

Doroth: ACT Wazalendo ndio kimbilio na matumaini ya Watanzania
Pemba. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu, amesema ushirikiano miongoni mwa viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya Taifa, mikoa na majimbo utaendelea kuimarishwa kwa lengo la kukijenga na kukifanya kiwe imara zaidi.
Amedai chama hicho ndicho kilichobeba matumaini ya Watanzania na kinaelekea kuwa kimbilio namba moja kwa wananchi.
Doroth amesema hayo jana Jumamosi, Oktoba 31, 2026, wakati wa Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Wete Kichama, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema chama hicho kimekuwa kikitekeleza shughuli zake kwa uwazi na uwajibikaji, hali ambayo, kwa mujibu wake, imeendelea kuwavutia Watanzania wengi kujiunga nacho.
“Chama cha ACT Wazalendo ni chama ambacho kimebeba matumaini ya Watanzania na kinaelekea kuwa kimbilio namba moja kwa wananchi wa Tanzania,” amesema Doroth.
Ameongeza kuwa viongozi wa chama hicho wana wajibu wa kuwafahamisha wananchi na wanachama kuhusu maendeleo na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na chama.
Amewasisitiza wanachama na viongozi katika ngazi zote kuendelea kushirikiana ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu na kufikia malengo ya chama.
Wete imara licha ya changamoto za kifedha
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Wete Kichama, Juma Khamis Ali, amesema chama katika mkoa huo kinaendelea kuwa imara licha ya kukabiliwa na changamoto za kifedha zinazotokana na kupata viti vichache vya ubunge na uwakilishi.
Juma amesema mkutano huo umefanyika baada ya kukamilika kwa mikutano mikuu ya matawi 120, iliyofuatwa na mikutano ya majimbo matano kabla ya kufanyika kwa mkutano wa mkoa.
Mratibu wa ACT Wazalendo Kisiwani Pemba, Rashid Ali Abdallah, amesema chama hicho kisiwani humo kinaendelea kuwa imara.
Katibu wa chama hicho Mkoa wa Wete Kichama, Masoud Juma amesema mkutano huo ni halali kwa mujibu wa Katiba ya chama, baada ya kuhudhuriwa na wajumbe 75 kati ya 90 waliotarajiwa.
Kabla ya kuhudhuria mkutano huo, Doroth alikagua jengo la ghorofa tatu la Ofisi ya Mkoa wa Wete Kichama, ambalo hadi sasa ghorofa mbili zimekamilika.
Katika ziara hiyo, pia alipata fursa ya kutoa pole kwa familia ya aliyekuwa mtendaji wa chama katika Ofisi ya Mratibu Kisiwani Pemba, Husna Hemed Salum, aliyefariki dunia mapema wiki hiyo.
Ziara hiyo imehitimishwa baada ya kiongozi huyo wa ACT Wazalendo kukamilisha ziara ya kikazi ya siku mbili kisiwani Pemba, iliyolenga kukagua na kujionea maendeleo ya chama, hususan katika Mkoa wa Wete Kichama.
You may also like

Ushahidi mtoto wa miaka mitatu wamfunga maisha

Chadema yaweka masharti kushiriki maridhiano


Leave a Reply