soko jipya linalotarajiwa kujengwa.
“Soko hili linahama, sababu walengwa wakubwa kwanza ni nyinyi. Tunawaondoa humu kwa sababu kubwa ya kiafya. Haitakuwa na maana tunaenda kuwahamisha lakini kipaumbele akapata mtu mwingine,” amesema.
Amesema halmashauri imeandaa eneo rasmi litakalowawezesha wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao, huku ikipanga kuwekeza katika miundombinu inayozingatia mahitaji yao na watumiaji wengine wa soko.
“Sisi kama Halmashauri ya Mwanza, kupitia vikao vyetu vya mabaraza, tuliona ni vema tuweze kuandaa eneo rasmi ambalo mtaweza kukaa. Kwanza ni eneo ambalo litawasaidia nyinyi na biashara zenu, lakini pili litakuwa eneo ambalo tutaenda kuwekeza na kuweka miundombinu ambayo itakuwa rafiki kwa watumiaji wa soko,” amesema.
Taka zilizokusanywa katika Soko la Dampo, Buhongwa jijini Mwanza zikiwa tayari kumwagwa, huku wafanyabiashara wakilalamikia changamoto za usafi na muda wa magari ya kuzoa taka kufika sokoni hapo.
Kuhusu malalamiko ya gharama za vyoo, Sima amesema halmashauri ina wajibu wa kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kuboresha miundombinu na kutoa huduma zinazostahili kwa wananchi.
Amesema malipo yanayofanywa na watumiaji yanapaswa kuendana na ubora wa huduma wanazopata, akisisitiza kuwa wananchi wana haki ya kupata huduma nzuri wanapolipia.
“Kama tunatoza ushuru kwenye choo, unalipia, tunasema kuna wajibu na haki. Tunasema ni wajibu wako kutoa, lakini ni haki yako kupata huduma nzuri,” amesema.
Ameongeza kuwa halmashauri inapaswa kuwajibika katika matumizi ya mapato yanayokusanywa kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii, akieleza kuwa wananchi hawapaswi kuendelea kulipa bila kuona maboresho ya miundombinu husika.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa halmashauri kuhakikisha mapato hayo yanatumika kurekebisha na kuboresha huduma ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Dampo wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero zao na kueleza hatua zinazochukuliwa kuboresha huduma za usafi, vyoo na mazingira ya soko jipya.
Katika hatua nyingine, Sima ametembelea mradi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wa kufyatua matofali, uliogharimu zaidi ya Sh129 milioni, kwa lengo la kukagua hatua iliyofikiwa na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Amesema ukaguzi huo unalenga kutathmini maendeleo ya mradi na kubaini maboresho yanayohitajika katika kipindi hiki cha maandalizi ya kuongeza vyumba vya madarasa.
You may also like

Mtanzania atwaa tuzo ya vijana 100 wa Jumuiya ya Madola

Tanzania mwenyeji mkutano waa maadili ya biashara Afrika


Leave a Reply