

Kasekenya aagiza Tanroads kuweka wakandarasi wa dharura mvua za El Nino
Same. Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amewaagiza mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mikoa yote nchini kuhakikisha wanaweka wakandarasi wa dharura katika maeneo yao ili kukabiliana na athari za mvua za El Nino zinazoweza kuathiri barabara kuu.
Kasekenya amesema maandalizi hayo ni muhimu ili kuwezesha matengenezo ya haraka pale miundombinu ya barabara itakapoharibiwa na mvua hizo, kwa lengo la kuzuia madhara yanayoweza kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara, uharibifu wa mali na watu kupoteza maisha.
Ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 23, 2026, alipokuwa akikagua daraja la Makanya, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, ambalo kwa miaka mingi limekuwa likikatika wakati wa mvua na kusababisha kukatika kwa mawasiliano katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Tanga – Same – Arusha.
Pamoja na kukagua madaraja katika Wilaya ya Same, amekagua mitaro mikubwa inayojengwa katika barabara kuu ya Himo – Holili inayounganisha nchi ya Tanzania na Kenya katika mpaka wa Holili, wilayani Rombo.
Aidha, Kasekenya amesema Mameneja wa Tanroads wanapaswa kuhakikisha wakandarasi wanapatikana katika barabara wanazosimamia ili waanze kazi mara moja changamoto zitapojitokeza.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, akizungumza wakati akikagua daraja la Makanya, wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro ambalo limekuwa likiathiriwa na mafuriko ya mvua na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara kuu ya Dar es salaam-Tanga- Same-Moshi-Arusha.
“Ni muhimu tuwe tayari muda wote, tuwe na wakandarasi katika kila barabara ambayo watakaa tayari inapotokea changamoto wanakuwa na utayari wa kuingia na kurekebisha pale changamoto zinapotokea,” amesema Kasekenya.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona dalili za kuharibika kwa miundombinu ya barabara, ikiwemo kwa viongozi wa Serikali za mitaa, madiwani, wakuu wa wilaya na mikoa pamoja na vyombo vya usalama.
Amesema taarifa hizo zitasaidia mamlaka husika kuchukua hatua za haraka hata pale ambapo watendaji wa barabara hawajabaini changamoto hizo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, akizungumza na wataalam wa Tanroads na Wakandarasi wakati alipokuwa akikagua mtaro mkubwa wa maji unaojengwa katika barabara kuu ya Moshi-Himo-Holili.
Katika hatua nyingine, Kasekenya amewataka mameneja hao kupunguza matawi katika miti mikubwa iliyo hatarini kuanguka kandokando ya barabara, hasa barabara za mikoa, ili kuzuia miti hiyo kuanguka na kuziba barabara au kusababisha ajali wakati wa mvua na upepo mkali.
Amesema maeneo mengi nchini yana miti mikubwa kandokando ya barabara, hivyo ni muhimu kufanya tathmini na maandalizi ya mapema ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Benito Mdzovera amesema matengenezo ya daraja la Makanya wilayani Same yamegharimu Sh150 milioni, baada ya kubainika kuwa maji yalikuwa yamechimba udongo chini ya daraja hilo na kuondoa sehemu ya msingi iliyokuwa ikiliimarisha daraja hilo.
Amesema hali hiyo ilikuwa tishio kwa usalama wa daraja na barabara hiyo muhimu ambayo ina unganisha mikoa ya kanda ya Kaskazini.
Amesema katika wilaya hiyo, maeneo mengine yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na daraja la mabilioni, ambako kumewekwa vikapu vya chuma pamoja na mawe, eneo la Hedaru na Stendi ya Miwa iliyopo Wilaya ya Mwanga, ambako madaraja hayo yalikuwa yamefukiwa na udongo na kushindwa kupitisha maji.
Daraja la Makanya, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro ambalo limefanyiwa ukarabati kutokana na kuathiriwa na mafuriko ya mvua.
“Katika Wilaya ya Same, daraja la Hingilili kwenye barabara ya Same – Kisiwani – Mkomazi nalo limefanyiwa matengenezo baada ya udongo kujaa na kupunguza uwezo wa daraja kupitisha maji,” amesema.
Katika maandalizi ya dharura, Mdzovera amesema mkoa huo umehifadhi daraja la chuma lenye urefu wa mita 20 na makalavati ya chuma yenye jumla ya mita 240, yanayoweza kutumika kutengeneza angalau makalavati 30 ili kurejesha mawasiliano pale miundombinu inapoharibika.
Naye, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni amesema kati ya asilimia 65 na 70 ya eneo la Wilaya ya Same lina milima, huku wananchi wengi wakiishi katika maeneo hayo, ambapo amesema kipindi cha mvua kubwa husababisha maporomoko ya ardhi, mawe na miti ambayo husombwa na maji mpaka kwenye barabara.
Ametoa wito kwa wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu na viongozi wa Serikali kuhusu maeneo wanayotakiwa kuyaepuka, akisisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kulinda maisha yao.
You may also like

Wabeba mizigo hatarini kupata matatizo ya mgongo, nyonga

UDSM yaadhimisha miaka 65 kwa elimu, tafiti, uhifadhi mazingira


Leave a Reply