

Wadau wapendekeza mifumo mipya kudhibiti bodaboda, bajaji
Dar es Salaam. Wadau wa usafirishaji wameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuimarisha usimamizi wa shughuli za bodaboda na bajaji kwa kuweka mifumo madhubuti ya usajili, mafunzo, ukaguzi na ufuatiliaji wa madereva ili kupunguza makosa na ajali barabarani.
Wakichangia mada mbalimbali katika maadhimisho ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2026, yaliyofanyika Novemba 25, 2026, wadau hao wamesema pamoja na umuhimu wa kutoa elimu kwa waendesha pikipiki na bajaji mamlaka zinapaswa kuhakikisha vyombo vinavyotumika kusafirisha abiria vinakidhi vigezo vya usalama na wanaokiuka sheria wanachukuliwa hatua.
Wamependekeza pia matumizi ya teknolojia katika ufuatiliaji wa pikipiki na bajaji kuimarishwa kwa vituo vyao na kuanzishwa kwa utaratibu wa kuwataka madereva kujiunga na vikundi ili kurahisisha usimamizi wao.
Mdau wa usafirishaji Meshack Mmelake amesema kuna umuhimu wa kuimarisha ukaguzi wa madereva ili kubaini wanaotumia vilevi wanapokuwa kazini, baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji hutumia vilevi, hali inayoweza kupunguza umakini wanapokuwa barabarani na kuongeza uwezekano wa ajali.
“Kuna umuhimu wa kutofautisha kati ya mtu anayejua kuendesha pikipiki na dereva mwenye mafunzo rasmi ya udereva, yupo mtu amejifunza kwa mwenzake, amejua kuendesha lakini si dereva, kwa sababu hana elimu au taaluma ya udereva,” amesema Mmelake.
Kuhusu usimamizi wa vituo, ameshauri vituo vya bodaboda na bajaji vinavyosajiliwa na halmashauri kuingizwa katika mfumo maalumu utakaowezesha kufuatilia waendesha pikipiki wanaofanya kazi katika maeneo hayo.
Amesema utaratibu huo utasaidia viongozi wa vituo kuwafahamu wanachama wao na kushirikiana na mamlaka kutoa elimu, kufuatilia mienendo yao na kuwajibishana pale mmoja anapokiuka taratibu.
Katika hoja nyingine, amesema umuhimu wa kutoa elimu kwa vijana wanaoendesha bodaboda na bajaji, akisema juhudi hizo zinapaswa kuanzia katika familia na kuendelezwa katika jamii kupitia vikundi vya waendesha vyombo hivyo.
Wadau wa usafirishaji wakiendelea na midahalo mbalimbali katika Maadhimisho ya Wiki ya Usafiri endelevu ardhini 2026 yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema vijana wengi huanza shughuli hizo wakiwa na umri mdogo na bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu hatari za barabarani, hivyo kujiunga katika vikundi kutasaidia kurahisisha upatikanaji wa elimu na usimamizi wao.
“Badala ya Latra kuanza kufuatilia kila mmoja mmoja kila mahali, tuanze kufikiria kuweka kwenye vikundi ili iwe rahisi kuwafikia kwa pamoja , ushirikiano kati ya mamlaka, familia, jamii na viongozi wa vikundi unaweza kusaidia kujenga utamaduni wa kuzingatia sheria na usalama barabarani,”amesema.
Kwa upande wake, mdau wa usafirishaji na teknolojia, Nickson Dawson, amesema ongezeko la pikipiki linahitaji kuendana na mifumo mipya ya usimamizi na teknolojia inayoweza kuboresha usalama na ufanisi wa huduma hizo.
Amesema kwa takwimu walizozichambua, Dar es Salaam pekee kuna zaidi ya pikipiki 32,000, bila kujumuisha vyombo vya magurudumu matatu, maarufu kama bajaji.
Dawson amesema pikipiki nyingi zinazoingia nchini zinatoka China na India, huku mabadiliko ya teknolojia yakitoa fursa ya kuanza kutumia pikipiki zinazotumia umeme badala ya mafuta.
“Bodaboda akiwa na hii pikipiki hatazunguka kutafuta sehemu ambayo anaweza akaweka mafuta, inakuwa rahisi kupata sehemu ambayo anaweza kufanya swapping technology,” amesema.
Kwa upande wake dereva wa bodaboda na mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Erick Tarimo amesema usalama wa waendesha bodaboda na abiria unapaswa kupewa kipaumbele kwa kuhakikisha pikipiki zinazotumika kibiashara zinakuwa na vifaa muhimu vya usalama.
Amesema baadhi ya pikipiki hazina vioo vya pembeni vinavyomwezesha dereva kuona vyombo vinavyotoka nyuma.
“Kutoa elimu kwa madereva pekee hakutoshi bila kuhakikisha usalama wa vyombo wanavyotumia unazingatiwa hali hiyo inaweza kuongeza hatari ya ajali, ambazo zinapotokea madereva na abiria wanaweza kupata majeraha ya kichwa, miguu na mikono,” amesema Tarimo.
Akijibu maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau hao, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Latra, Abdallah Mhagama amesema matumizi ya teknolojia katika pikipiki yanaweza kurahisisha ufuatiliaji wa vyombo hivyo na kuwasaidia wasimamizi kujua vilipo.
Hata hivyo, amesema changamoto iliyopo ni baadhi ya waendesha bodaboda kukimbia wanapofanya makosa, hali inayoongeza gharama na ugumu wa kuwafuatilia na kuwakamata.




Leave a Reply