

Magari yaongezeka, usalama barabarani shakani
Dar es Salaam. Ongezeko la magari nchini limeanza kuongeza shinikizo kwenye miundombinu ya barabara, huku ajali zikizidi kuongezeka na kuibua wito wa kuimarisha usimamizi, matumizi ya teknolojia na uwekezaji katika usalama wa watumiaji.
Hali hiyo inajidhihirisha katika takwimu za Jeshi la Polisi zinazoonyesha ajali zilizoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026 ziliongezeka kwa asilimia 20.2, kutoka 642 mwaka 2025 hadi 772.
Katika kipindi hicho, ajali zilizosababisha vifo ziliongezeka kutoka 443 hadi 500, huku idadi ya waliofariki ikipanda kutoka 640 hadi 663. Hata hivyo, majeruhi walipungua kutoka 1,100 hadi 1,007.
Jeshi la Polisi limetaja mwendokasi, kuyapita magari bila tahadhari, hitilafu za magari, ubovu wa barabara na kutowajali watumiaji wengine kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia ajali hizo.
Kutokana na hali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa kudhibiti makosa ya barabarani, akielekeza kukamilishwa kwa Mradi wa Miji Salama (Safer Cities).
Rais alitoa msisitizo huo Novemba 20, 2026, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro. Pia alihimiza utoaji wa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri, hususan madereva wa bodaboda.
Suala la usalama barabarani limeendelea kupewa uzito na Serikali, huku Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, akieleza kuwa athari za ajali haziishii kwenye vifo na majeraha, bali huacha familia katika majonzi, watoto yatima na Taifa kupoteza nguvu kazi.
Akizungumza jana Jumatatu, Novemba 23, 2026, wakati akifungua kongamano la usalama barabarani Afrika 2026 lililoandaliwa na Taasisi ya Mpango wa Usalama Barabarani (Tarsi), jijini Dar es Salaam, Kihenzile alisema ni muhimu kuchunguza kwa kina sababu za ajali na ufanisi wa mifumo iliyopo ya kuzuia matukio hayo.
Alitaka wadau kujiuliza kama adhabu zinazotolewa zinatosha, mifumo ya usimamizi inafanya kazi na kama miundombinu pamoja na utekelezaji wa sheria vina changamoto.
“Muhimu kujiuliza dereva anajisikiaje anapohatarisha maisha ya abiria 60 waliopanda gari kwa lengo la kwenda kutafuta riziki na kusaidia familia zao, lakini kutokana na uzembe wake baadhi yao wanapoteza maisha au kupata ulemavu,” alisema.
Alisema Serikali inaendelea kutoa elimu, kudhibiti maeneo yenye ajali nyingi na kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaokiuka sheria, huku akilitaka Jeshi la Polisi kuwawajibisha madereva wazembe.
Mbali na tabia za madereva, Kihenzile alitaja ongezeko la magari dhidi ya miundombinu iliyopo kuwa changamoto nyingine inayohitaji kushughulikiwa.
Alisema baadhi ya barabara zimeelemewa na idadi ya magari kutokana na kutopanuliwa kwa miundombinu hiyo ili kuendana na mahitaji yanayoongezeka.
Akitoa mfano wa Barabara ya Tanzam, alisema magari yaliyokuwa yakitoka nje ya nchi yalikuwa 53,000 mwaka 2021, lakini idadi hiyo iliongezeka hadi 180,000 mwaka 2026.
Aidha, alisema magari yaliyosajiliwa nchini yaliongezeka kutoka 123,000 hadi 287,000 mwaka 2025, wakati miundombinu ya barabara ikiendelea kuwa ileile.
Wakati changamoto hiyo ikiendelea kujitokeza, uzoefu wa Zanzibar unaonyesha namna teknolojia inavyoweza kutumika kufuatilia na kudhibiti ukiukaji wa sheria za barabarani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Ardhi na Tehama ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mwakilishi wa Mwera, Mihayo Juma N’hunga, alisema ufungaji wa kamera za CCTV katika barabara kuu umesaidia kudhibiti makosa ya barabarani.
Alisema kamera hizo zimeunganishwa na mfumo wa usajili wa magari pamoja na taarifa za wamiliki, hivyo dereva anapokiuka sheria anaweza kupokea ujumbe mfupi ndani ya dakika tano ukimweleza kosa alilofanya.
“Lengo siyo kwenda kukusanya mapato, lengo ni kusaidia madereva wanapokuwa wanaendesha wawe katika mazingira ya usalama,” alisema.
N’hunga alisema katika takribani miezi sita tangu hatua hizo zianze kutekelezwa, ajali zisizo za lazima mijini zimepungua kwa kiwango kikubwa.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuchunguza maeneo yanayokumbwa na ajali nyingi ili kubaini kasoro za miundombinu na alama za barabarani zinazoweza kuchangia matukio hayo.
Kwa upande wa miundombinu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tarsi, Bariki Barongo, alisema elimu ya usalama barabarani haipaswi kuishia kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara, bali inapaswa kuwafikia pia wahandisi na wajenzi.
Alisema ni muhimu masuala ya usalama kuzingatiwa kuanzia hatua za usanifu hadi ujenzi wa barabara ili kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali.
Aliongeza kuwa ajali husababisha upotevu wa nguvu kazi na kuharibu miundombinu ambayo Serikali hutumia fedha nyingi kuijenga na kuitengeneza.
Kwa mtazamo wa afya ya umma, Ofisa Mahusiano ya Nje wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Humayun Salim, alisema usalama barabarani si suala la usafiri pekee, bali ni changamoto inayogusa afya ya jamii na maendeleo.
Alisema takwimu za WHO zinaonyesha takribani watu milioni 1.16 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, huku majeraha yatokanayo na ajali hizo yakiwa chanzo kikuu cha vifo kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka mitano hadi 29.
Alisema Afrika inachangia takribani asilimia 19 ya vifo hivyo duniani.
Salim alitaja Mpango wa Muongo wa Hatua za Usalama Barabarani wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2021 hadi 2030 kuwa na lengo la kupunguza vifo na majeraha kwa angalau asilimia 50, akizitaka nchi za Afrika kuimarisha mikakati na ushirikiano ili kufikia lengo hilo.
You may also like

Tanzania: What Two Global Outages Mean for Tz’s Digital Finance

Ushahidi mtoto wa miaka mitatu wamfunga maisha


Leave a Reply