

AFD yaipa Tanzania mkopo nafuu wa Sh513 bilioni
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimesaini mikataba mitatu ya mikopo nafuu yenye thamani ya euro milioni 175 (Sh513 bilioni), inayolenga kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira, miundombinu ya biashara ya chakula na uzalishaji wa maziwa kwa wafugaji wadogo.
Fedha hizo zimeelekezwa katika miradi mitatu inayogusa sekta muhimu za maisha na shughuli za kiuchumi za wananchi hususan katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria na miji ya Mwanza na Tanga pamoja na maeneo ya wafugaji wadogo.
Kusainiwa kwa mikataba hiyo jijini Paris, Ufaransa, thamani ya jumla ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na AFD imefikia euro 1.3 bilioni (Sh trilioni 3.81).
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar na Mkurugenzi Mkuu wa AFD, Christophe Lecourtier ndio waliotia saini mikataba hiyo katika makao makuu ya shirika hilo.
Mkataba wenye thamani kubwa zaidi ni ule wa euro milioni 90 (Sh bilioni 263.8), unaofadhili awamu ya pili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria (LV WATSAN II).
Mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa maji na huduma za usafi wa mazingira kwa jamii zinazoishi katika maeneo hayo. Ufadhili huo utaongezewa ruzuku kutoka Umoja wa Ulaya itakayosimamiwa na AFD.
Akizungumzia umuhimu wa mikataba hiyo, Waziri Khamis alisema manufaa yake yanapaswa kuonekana katika utekelezaji wa miradi na huduma zitakazowafikia wananchi.
Amesema familia zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria, watafikiwa na upatikanaji bora wa huduma za maji na huduma za usafi wa mazingira.
“Kwa wafanyabiashara wa chakula Mwanza na Tanga itasaidia kuboreshwa kwa miundombinu ya kufanyia biashara huku wafugaji wadogo wakitarajiwa kunufaika na uwezo ulioimarishwa wa kuendeleza uzalishaji licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi.,” amesema.
Mkataba wa pili wenye thamani ya euro milioni 55 (Sh bilioni 161.2) unalenga kuboresha miundombinu ya biashara na usambazaji wa chakula katika miji ya Mwanza na Tanga kupitia Programu ya Uwekezaji Endelevu katika Mifumo ya Chakula Mijini (TASUFIP).
Programu hiyo inalenga kuimarisha miundombinu inayohudumia shughuli za biashara ya chakula, eneo ambalo lina umuhimu katika usambazaji wa bidhaa hizo mijini. Kama ilivyo kwa mradi wa maji, ufadhili wake utaongezewa ruzuku ya Umoja wa Ulaya kupitia AFD.
Mkataba wa tatu wenye thamani ya euro milioni 30 (Sh bilioni 87.9) utaelekezwa katika Programu ya Kuendeleza Ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa kwa Wafugaji Wadogo kwa Kuzingatia Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP).
Programu hiyo inayofadhiliwa kwa pamoja na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), inalenga kusaidia wafugaji wadogo kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kikao cha utiaji saini kilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakubu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Asha Khamis Abdulla, na Kamishna wa Fedha za Nje, Rished Bade.



Leave a Reply